Advertisements

Thursday, June 30, 2016

MSIGWA SASA AJA NA HOJA YA KUMWONDOA NAIBU SPIKA

Mchungaji Msigwa analalamikia Muswada wa Sheria
By Sharon Sauwa, Mwananchi; ssauwa@mwananchi.co.tz

Dodoma. Zikiwa zimepita siku kadhaa tangu wabunge wa Ukawa kuanza kususia vikao vinavyoendeshwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson, mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa amewasilisha hoja ya kumwondoa madarakani kwa madai ya kukiuka kanuni za Bunge wakati wa uwasilishwaji wa mjadala wa Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2016/17.

Msigwa amewasilishwa barua kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai kuiomba Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge iangalie na kujiridhisha na hoja hizo.

Akizungumza na waandishi wa habari bungeni jana, Msigwa alidai kuwa Dk Tulia aliondoa mapendekezo ya mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe na Jitu Son wa Babati Mjini (CCM) katika Bunge kwa sababu hayakufuata kanuni ilhali wabunge hao walipeleka marekebisho yao katika Kamati ya Bajeti ya Bunge.

“Dk Tulia amekiuka kanuni kwa kuzuia marekebisho ya waheshimiwa wabunge kwa kuzuia hoja zao zisijadiliwe na kamati ya Bunge huku akijua kuna uamuzi wa Spika wa Bunge kuhusu utaratibu wa kutekeleza kanuni ya 109 fasili ya pili ya Kanuni za Bunge toleo la Januari 2016,” alisema.

Pia, alisema Muswada wa Sheria ya Fedha wa 2016/17 uliosomwa kwa mara ya kwanza bungeni uliopewa namba tisa haukuwa ule uliowasilishwa kwa mara ya pili kwa kujadiliwa na kupitishwa na wabunge.

Alisema muswada huo uliowasilishwa mara ya pili uliwasilishwa kinyume cha kanuni za Bunge kwa sababu haukufuata taratibu na kupewa namba 12.

Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano ya Bunge, Owen Mwandumbya alisema muswada huo ulifuata taratibu za kikanuni kuanzia uwasilishaji, mijadala na upitishwaji.

Alisema maoni ya wadau katika muswada huo yalikuwa mengi, hivyo kulazimu kuchapishwa mara ya pili ili maoni ya wadau yazingatiwe.

Mbunge wa Rufiji, Mohamed Mchengerwa alisema kama maudhui ya muswada ni sawa hata kama namba zikikosewa haina madhara.
MWANANCHI

No comments: