Advertisements

Saturday, July 23, 2016

MKUTANO WA CCM KIKWETE AFUNGUKA SWALA LA LOWASSA

Mweneyekiti wa CCM mstaafu Rais Mstaafu Jakaya Kikwete na Mwenyekiti Mpya wa CCM Rais Dk. John Magufuli wakipunga mkono baada ya Magufuli kutawazwa rasmi kushika nafasi hiyo leo mjini Dodoma (PICHA NA BASHIR NKOROMO)

By Boniface Meena na Tausi Mbowe, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Dodoma. Hatimaye Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete amezungumzia sakata lililotokea mwaka jana kwenye kikao cha Halmashauri Kuu baada ya jina la Edward Lowassa kuenguliwa kwenye mbio za urais ndani ya chama hicho, akisema chombo hicho ni kigumu na kinahitaji umakini katika kukiendesha.

Kikwete, ambaye leo anavua uenyekiti, alitumia sakata hilo kumtahadharisha mrithi wake, John Magufuli kuhusu uendeshaji wa chama hicho, hasa Halmashauri Kuu ambayo ni chombo cha pili kwa ukubwa baada ya Mkutano Mkuu.

Kikwete alitoa tahadhari hiyo jana alipokuwa akifungua kikao cha Halmashauri Kuu kilichohudhuriwa na wajumbe 365 kwenye ukumbi wa White House mjini hapa.

Mwaka jana, baada ya jina la Lowassa kutokuwamo kwenye orodha wagombea watano waliotakiwa kuwasilishwa kwenye Halmashauri Kuu kwa ajili ya kupigiwa kura ili kubakiza majina matatu ya kupelekwa kwenye Mkutano Mkuu, baadhi ya wajumbe walichukizwa na uamuzi huo wa Kamati Kuu na waliamua kumaliza hasira zao kwa mwenyekiti wao.

Siku iliyofuata Julai 11, wakati Kikwete akiingia ukumbini kuendesha kikao cha Halmashauri Kuu, kundi la wajumbe liliimba kwa sauti “tuna imani na Lowassa”, kitendo ambacho kilionekana kuwashangaza viongozi wakuu wa CCM waliokuwa pamoja na mwenyekiti.

Kikwete aliungana nao kupiga makofi na baada ya sauti hizo kutulia, alifungua kikao na akakiahirisha kwa muda ili kujadili sakata hilo. Marais wa zamani, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa walifanya kazi ya kutuliza hasira wajumbe na kuwezesha kikao kuendelea na shughuli zake baadaye mchana.

Na jana, Kikwete hakuliweka kando tukio hilo la kihistoria lililotingisha chama hicho kikongwe nchini.

“Uzuri wa baraza hili la wazee ni wanapohitajika. Na wanapohitajika ni wakati muhimu, kwenye masuala makubwa ya chama chetu na uhai wake, Kama ilivyokuwa mwaka wa jana,” alisema Kikwete na kusababisha wajumbe wamkatishe kwa kupiga makofi kwa nguvu, vicheko na vigelegele.

“Chama chetu kilikuwa na msukosuko mkubwa. Na (wakati) naingia hapa, watu wanaimba hivi, vijana wanaimba hivi; mjadala mkali. Lakini nikasema tutavuka tu. Maadam tupo, ndiyo changamoto yenyewe ya uongozi.”

Kikwete aliwahakikishia kuwa baada ya CCM kuvuka mgogoro huo, sasa kimekuwa imara zaidi.

“Na maadam CCM haikuvunjika mwaka wa jana, haivunjika tena,” alisema Kikwete na kushangiliwa tena kwa nguvu na wajumbe.

“Maana kuna mafisi yalikaa hapa, yanasubiri mkono udondoke, haukudondoka. Na maadam haukudondoka mwaka wa jana, CCM haidondoki.”

Kikwete pia alitumia nafasi hiyo kumshauri mrithi wake kuhusu chama hicho.

“Ndugu Rais (Magufuli), hivi karibuni utakuwa mwenyekiti. Kikao hiki kinakuwa kigumu, kigumu sana na ni kikao cha juu cha uongozi, hasa kipindi ambacho hakuna Mkutano Mkuu,” alisema Kikwete, ambaye amekulia kwenye chama hicho akishika nafasi tofauti hadi uenyekiti wa taifa.

“Wanasifia sana hawa (wajumbe). Lakini mambo yao yasipokuwa mazuri, wanakuwa wakali, tena wakali kwelikweli, ila ni kwa nia njema tu.”

Lowassa alikuwa mmoja wa makada waliokuwa wanapewa nafasi kubwa ya kupitishwa na CCM kuwania urais, lakini kikwazo hicho kilifanya jaribio lake la pili la kuingia Ikulu kushindikana na baada ya siku chache alitangaza kujiunga na Chadema, ambayo ilimpa nafasi ya kuendelea na “safari ya matumaini”.

Uamuzi wake wa kuihama CCM ulifuatiwa na makada wengine waliowahi kuwa mawaziri, wenyeviti wa mikoa, wabunge na madiwani, wakiongozwa na Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye, hali iliyofanya Uchaguzi Mkuu uliopita kuwa na upinzani mkali.

Kikao cha jana cha Halmashauri Kuu kilikuwa ni cha maandalizi ya Mkutano Mkuu Maalumu ambao utakuwa na ajenda moja ya kumchagua mwenyekiti mpya wa CCM.

Kikwete analazimika kuachia uenyekiti mwaka mmoja kabla ya muda wa kikatiba, akiendeleza utamaduni wa chama hicho wa kumuachia Rais mpya wa Jamhuri ya Muungano anayechaguliwa kwa tiketi ya CCM, muda wa kujiandaa kwa Uchaguzi Mkuu wa chama hicho.

Akijua kazi iliyo mbele yake, Kikwete alitumia kikao hicho cha mwisho kwake kuwaaga wajumbe na kuwaomba wamuunge mkono na kumpa ushirikiano mwenyekiti mpya, akisema “hayo mengine ni historia tu”.

Akizungumzia kuondoka kwake, Kikwete aliwashukuru wajumbe wa kikao hicho kwa ushirikiano waliompa huku akiwataka kumpa ushirikiano mwenye kiti mtarajiwa ambaye alimtaja kuwa ni Rais Magufuli.

Alisema kwa kuwa kikao chaki hicho ni cha mwisho, siku nyingine atakayohudhuria atakuwa mwalikwa akiwa na sifa ya mzee wa CCM.

Kikwete pia alizungumzia baraza la wazee wa CCM akisema alilianzisha baada ya kupata ombi kutoka kwa Mkapa, ambaye aliongoza Serikali ya Awamu ya Tatu.

“Siku hiyo Mzee Mkapa alisema hebu tuacheni tupumzike mnafanya vikao mpaka saa nane za usiku. Sisi tulishaongoza muda wetu umekwisha tunatamani kuwaona nyie mkiongoza,” alisema Kikwete na hapo wakaunda baraza la wazee.

“Watu wakaleta maneno mengi kwamba Kikwete hapendi wazee, lakini wote ni mashahidi walivyofanya kazi nzuri kipindi kile (cha sakata la Lowassa). Uzuri wa baraza hili wanapoitwa kwenye masuala makubwa, mfano la mwaka jana, wanatusaidia sana,” alisema Kikwete huku akishangiliwa na ukumbi mzima.

Awali akimkaribisha mwenyekiti, katibu mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema mkutano huo huwa na wajumbe 374 lakini waliohudhuria ni 365, idadi ambayo ni sawa na asilimia 97.5.

Baada ya Kinana kusema hivyo Kikwete alisema: “Kikao hiki hatumwi mtoto dukani, lazima uje mwenyewe.”

No comments: