Advertisements

Thursday, June 30, 2016

TP MAZEMBE WAMTAMANI KAMUSOKO

Kiungo wa Yanga, Thabani Kamusoko
TIMU ya soka ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), imesema imevutiwa na kiungo wa Yanga, Thabani Kamusoko.

Yanga na TP Mazembe zilichuana juzi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF CC) uliomalizika kwa Yanga kulala bao 1-0.

Akizungumza na gazeti hili juzi baada ya mchezo huo, Makamu wa Rais wa TP Mazembe, Mario Kawel alisema Kamusoko alicheza vizuri na ni aina ya mchezaji ambaye anafahamu majukumu yake uwanjani.

Mchezaji pekee wa Yanga aliyemvutia katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi yao ni Thabani Kamusoko.

“Mchezaji mzuri aliyenivutia ni yule mwenye rasta kichwani (Kamusoko), sijui anaitwa nani, lakini ndiye aliyecheza kiwango bora katika mchezo wetu, nina hakika anastahili kucheza kwetu, “ alisema Kawel.

Hata hivyo, alipoulizwa kama watafanya utaratibu wa kumsajili hivi sasa kwa kuzungumza na Yanga, alijibu kwa kuhoji: “Wataka kutusaidia ili iwe rahisi kumpata?”

Alisema suala la usajili ni mchakato mrefu, pia linahusisha kwanza klabu na hatimaye mchezaji kwa kuangalia maslahi zaidi, hivyo wao wamethibitisha ubora wake na kwamba kama watataka wamsajili sasa au baadaye, hilo hawezi kuzungumza.

“Ni mchezaji wa Yanga, ana mkataba na Yanga, mimi binafsi nimesema nimevutiwa naye natamani acheze kwetu, kwanza nitazungumza na kocha wetu kuona naye kama amevutiwa, ndipo tujipange,” alisema kiongozi huyo. Naye kocha wa TP Mazembe, Mfaransa, Hubert Velud, alimsifu kiungo huyo na kusema ana vitu vyote muhimu anavyopaswa kuwa navyo mchezaji. “Ni mchezaji mzuri, sijui mkataba wake ukoje, lakini ningefurahi kujumuika naye kikosini kwangu,” alisema kocha huyo.

Kamusoko raia wa Zimbabwe, amekuwa akifanya vizuri katika michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara na hata michezo ya kimataifa tangu atue nchini msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

TP Mazembe ilipokuja kucheza na Simba mwaka 2011 katika Ligi ya Mabingwa Afrika na kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 iliwasajili wachezaji wa Simba, mshambuliaji Mbwana Samatta na kiungo Mganda, Patrick Ochan. Samatta kwa sasa yupo KRC Genk ya Ubelgiji.

HABARI LEO

No comments: