Advertisements

Tuesday, May 3, 2016

WAZIRI DK. AUGUSTINE MAHIGA, AMEZUNGUMZIA SAKATA LA MKE WAKE NA ASKARI WA KIKOSI CHA USALAMA BARABARANI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Augustine Mahiga, amezungumzia sakata la mke wake kudaiwa kumtukana askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani.

Dk. Mahiga alisema kwamba mke wake alipishana kauli na askari huyo aliyefahamika kwa jina la Deogratius Mbango, na hakutoa lugha ya matusi kama inavyodaiwa.
Alisema baada ya kupokea taarifa hiyo, alifuatilia ili kujua ukweli, ikiwamo kusikiliza sauti ya majibizano baina ya askari huyo na mkewe, ambapo alibaini kuwa walipishana kauli.
Hata hivyo Balozi Mahiga alisema suala hilo kwa sasa limemalizika na asingependa kuingia kwenye malumbano zaidi kwa jambo lililopita.
“Ni kweli mama (mke wake) alikuwa katika barabara ya Namanga, ambako alipishana kauli na askari wa usalama, nami nilifuatilia suala hili kwa undani sana. Ninachoweza kusema sitaki kuingia kwenye malumbano juu ya suala hili kwa kuwa limemalizika.

“Wewe umesikiliza hiyo ‘clip’ (sauti ya mazungumzo) je, umesikia neno tusi? Hilo ndilo ninalojua kwa sasa, mengine sijui yanayoendelea,” alijibu kwa kifupi Balozi Mahiga.
Alipoulizwa kuhusu kusambaa kwa picha inayomdhalilisha, Dk. Mahiga alisema kwamba alishangazwa na picha hiyo huku akishindwa kuelewa lengo la watu walioitengeneza na kuisambaza.
“Hata mimi sijui lengo lao nini kuisambaza ile picha, maana mimi niliiona kama ulivyoiona wewe,” alisema.
Picha ya Balozi Mahiga inayoonyesha suruali yake imelowa sehemu ya mbele, imekuwa ikizunguka katika mitandao ya kijamii kwa takriban wiki moja sasa.
Source: Mtanzania.

2 comments:

Anonymous said...

Hizo picha zinazosambazwa hazimtendei haki Mhe Waziri wala nchi yetu. Tu tafakari kabla hatujachukuahatua ndiyo rai yangu.

Anonymous said...

Ameitisha waandishi kukanusha? muheshimiwa kubali yaishe omba msamaha tusonge mbele usipoteze muda wa waandishi huyo askari hawezi kusema uongo na rekodi ilirekodiwa baada ya kutukanwa omba msamaha polisi tuendelee hapa kazi tu mtakoma mwaka huu kujisifia mie mke wa fulani yamekwisha wengine nao wameshajifunza