VIONGOZI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Pwani, wamewapiga marufuku mameya wa chama hicho kuhudhuria mikutano ya kitaifa inayowahusisha viongozi wa juu wa serikali ndani ya kanda hiyo.
Viongozi waliotoa zuio hilo ni Katibu wa CHADEMA Kanda ya Pwani, Casmir Mabina na wenyeviti wa chama hicho mikoa ya kichama ya Dar es Salaam, Mwita Waitara, Makongoro Mahanga, mkoa wa Ilala, Baraka Mwago, mkoa wa Pwani na Stephano Waryoba, mkoa wa Temeke.
Wakizungumza na waandishi wa habari jijiji Dar es Salaam jana, viongozi hao wa CHADEMA walidai mara kadhaa mameya wao wamekuwa wakidhalilishwa katika mikutano hiyo, hivyo wameamua kuwazuia kwa muda wasihudhurie wakati wanasubiri maelekezo mengine kutoka uongozi wa juu wa chama.
Mabina alitaja baadhi ya matukio aliyosema kwamba mameya wa chama hicho walidhalilishwa katika mikutano kuwa ni, siku ya uzinduzi wa mradi wa umeme wa Kinyerezi II na siku ya uzinduzi wa Daraja la Kigamboni.
Alidai tukio jingine ni mameya hao akiwamo wa Kinondoni Boniface Jacob kurudishwa Uwanja wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) wakati akisafiri kwenda nje ya nchi kwa safari ya kikazi ambayo haikugharimiwa na fedha za serikali.
Alisema mwingine aliyezuiliwa ni Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara, ambaye aliteuliwa na Bunge kwenda kuwakilisha katika mkutano wa ukimwi duniani.
“Juzi Rais alishangaa kutokumuona Meya wa Kinondoni katika mkutano uliofanyika katika viwanja vya Biafra, hivi alitarajia kwamba pamoja na kumdhalilisha kote huko angewezaje kwenda katika mkutano huo ili akadhalilishwe tena au?,” alihoji Mabina na kuongeza:
“Kwa sasa maamuzi ambayo tumeamua CHADEMA Kanda ya Pwani ni hayo, hatukubali viongozi wetu kwenda kwenye mikutano hiyo na kudhalilishwa, kwa sasa tumeamua kuwalinda wakati tunasubiri maelekezo mengine kutoka uongozi wa juu wa chama, lakini kushirikiana katika kazi nyingine za maendeleo watakua wanafanya kama kawaida.”
Waitara alisema pamoja na mameya wao kuwewkewa vikwazo, lakini kazi zao wanafanya vizuri na mipango ambayo wameiweka ina lenga kuibadilisha Dar es Salaam.
“Hata mkutano ambao Jacob alikuwa anaenda huko nje ya nchi ulikuwa ni kwa ajili ya kupeleka mipango kwa ajili ya halmashauri yake, lakini wameikosa, pamoja na hayo nina amini hatashindwa kuingoza Kinondoni kwa kuwa ukiangalia mipango waliyoiweka kwa sasa haijawahi kutokea, hivyo hivyo kwa Ilala na kwa jiji,” alisema Waitara
Chanzo: Nipashe
1 comment:
Kama viongozi wa nchi idara mbalimbali wataendelea na dharau kwa viongozi waliochaguliwa kihalali toka vyama vyote mwisho wa siku Tanzania itaendelea kuwa gunia lililo na tobo na kuvuja hovyo.
Hawa ni viongozi kama wengine na wanawakilisha wananchi hivyo dharau hizi ni mbaya kabisa. Watawala acheni chuki.
Post a Comment