ANGALIA LIVE NEWS

Monday, May 9, 2016

UKAWA WAIGOMEA SERIKALI KUHAMISHWA MACHINGA KATIKATI YA JIJI LA DAR ES SALAAM

Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Isaya Mgurumi
 
Sakata la kuhamishwa kwa wafanyabiashara wadogo katikati ya Jiji la Dar es Salaam limeingia mdudu baada ya madiwani wa Ukawa kugomea uamuzi uliotolewa na uongozi wa jiji hilo.

Uamuzi huo uliotolewa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Isaya Mngurumi, unadaiwa kutowashirikisha wadau hao na wafanyabiashara wenyewe.

Mwenyekiti wa madiwani wa Ukawa, Manase Mjema amesema Mngurumi ametoa uamuzi huo bila pia kumshirikisha hata Meya wa Ilala, Charles Kuyeko.

Wamesema masoko ya Kivule, Tabata Muslim, Ukonga na Kigogo Fresh ambayo mkurugenzi huyo amesema yametengwa kwa ajili ya wafanyabiashara hao, hayajaboreshewa miundombinu yake ikiwamo ujenzi wa vyoo na mabomba ya maji.

Wamemtaka kusitisha mchakato huo mpaka watakapo jadiliana tena


“Ieleweke kwamba hatupingi hatua hii, lakini Mngurumi alipaswa kutushirikisha madiwani ili tutoe mawazo ambayo yangesaidia kuboresha mpango wake huu,” alisema Mjema.


Alisema Mngurumi angetumia busara ya kushirikiana na baraza la madiwani na angewapa muda wafanyabiashara hao kujiandaa, tofauti na muda wa siku mbili aliowapa kuondoka kwenye maeneo hayo.

“Tulitegemea mkurugenzi angekaa na madiwani na wafanyabiashara meza moja ili kutoa uamuzi ambao ungekuwa na tija kwa pande zote, badala ya kukurupuka kama alivyofanya,” alisema Mjema ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kimanga (Chadema).

Kwa upande wake, Kuyeko alidai kupewa maagizo na Mngurumi jana kuitisha mkutano na wanahabari ili kukazia agizo hilo.

Hata hivyo, meya huyo alishindwa kufanya hivyo kwa madai ya kutoshirikishwa.

“Nilisita kuunga mkono uamuzi wake kwa sababu baraza langu la madiwani halijui kinachoendelea zaidi ya kusikia katika vyombo vya habari,” alidai Kuyeko.

Diwani wa Kata ya Tabata (Chadema), Patrick Asenga ambaye eneo lake limetengwa kwa ajili ya wafanyabiashara hao, alisema hawezi kuwapokea kwa sababu eneo hilo lina mgogoro na halmashauri.

Mjumbe wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Wadogo, Idd Omary alisema wamekubaliana kutohamia katika masoko waliyopangiwa kwa sababu hawakushirikishwa katika mchakato wote na Mkurugenzi huyo.

“Mngurumi alimtuma mwakilishi katika kikao cha jana (juzi), kilichotukutanisha na uongozi wa Manispaa ya Ilala. Tulimuuliza masoko waliyotupangia yana miundombinu mizuri, tukajibiwa ndiyo, lakini siyo kweli, hayana vyoo wala maji,” alidai Omary.

Akizungumzia madai ya madiwani hao, Mngurumi alisema anashangazwa na kauli zao kwani kuna mambo walikubaliana na Meya Kuyeko ambayo hakuyataja na badala yake alisema atawasiliana naye kwa mara nyingine kwa mazungumzo zaidi.

1 comment:

Anonymous said...

Ingekuwa vizuri kama mwandishi utatuwekea chama kwenye mabano ni chama gani anatoka. anapotoka huyo kiongizi(mkurugenzi) kama hivi:mkurugenzi wa manispaa ya ilala ndugu...(ccm)au