ANGALIA LIVE NEWS

Monday, June 27, 2016

WAZIRI MKUU AHUDHURIA MKUTANO WA SADC BOTSWANA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa anaondoka nchini leo (Jumatatu, Juni 27, 2016) kwenda Gaborone, Botswana kuhudhuria Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika wa Double Troika ya Asasi ya Siasa Ulinzi na Usalama (SADC Double Troika Summit) utakaofanyika kesho (Jumanne, Juni 28, 2016). 

Mhe. Waziri Mkuu anamuwakilisha Mhe. Rais Dk. John Pombe Magufuli kwenye mkutano huo utakaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Gaborone (GICC). 

Mkutano huo utafunguliwa na Rais wa Jamuhuri ya Botswana Mhe. Lt. Jen. Seretse Khama Ian Khama ambaye ni SADC, utajadili hali ya siasa, ulinzi na usalama nchini Lesotho. Mkutano huu utatanguliwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu ambao utafanyika leo (Jumatatu, 27 Juni, 2016). 
Pia mkutano huo utahudhuriwa na Marais wa Afrika Kusini, Mwenyekiti aliyetoka (outgoing chair) wa Asasi ya Siasa Ulinzi na Usalama Mhe. Jacob Zuma , Mhe. Jacinto Filipe Nyusi, Rais wa Jamuhuri ya Msumbiji na Mwenyekiti wa Asasi ya SADC ya Siasa, Ulinzi na Usalama. 

Wengine ni Mfalme Mswati III, Mfalme wa Swaziland ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa SADC, Mhe. Robert Mugabe, Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe na Mwenyekiti anayeondoka wa SADC. 

Waziri Mkuu amefuatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk. Augustine Mahiga, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dk. Aziz Mlima na Maofisa wengine waandamizi. 


IMETOLEWA NA: 

OFISI YA WAZIRI MKUU, 
2 MTAA WA MAGOGONI, 
S. L. P. 3021, 
11410 DAR ES SALAAM. 
JUMATATU, JUNI 27, 2016.

No comments: