Advertisements

Thursday, June 30, 2016

GESI ILIYOGUNDULIWA TANZANIA YAZUA MJADALA MZITO

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
By Elias Msuya, Mwananchi ;emsuya@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati Rais John Magufuli akiungana na Watanzania wengine wanaofurahia kugunduliwa kwa gesi ya helium nchini, baadhi ya wataalamu wa miamba wameshauri uchunguzi zaidi ufanyike ili kuthibitisha uwepo wa kiasi hicho.

Juzi, kulikuwa na taarifa za watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Oxford na kile cha Durham kwa ushirikiano na wataalamu wa madini kutoka Norway kuwa wamegundua uwepo wa takriban futi 54 bilioni za ujazo za hifadhi kubwa zaidi duniani ya gesi adimu zaidi ya helium katika Bonde la Ufa, Kusini mwa Tanzania.

Katika ukurasa wake wa Tweeter, Dk Magufuli alisema ni jambo la kumshukuru Mungu huku akiwataka wachumi, wanasheria na Watanzania kwa ujumla kujiandaa.

“Tunamshukuru Mungu Tanzania tumegundua gesi aina ya helium, wito wangu kwa wachumi, wanasheria na Watanzania wote kwa ujumla tujipange. Ugunduzi huu utuelekeze kujipanga hasa katika eneo la mikataba yetu ili rasilimali hii adimu isaidie kuujenga uchumi wetu,” alisema.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alikaririwa akithibitisha ugunduzi huo na kusema Serikali itaitumia gesi hiyo vizuri.

Hata hivyo, akizungumzia utafiti huo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Miamba (Geological Survey of Tanzania), Profesa Abdulkarim Mruma alisema hawakushiriki kwenye utafiti huo, hivyo ni mpaka wafanye utafiti wao kuthibitisha.

“Kwanza tulikuwa na mradi wa kutafuta helium na Wajerumani na tuliainisha maeneo yanayoweza kupatikana. Kwa hiyo hao watatifi walikuja kufuatilia maeneo tuliyoyaweka, ila hatukwenda nao,” alisema.

“Unajua mara nyingi watafiti wa madini huwa wana tabia ya kutaja viwango vikubwa vya upatikanaji wa madini ili kuongeza hisa za kampuni zao kwenye masoko ya madini. Kwa hiyo tutafuatilia kwa kuchimba ili kuhakikisha kama kweli hicho kiwango walichosema kipo. Kama hakipo tutawaeleza,” alisema Profesa Mruma.

Alisema gesi ya helium imekuwa ikipatikana kwa kiasi kidogo nchini tangu wakati wa ukoloni, lakini ugunduzi wa sasa ni mkubwa kidunia.

Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dk James Mataragio alisema hawana taarifa rasmi ya ugunduzi huo, hivyo hawezi kusema Taifa litafaidikaje.

“Tangu jana (juzi) tumeona vyombo vya habari vimeandika kuhusu gesi hiyo. Ukweli ni kwamba sijapokea taarifa rasmi kuhusu ugunduzi huo. Uchimbaji wa gesi ya helium ni tofauti kidogo na gesi nyingine, ni mpaka ithibitishwe kwanza na wataalamu kama ipo kweli ndipo tujue tutafaidikaje,” alisema.

Mkuu wa Idara ya Jiolojia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Elisante Mshiu alisema kama kweli kiasi hicho cha gesi kipo, Tanzania itakuwa na gesi hiyo mara mbili kuliko inayopatikana kote duniani.

“Ugunduzi wa sasa wa helium kwa kutumia njia za kisayansi umefungua zama mpya duniani. Ugunduzi huo unatoa uhakika wa upatikanaji wa gesi hiyo tofauti na utabiri uliotolewa na wanasayansi kuwa iliyopo itaisha ifikapo mwaka 2030. Helium iliyogunduliwa Tanzania ni meta za ujazo 54.2 bilioni, kwamba Tanzania itaongoza kwa kuzalisha gesi hiyo duniani.”

Dk Mshiu alisema gesi hiyo inayopatikana maeneo mbalimbali duniani ina mita za ujazo 25 bilioni, hivyo iliyopo Tanzania ni mara mbili yake.

Akizungumza kupitia mtandao wa ABC, mmoja wa wanasayansi Profesa Chris Ballentine kutoka Chuo Kikuu cha Oxford cha Uingereza alisema gesi hiyo iliyogunduliwa inaweza kutumika kwa zaidi ya miaka 20 ijayo.

Profesa Ballentine anayefanya kazi na kampuni ya Norway ya kutafuta helium, alisema ni mara ya kwanza kuitafuta helium na kuipata kwani mara nyingi hupatikana kwa bahati tu.
MWANANCHI

No comments: