Tuesday, June 7, 2016

MAGGID MJENGWA NA UCHAMBUZI WA HAYATI MUHAMED ALI BONDIA ALIYEFANYA MAKUBWA KATIKA MASUMBWI

R.I.P Muhammad Ali
– Daima Alikataa Kuwa Mbeba Mabuli..
Ndugu zangu,

Usiku wa kuamkia leo ulimwengu umefikiwa na habari za kifo cha mwanamasumbwi mahiri kupata kutokea hapa duniani, ni Muhammad Ali.

Muhammad Ali, atakumbukwa kama shujaa wa wanyonge wa dunia. Alikuwa bondia na mwanaharakati wa haki za wanyonge. Daima Ali hakukubali kuburuzwa.

Hapa nyumbani, Rais Mstaafu , Mzee Ali Hassan Mwinyi amejaliwa kipawa cha kutumia vema lugha ya Kiswahili anapowasilisha ujumbe wake. Kuna wakati alipata kutamka;
“ Ndugu zanguni, kuna wasafiri na wabeba mabuli!”.

Wabeba mabuli ni wale wanaotumiwa safarini kwa kazi ya kubeba hiki na kile, ni kama wapagazi. Wabeba mabuli ni watu wa kuamrishwa safari bila kujua inakwenda wapi. Lakini wabeba mabuli anaowazungumzia Mzee Ali Hassan Mwinyi ni viumbe wenye kufikiri.

Bondia Mohammed Ali alipata kuvuliwa ubingwa wa uzito wa juu duniani kwa kukataa kwenda kupigana vita Vietnam. Alipotakiwa aende vitani Mohammed Ali alikataa na kusema;

“ Siwezi kwenda Vietnam kwa vile sijui hao tunaokwenda kuwapiga wana kosa gani”

Mohammed Ali akaambiwa , kuwa wenzake wameshakwenda huko Vietnam, naye akajibu; 
“ Hao waliokwenda huenda wameshaambiwa kosa walilofanya Wa- Vietnam, miye bado sijalijua”.

Naam. Mohammed Ali hakwenda Vietnam, ni kiumbe anayefikiri na alikataa kuwa mbeba mabuli. Waliompa Mohammed Ali adhabu ya kunyang’anywa mkanda wake wa ubingwa na hata kufungiwa kucheza ngumi kwa muda fulani bado wanamuheshimu Mohammed Ali kwa msimamo wake ule.

Muhammad Ali atakumbukwa daima.
Maggid,
Iringa.

No comments: