Advertisements

Wednesday, July 6, 2016

MWANAMUKE AGONGA MAJAMBAZI KWA GARI

Simon Sirro, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya
By Colnely Joseph, Mwananchi cjoseph@mwananchipaperts.co.tz

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limempongeza mwanamke mmoja kwa ujasiri aliouonyesha alipowagonga kwa gari majambazi waliokuwa wanakimbia baada ya kuvamia duka lake kwa lengo la kumwibia.

Kamanda wa kanda hiyo, Simon Sirro aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba tukio hilo lililohusisha majambazi wanne wenye silaha lilitokea Juni 21, maeneo ya Buguruni Malapa.

Katika tukio hilo, Kamanda Sirro alisema majambazi hao walivamia duka la mwanamama huyo (polisi wamehifadhi jina lake) na kumtaka atoe fedha zote za mauzo.

Kwa mujibu wa Sirro, mwanamke huyo aliomba wasimdhuru badala yake aliwasihi waingie dukani wachukue hela na wakati wao wanaingia dukani, yeye aliingia ndani ya gari yake na kutulia. Lakini walipokuwa wanatoka na kupanda kwenye pikipiki zao, mwanamke huyo aliwasha gari akaendesha kwa kasi na kuwagonga wakaangusha bunduki aina ya shortgun, ingawa walifanikiwa kutoroka na Sh420,000 walizoiba. “Tunampongeza mwanamke huyu jasiri kwa kitendo cha kishujaa alichokifanya na tunaomba watu, hususan wanawake, waige mfano wake inapotokea nafasi kama hiyo waitumie,” alisema.

Kuhusu usalama wakati wa Sikukuu ya Eid el-Fitr, Kamanda Sirro alisema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama wamejipanga vizuri kuhakikisha sikukuu hiyo inasherehekewa katika hali ya utulivu na amani.

Alisema wahalifu hutumia sikukuu kama hizi kufanya matukio mabaya, hivyo jamii haina budi kuhakikisha kunakuwa na usalama hususani usimamizi wa watoto watakaokwenda kuogelea.

“Kusifanyike disko toto katika kumbi ambazo hazikidhi viwango vya kiusalama na askari wetu watafanya doria maeneo mbalimbali,” alisema.

No comments: