MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, jana alifungua kesi ya madai katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, kupinga amri ya polisi kuzuia mikutano ya vyama vya siasa nchini.
Kesi
hiyo namba 79 ya mwaka 2016, ilifunguliwa jana na kusimamiwa na
mawakili watatu Gasper Mwanalyela, John Mallya na Paul Kipeja.
Licha
ya kuwepo na ulinzi mkali wa jeshi la polisi uliowekwa katika barabara
zote za kuelekea Mahakama Kuu, viongozi na wafuasi wa Chedema
walifanikiwa kuvuka vizuizi hivyo.
Akizungumza na waandishi wa
habari baada ya kutoka mahakamani jana jioni, Mbowe alisema sababu za
kufunguliwa kwa kesi hiyo ni baada ya kuona demokrasia ya vyama vingi
"inabakwa nchini."
Mbowe alisema watu wanne waliotajwa katika kesi
hiyo ya madai ni Kamanda wa Polisi wilayani Geita, Kamanda wa Polisi
wilayani Kahama, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa polisi (Makao
Makuu) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Alisema wadaiwa hao
wamefunguliwa kesi kutokana na kukiuka Sheria ya Vyama vya Siasa nchini,
kwa kuchukua maamuzi ambayo hayaendani na demokrasia.
“Tunaiomba
mahakama itangaze amri ya jeshi la polisi ya kuzuia mikutano ya vyama
vya siasa ni batili, utekelezaji unaofanywa ni batili, polisi wapewe
tangazo la kutowanyanyasa wapinzani na pia itoe amri ya vyama vya siasa
kufanya mikutano yake na polisi wawe walinzi wa mikutano hiyo,” alisema
Mbowe.
Alisema pamoja na polisi kuwabana hawataondoka jijini Mwanza, na wataongezeka zaidi mpaka kieleweke.
Alisema
upo mkakati wa makusudi kuhakikisha Chadema inafutika katika mikoa ya
Kanda ya Ziwa kutokana na baadhi ya viongozi wake kutekwa na kunyanyaswa
na polisi.
Mkutano huo na waandishi wa habari ulihudhuriwa pia na
Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Saidi Issa Mohamed, Dk. Vincent Mashinji
(Katibu Mkuu), Salum Mwalimu (Naibu Katibu Zanzibar), Halima Mdee
(Mwenyekiti Bawacha) na Pastrobass Katambi (Mwenyekiti Bavicha) na
baadhi ya wabunge wa chama hicho.
Kesi hiyo ya madai inatarajiwa kupangiwa Jaji Jumatatu ijayo.
Polisi
ilisambaratisha mkutano wa Chadema uliokuwa ufanyike Kahama katikati ya
wiki, ambapo mabomu ya machozi na magari ya 'washawasha' vilitumika
kuondoa wafuasi wa chama hicho waliokuwa wasikilize hotuba za viongozi
wa kitaifa.
Chadema imepanga kufanya mikutano nchi nzima kulaani inachodai uonevu unaofanywa dhidi ya wabunge wake Bungeni.
1 comment:
Watu wafajye kazi sasa. Uchaguzi umekwisha. Vyama vifanye Mikutano kwenye kumbi za mikutano waite wanachama wachache waongee shida zao na ujumbe utawafikia watu. Mikutano hii ya hadhara inaleta fujo na wanaohudhuria mara nyingi ni watu wasiokuwa na kazi!
Post a Comment