Wednesday, June 1, 2016

NEC yakubali kukabidhi baadhi ya Mitambo ya TEHAMA kwa NIDA

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeridhia kuiazima Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) sehemu ya mitambo ya TEHAMA kwa ajili ya kuchakata taarifa wakati wa utekelezaji wa zoezi la utoaji wa Vitambulisho vya Taifa. 


Mitambo hiyo inayoazimwa na NIDA ni ile iliyotumika kuchakata taarifa za Wapiga Kura zikiwemo alama za vidole wakati wa Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Uamuzi huo umefikiwa katika kikao cha Tume hiyo kilichokutana leo  Jumatatu tarehe 30/05/2016 katika ofisi za NEC jijini DSM ambapo wajumbe walikubaliana kwa kauli moja kuhamishwa kwa muda mitambo hiyo kutoka ofisi za NEC na kwenda NIDA kwa gharama za Mamlaka hiyo.

Hatua hiyo inatokana na kuwepo kwa ugumu wa Mitambo hiyo kutumiwa na NIDA ikiwa katika ofisi za NEC kutokana na kutokuwepo kwa miundombinu ya mawasiliano (Mkongo wa Taifa) ambayo ingeunganisha mahali ilipo mitambo ya NEC (Processing Centre) na Mahali NIDA wanapofanyia uchakataji wa Vitambulisho (Data Centre).
Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Damian Lubuva amewaambia wajumbe wa Tume kuwa Mitambo hiyo itaazimwa na NIDA  kwa muda wa siku 90. 

Mapema akiwasilisha taarifa ya timu ya wataalam iliyopitia maombi ya NIDA, pamoja na maoni ya Menejimenti ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mkurugenzi wa Uchaguzi ndugu, Kailima Ramadhani amesema, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilinunua mitambo hiyo ya TEHAMA kwa ajili ya kufanikisha zoezi la Uandikishaji  Wapiga Kura na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Aidha, mitambo hiyo ina uwezo mkubwa wa kuchakata taarifa hususan uchakataji wa alama za vidole (finger prints).
Kwa mujibu wa Jaji Lubuva taratibu kwa ajili ya makabidhiano hayo zitaandaliwa ili kuwezesha baadhi ya mitambo hiyo ya TEHAMA kuhamishiwa kwa muda NIDA kwa mujibu wa makubaliano. 

No comments: