SERIKALI imeagiza wote waliotengeneza watumishi hewa wafunguliwe mashitaka mahakamani huku ikionya kuwa iko tayari kusimamisha kazi maofisa utumishi wote nchi nzima wanaofikia 1,500 katika sakata hilo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angella Kairuki alisema hayo jana alipokuwa akichangia mjadala wa Hotuba ya Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2016/2017 bungeni mjini Dodoma.
Amesema tayari serikali imeshatoa agizo hilo la kuwashitaki maofisa wote waliotengeneza watumishi hewa na ikibidi iko tayari kuwasimamisha kazi maofisa utumishi 1,500 waliofundishwa kazi hiyo na serikali.
Kwa mujibu wa Waziri Kairuki, mpaka mwishoni mwa Mei, serikali ilikuwa imebaini uwepo wa watumishi hewa 12, 246 waliokuwa wakitafuna Sh bilioni 25.06 kila mwezi.
Katika kuelezea athari za ufujaji huo wa fedha za serikali, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji alisema hata katika ulipaji wa madeni ya mifuko ya hifadhi ya jamii, Rais John Magufuli aliagiza uhakiki ufanyike, kabla ya kulipa kwa kuwa penye wafanyakazi hewa, kuna malipo hewa ya wastaafu.
Alitoa mfano wa deni la Mfuko wa Pensheni wa PSPF, Serikali ilikuwa ikidaiwa Sh trilioni 2.67 lakini uhakiki wa deni hilo ulipofanyika, deni hilo likabainika ni Sh trilioni 2.04, hatua iliyosaidia Serikali kuepusha wizi wa karibu Sh bilioni 600 za wastaafu hewa.
January na uthubutu
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Muungano), January Makamba alizungumzia ahadi ya Rais ya kutoa Sh milioni 50 kila kijiji na kufafanua kuwa Sh bilioni 59 zilizotengwa, zitatumika kujifunza namna ya kutekeleza ahadi hiyo.
Aliwataka wabunge wa CCM kukumbuka kuwa chama hicho kilipomtangaza Dk Magufuli kuwa ndiye mgombea urais, kilitoa taarifa duniani ya aina ya Serikali, uongozi na mabadiliko wanayotaka Watanzania.
Alisema mabadiliko ya kweli hayawezi kutokea bila kuwepo kwa hatua kubwa na uthubutu ndio maana serikali imethubutu kuwa na Bajeti ya Sh trilioni 29.5 na uthubutu wa kutenga asilimia 40 ya bajeti hiyo katika maendeleo.
Kwa mujibu wa January, mahali popote kwenye uthubutu, lazima kutakuwa na watu watakaotia shaka na kuwataka wabunge wa CCM wasitilie shaka uwezo wa serikali katika kukusanya Sh trilioni 29.5 zilizokusudiwa.
Alisema wabunge wa CCM ndio wengi katika Bunge na Ilani ya Uchaguzi inayotekelezwa ni ya chama hicho, hivyo ni muhimu wamuunge mkono Rais Magufuli kwani akifanikiwa Rais na Tanzania imefanikiwa.
Alikumbusha kuwa maendeleo yanahitaji kujitoa sadaka na viongozi wao wamekubali kujitoa sadaka, hivyo wabunge, wafanyabiashara mpaka wadogo wakiwemo bodaboda, wajitoe sadaka kwa kulipa kodi.
Alitumia kauli ya Rais John Kennedy wa Marekani aliyoitoa miaka ya mwanzo ya 1960, alipowataka wananchi wa nchi hiyo, kutouliza nchi hiyo itawafanyia nini, bali wajihoji wao wataifanyia nini nchi yao.
Watanzania wanune
Naye Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alieleza namna Serikali ya China ilivyoridhia kutoa Sh trilioni tano nje ya Bajeti ya Serikali kwa ajili ya ujenzi wa viwanda kwa sekta binafsi, huku ikiahidi kutoa fedha nyingine Dola za Marekani milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vidogo.
Alihitimisha kwa kusema ujenzi wa uchumi wa viwanda ni sawa na vita na wakati wa vita, hakuna anayecheka hivyo Watanzania wote lazima wanune, ili kutimiza malengo ya kuongeza pato la jumla la taifa.
Aidha, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alisema pato la jumla la Taifa kwa sasa ni Dola za Marekani bilioni 55 na ili Tanzania ifike katika uchumi wa kati, inatakiwa kuongeza uzalishaji utakaoongeza pato la jumla la Taifa kuwa Dola za Marekani bilioni 200.
Alisema injini za kupeleka uzalishaji na uchumi katika kipato hicho, ziko nyingi na mojawapo ni sekta ya nishati ya umeme ambayo katika bajeti hiyo ya serikali, Wizara ya Nishati na Madini imetengewa Sh trilioni 1.43 ambapo asilimia 94 ya hizo ni za maendeleo na kati ya fedha hizo za maendeleo, asilimia 95 inakwenda kwenye umeme.
Katika kudhihirisha nia ya serikali katika sekta hiyo, Profesa Muhongo alisema katika bajeti inayomaliza muda wake, wizara hiyo imeshapata asilimia 80 ya fedha zilizotengwa katika bajeti ya mwaka huu unaoisha huku Wakala wa Umeme Vijijini (Rea) ikiwa imeshapata asilimia 80 ya fedha iliyotarajia.
Aliwaeleza wabunge kuwa katika bajeti waliyopitisha, usambazaji wa umeme vijijini umepangiwa Sh bilioni 534.
No comments:
Post a Comment