Monday, May 9, 2016

WADAU WA MAJI KUJADILI RASILIMALI ZA BONDE LA MTO RUFIJI


Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO

Wizara ya Maji na Umwagiliaji imeandaa warsha kwa wadau wake juu ya tathmini ya kimkakati ya athari za kimazingira na jamii juu ya mpango jumuishi wa usimamizi na maendeleo ya rasilimali maji za bonde la Mto Rufiji zitakayofanyika Jijini Dar es salaam na mkoani Iringa.

Taarifa hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhandisi Mbogo Futakamba alipokua akifafanua kuhusu mpangilio wa warsha hizo zitakazofanyika katika mikoa miwili ambapo kwa Jijini Dar es salaam warsha hiyo itafanyika Mei 20 mwaka huu na mkoani Iringa itafanyika Mei 23 mwaka huu kuanzia sa 3 kamili asubuhi hadi sa 10:30 jioni.

"Wizara yetu inawakaribisha wadau wake wote kushiriki warsha hii na mada zitakazotolewa zitahusisha maelezo ya jumla juu ya mipango ya maendeleo ya muda mrefu ya rasilimali za maji ya bonde la mto Rufiji na athari zake tarajiwa za kimazingira na kijamii, kuwapa fursa ya kutoa maoni na mitazamo yao juu ya mipango inayokusudiwa pamoja na kutoa ufafanuzi kuhusu maamuzi na taratibu zinazofuata,"alisema Mhandisi Futakamba.

Aidha, Mhandisi Futakamba ameongeza kuwa warsha hizo zitaandaliwa na kuwezeshwa na washauri elekezi kutoka Kampuni ya uingereza ijulikanayo kama Environmental Resource Management ikishirikiana na kampuni za JSB Envi-Dep na eMjee Consult za Tanzania.

Warsha hizo zitaruhusu wadau kujadiliana kwa pamoja na kutoa maoni ya kutosha juu ya mada zitakazoongelewa ili kusaidia kuinua uchumi wa Tanzania kupitia rasilimali maji zilizopo kwenye bonde la mto huo.

No comments: