Thursday, June 9, 2016

Pemba hali si shwari CUF, CCM hawazikani

By Fidelis Butahe, Mwananchi fbutahe@mwananchi.co.tz

Pemba. Makovu ya kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu uliopita yanakitafuna kisiwa cha Pemba baada ya kuibuka ubaguzi baina ya wafuasi wa vyama vikuu vya kisiasa vya CCM na CUF na kuzorotesha shughuli za kijamii na kiuchumi.

Uchaguzi huo ulifutwa Oktoba 28 na mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salim Jecha kwa maelezo kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa sheria na kanuni za uchaguzi, jambo ambalo CUF walilipinga wakisema si mwenyekiti huyo au ZEC mwenye mamlaka ya kufuta uchaguzi, ikidai kuwa chama hicho kikuu cha upinzani kiliibuka mshindi.

Jecha alifuta uchaguzi huo siku ambayo alitakiwa atangaze mshindi wa mbio za urais, huku matokeo ya majimbo 31 yakiwa yameshatangazwa na matokeo ya majimbo mengine tisa yakiwa yameshahakikiwa na washindi kupewa vyeti vyao.

ZEC ilitangaza uchaguzi mpya ambao ulisusiwa na CUF ambayo ilitangaza kutoutambua.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwenye kisiwa hicho kidogo chenye watu takribani 400,000 umebaini kuwa wananchi hao wanabaguana katika misiba, sherehe, vyombo vya usafiri na biashara, jambo ambalo limethibitishwa na polisi, viongozi wa mikoa ya Kusini na Kaskazini Pemba pamoja na wa vyama hivyo viwili.

Matukio ya watu kuvamiwa na kupigwa, wananchi kususa kununua bidhaa za wafuasi wa chama kimoja, mabasi kukosa abiria au abiria kushushwa kwa sababu ya tofauti za kiitikadi, kususia kushiriki katika maziko na harusi yametawala kwenye kisiwa hicho ambacho ni moja ya visiwa vikubwa viwili vinavyounda Zanzibar.

“Wakati baba anafikwa na mauti alikuwa naibu sheha wa shehia ya Bopwe Wete. Lakini wakati wa shughuli za mazishi yake, watu waliokuja msibani walikuwa wachache kwa sababu tu alikuwa mwanaCCM. Tunawajua watu wa CUF pale kijijini na hawakuja msibani,’’ alisema Said Abrahaman mkazi wa wilaya ya Wete akizungumzia mazishi yaliyofanyika mwanzoni mwa Mei.

Abdallah Vuai Ali, dereva wa daladala linalofanya safari zake kati ya Chakechake na Ndagoni, alisema wiki mbili zilizopita alilazimika kupakia abiria mmoja kutoka Ndagoni hadi Chakechake kutokana na watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa CUF kuteremka katika gari hilo baada ya kupanda kada wa CCM.

“Yule mama naye aligoma kushuka katika gari, hivyo nililazimika kumpeleka kituo cha tatu kutoka hapa Ndagoni kisha nikawarudia wale abiria walioshuka,” alisema Ali.

Mwanachi lilifika Wilaya ya Mkoani ambako ilielezwa na baadhi ya wakazi wa eneo la bandari wanavaa sare za vyama ili waweze kutambulika itikadi zao kwa wateja wanaonunua bidhaa mbalimbali.

Omar Ali Faki, aliyedai kuwa ni kada wa CUF, alisema kabla ya wafanyabiashara kuondolewa eneo hilo kutokana na kuibuka kwa ubaguzi huo, biashara zake hazinunuliwi na wafuasi wa CCM.

Gazeti hili lilishuhudia wafanyabishara hao wakiwa wamezuiwa kuendelea na shughuli zao kutokana na uhasama huo wa kisiasa, huku mkuu wa kituo cha Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo (KMKM) katika bandari hiyo, Bakari Kombo Khamis akisema waliwaondoa wafanyabiashara hao kwa kisingizo cha mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu.

“Ilikuwa si ajabu kuona watu wamevaa sare za vyama sokoni na wateja walikuwa wananunua bidhaa kwa kutazama alichovaa muuzaji,” alisema Khamis.

“Kamati ya ulinzi ya wilaya tulikutana kujadili suala hili na kuamua kuwaondoa wafanyabiashara hao ili kupunguza hali hiyo ya kubaguana lakini bado wanafanya biashara kwa kujificha.”

Alidai baadhi ya wananchi wamesusa kupanda meli ya Mv Maendeleo na Mv Mapinduzi kwa maelezo kuwa ni za Serikali iliyopo madarakani na badala yake wanapanda meli ya Sealink ya kampuni ya Azam pamoja na Serengeti.

Viongozi waliozungumza na gazeti hili walisema mvutano na uhasama wa kisiasa upo kwa kiasi kikubwa katika wilaya ya Wete na Micheweni zilizopo Mkoa wa Kaskazini, huku viongozi wa CCM na CUF wakibainisha hatua wanazochukua kuwalinda wanachama wao.

Katibu wa CUF wilaya ya Micheweni, Khatib Hamad Sheikh na katibu wa chama hicho wilaya ya Wete, Riziki Omar Juma wanasema wafuasi wao wataendelea kutoshirikiana na CCM kwa sababu Serikali ikiwabagua kwa muda mrefu.

“Wanachama wetu wanapigwa na polisi bila sababu na tukipeleka taarifa vituoni, hakuna hatua zinazochukuliwa. Vijana wa CUF wananyimwa ajira, wananyimwa vitambulisho vya ukaazi na hati za kusafiria. Haya yote ni mateso ambayo tumeyavumilia na sasa yamefika mwisho,” alisema Riziki.

Katibu wa CCM wa Wilaya ya Kaskazini Pemba, Hadija Nassor Abdi alisema uhasama baina ya wanachama wa CUF na CCM ni mkubwa kiasi cha kutoshirikiana katika shughuli za kijamii.

“Wanachama wetu wakishiriki katika shughuli za watu wa CUF wanafukuzwa, wanawashusha katika daladala na hawawauzii bidhaa ya aina yoyote wanapokwenda dukani,” alisema.

“Mashamba kuvamiwa na mazao kuharibiwa kwa sasa si jambo la ajabu. Nyumba kadhaa zimebomolewa na wiki mbili zilizopita walichoma moto nyumba ya mwanaCCM iliyopo kijiji cha Shumba.”

Itaendelea kesho

1 comment:

Anonymous said...

Ujinga kabisa cha kushangaza wakati watu hao hao wanajifanya waumini waliotukuka mbele ya M/Mungu kama si kulaanika kitu gani?