Advertisements

Saturday, July 9, 2016

MASHIRIKA YANAYOTETEA HAKI ZA WANAWAKE WAZUNGUMZIA NAFASI YA MWANAMKE KATIKA TEUZI MBALIMBALI ZA RAIS MAGUFULI

Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Mtandao, Lilian Liundi(kulia) akisoma tamko lililotolewa na mashirika yanayotetea haki za mwanamke kuusu uteuzi mdogo wa wanawake katika ngazi za wakuu wa wilaya, makatibu tawala pamoja na Wakurugenzi kuwa haujazingatia usawa. Katikati ni Mwanaharakati kutoka TGNP Mtandao Bi. Dina Mbaga 
Mratibu wa Kituo cha Usuluishi cha TAMWA, Bi. Gladness Hemedi Munuo(kushoto) akifafanua jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari waliofika katika ukumbi wa TGNP Mtandao leo, Kulia ni Mwanaharakati kutoka TGNP Mtandao Bi. Dina Mbaga
Baadhi ya wadau wa mashirika yanayotetea haki za wanawake wakifuatilia kwa makini wakati wa mkutano na waandishi wa habari
Waandishi wa habari wakiwa kazini

Mashirika yanayotetea haki za wanawake na usawa wa kijinsi nchini yamesema uteuzi wa nafasi muhimu za uongozi serikalini unaofanywa na Rais John Magufuli, hauzingatii hali halisi ya uwakilishi wa kijinsia. 

Akizungumza leo  jijini Dar es Salaam kwa niaba ya mashirika hayo, Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi alisema licha ya kupiga kelele tangu uteuzi wa Baraza la Mawaziri kuwa haukuzingatia usawa huo, bado hali inaonekana kuwa tete kwa upande wa wanawake. 

Alisema katika baraza hilo, kati ya mawaziri 19, wanne pekee ndiyo wanawake sawa na asilimia 21.1 ya mawaziri wote ikilinganishwa na uteuzi wa baraza la Serikali ya Awamu ya Nne ambalo lilikuwa na mawaziri wanawake 10 sawa na asilimia 33.3. 

Alisema manaibu waziri kati ya 16 waliopo, wanawake ni watano sawa na asilimia 31.25. 

“Ukiangalia upande wa makatibu wakuu, walioteuliwa ni 29 kati ya hao, wanaume ni 26 sawa na asilimia 89.7 huku wanawake wakipungua kutoka watano sawa na asilimia 21.7 ya mwaka 2014 hadi kufikia watatu sawa na asilimia 10.3 kwa sasa,” alisema Liundi. 

Alisema uteuzi wa wanawake katika nafasi hizo umepungua kwa asilimia 10. Katika nafasi ya wakuu wa mikoa, Liundi alisema idadi ya wanawake imeshuka zaidi, kati ya wakuu wa mikoa 26 Tanzania Bara, 21 ni wanaume sawa na asilimia 80 na wanawake ni watano sawa na asilimia mbili.

Kadhalika, alisema idadi ya wakuu wa wilaya imezidi kuporomoka ikilinganishwa na ya Februari mwaka jana ambako wanawake walikuwa asilimia 35.07: “Kwa maana nyingine, hapa uteuzi umepungua kwa asilimia saba.” 

Liundi alisema mikoa mitatu ya Simiyu, Songwe na Singida haina wawakilishi wanawake kwa nafasi ya ukuu wa wilaya. 

“Hii iko hata kwenye nafasi za makatibu tawala wa mikoa na wilaya na wakurugenzi wa halmashauri, hatuoni idadi ya wanawake ikiongezeka na badala yake inashuka,” alisema. 

Mwakilishi wa Taasisi ya Women Fund Tanzania (WFT), Dk Dinna Mbaga alisema Tanzania ni kati ya mataifa duniani yaliyoridhia na kusaini mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda inayoweka misingi ya usawa kwa binadamu ikiwamo ushiriki katika ngazi zote za uamuzi, lakini haitekelezi mikataba hiyo kwa ridhaa mpaka isukumwe na asasi za kiraia jambo linaloleta ukakasi. 

Alisema miongoni mwa mikataba hiyo ni Tamko la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu (UDHR: 1948), Mkataba wa Kimataifa wa Kutokomeza aina zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake (CEDAW: 1979), Mpango kazi wa Beijing (1995), Mkataba wa Ziada wa Maputo na Mkataba wa Nyongeza wa Jinsia na Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). 

Mwakilishi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Gladness Munuo alisema Tanzania kupitia Dira ya Maendeleo ya 2025, imetambua kuwa mojawapo ya vichocheo vya ukuaji wa uchumi ni pamoja na kuwa na jamii yenye maono ya kimaendeleo na utamaduni wezeshi kwa wanawake na makundi mengine.

2 comments:

happyhomemagazine said...

Katika hii issue ya uteuzi kushika nafasi mbalimbali vyama hivi vingetilia mkazo kumuinua mwanamke katika strategies ambazo zitapelekea wanawake wengi kuchaguliwa katika nyazifa mbalimbali. Hii issue ya kutaka wanawake wachaguliwe kwa kuwa ni wanaweka si sahihi matokeo yake itakuwa watu wapewa nafasi hawatoi matokeo mazuri wanazidi kuharibu reputation ya wanawake wenye uwezo.Mama Clinton hapa marekani husikii anasema apate nafasi kwakuwa ni mwanamke bali kwakuwa anao uwezo wa kuimudu nafasi anayoigombea, anajinadi. Harafu wanawake inabidi tuelewe jinsi ya kujinadi kama mwanamke anajua anaouwezo wa kuwa mkuu wa mkoa,au wilaya etc.tafuta njia sahihi za kufikisha ujumbe huo mahali panapohusika .Wanaume wengi wanapata nafasi kwa kujinadi hawaoni aibu kusema uwezo wao,experience zao kama sisi tunasubiri mtu akuone,afuatilie, akuteue, kwa design hii tutasubiri sana. Wapeni wanawake mbinu na elimu stahili.Statistics hazitatatua tatizo hili sisi tutakaa kuongea tu na kulaumu wanaume wao wanapeta.Ni maoni yangu

Anonymous said...

Serikali ya awamu ya nne ilijitahidi kuweka uwiano wa 50:50 matokeo yake tuliyaona.wanachopaswa kufanya ni kuwajengea wanawake wengi uwezo wa kielimu,uongozi nk.