Wednesday, June 15, 2016

DAR, KIBAHA KUKOSA MAJI KWA SIKU TATU

SHIRIKA LA Majisafi na Majitaka Dar es salaam (DAWASCO), imetangaza kuwapo tatizo la upatikanaji wa huduma ya Maji katika maeneo yote yanayohudumiwa na mtambo wa Maji wa Ruvu Juu, jijini Dar es salaam, pamoja na maeneo yote ya mji wa Kibaha mkoani Pwani kutokana na mtambo huo kuzimwa kwa wastani wa saa 72, kuanzia siku ya Ijumaa 17/06/2016, Jumamosi 18/06/2016 na Jumapili 19/06/2016.

Akizungumzia kukosekana Kwa huduma hiyo ya Maji, Kaimu Meneja Uhusiano wa DAWASCO, Bi. Everlasting Lyaro, ameeleza sababu ya kuzimwa kwa mtambo wa Ruvu Juu, ni kumruhusu Mkandarasi (WABAG) kuunganisha mtambo mpya wa Maji na ule wa zamani, ambapo baada kukamilika kwa kazi hiyo, uzalishaji wa Maji utaanza mara moja.

“Tuko kwenye hatua ya mwisho ya kuunganisha mtambo mpya wa Maji na ule wa zamani, kazi hii ikikamilika, uzalishaji utapanda kutoka wastani wa lita Milioni 70 hadi kufikia lita Milioni 106 kwa siku hivyo kuweza kutimiza lengo letu la kumtua mama ndoo ya Maji kichwani” alisema Lyaro

Lyaro, ameeleza kuwa kuzimwa kwa mtambo huo, kutasababisha maeneo ya Mlandizi, Kibaha, Kibamba, Mbezi, Kimara, Ubungo, Kibangu, Makuburi pamoja na eneo lote la Tabata, Segerea hadi Kinyerezi kukosa huduma ya Maji.

Hivyo, ametoa wito kwa wateja na wananchi wote kuhifadhi Maji ya kutosha na kuyatumia kwa matumizi muhimu na lazima ili kukidhi mahitaji yao kwa kipindi chote cha kukosekana kwa huduma hiyo.

No comments: