Sunday, June 5, 2016

MBWANA SAMATA AKABIDHIWA ENEO LA HEKARI 5 MKURANGA

Kaimu Mkurugenzi Idara ya Sanaa wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bi. Leah Kihimbi (wa pili kulia) akimkabidhi cheti cha umiliki wa eneo la ekari tano Baba yake Mbwana Samata huko Mkuranga leo 5 Juni, 2016. 

PICHA NA BENEDICT LIWENGA, MAELEZO.


NA BENEDICT LIWENGA, MAELEZO.

5/06/2016 DAR ES SALAAM.
Wasanii nchini wamehimizwa kuchangamkia fursa ya kujiunga na Shirikisho la Wasanii Tanzania (SHIWATA) ambao ndiyo waanzilishi wa kijiji maalum cha wasanii kilichopo Wilayani Mkuranga, lengo likiwa kuwavutia wasanii hao kuhamia katika kijiji hicho.

Kauli hiyo imetolewa leo na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Sanaa, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bi. Leah Kihimbi wakati wa hafla maalum ya kuwakabidhi maeneo wasanii 35 akiwemo Mwanasoka Mahiri wa Tanzania anayechezea soka la Kulipwa nchini Ubelgiji Bw. Mbwana Samata.

Bi. Kihimbi amewapongeza baadhi ya wasanii wa Shirikisho hilo kwa uthubutu wao wa kujiunga ndani ya kijiji hicho kwa kupata nafasi ya kujengewa makazi yao.

Katika hafla hiyo, wasanii mbalimbali nchini wamefanikiwa kupewa vyeti vya umiliki wa maeneo waliyogawiwa kulingana na pesa za michango yao huku akiwataka wasanii wengine kuiga mfano huo.

"Nimeambiwa kuwa Shirikisho hili la Shiwata linafanya kazi kwa kuwashirikisha wadau wake kama vile warsha,makongamano, mafunzo ya kitaaluma na ujasiriamali kwahiyo naamini kijiji hiki kitasheheni sifa zote hizi", alisema Kihimbi.

Akizungumzia suala la miradi miwili katika eneo hilo, amesema kuwa Shiwata imechagua eneo zuri huku akiahidi kuzifikisha kwa Waziri mwenye dhamana, Mhe. Nape Nnauye baadhi ya changamoto zilizopo ndani ya eneo hilo kama vile barabara, maji pamoja na umeme.

" Nimeambiwa kuwa kuna miradi hii miwili ya ekari 500 katika kijiji cha Ngarambe ambayo ni mashamba makubwa na ekari 300 ambazo ndo hizi tulizopo, naipongeza Halmashauri ya Mkuranga kwa jambo hili zuri na Shiwata hawajafanya makosa kuchagua eneo hili, naahidi kuzifikisha baadhi ya changamoto za hapa kwa Mhe. Waziri kwani yeye anapenda sana kuona maendeleo katika tasnia hii", alisema Kihimbi.

Kwa upande wake Afisa Utamaduni Wilaya ya Mkuranga Bw. Pembe Mlekwa ameeleza kuwa, Wilaya yake imekuwa ikifanya jitihada za kuwawezesha wasanii kupatiwa maeneo wakati wa mbio za mwenge mwaka 2014 lengo likiwa kuitambulisha Tanzania na Dunia kwa ujumla.

"Lengo la Wilaya yetu la kuweka maeneo haya ni kuitambulisha Tanzania na Dunia kwa ujumla kuwa kuna kijiji cha Wasanii hapa nchini, kama ilivyo kule kwa wenzetu kama vile Hollywood nchini Marekani, ili wasanii wetu nao wajiskie kuwa wana eneo lao", alisema Mlekwa.

Naye baba wa Mwanasoka bora wa Tanzania Mbwana Samata ameipongeza Serikali kwa kumpatia mwanae eneo lenye ukubwa wa ekari tano ambapo mwanasoka huyo ameahidi kujenga Kituo cha Mafunzo cha Michezo ili vijana ndani na nje ya nchi waweze kuja na kupatiwa ujuzi.

" Mbwana Samata ameniambia kuwa anataka kupafanya mahali hapa kuwa pa Kimataifa kwani anataka kuanzisha Kituo Maalum cha Wanasoka kuja kujifua hasa vijana wadogo toka ndani na nje ya Tanzania", alisema mzee Samata.

Katika hafla hiyo, jumlanya Wasanii 35 wamepatiwa vyeti vya umiliki wa maeneo yao pamoja na ekari tano zimetolewa kwa ajili ya kumzawadia Mbwana Samata kwa kuifanyia Tanzania kung'ara katika soka.


MWISHO.

No comments: