Advertisements

Friday, July 29, 2016

Mwigulu ‘aisaidia’ polisi kukamata mtuhumiwa

Raia wa China, Leo Swi akikamatwa kwa tuhuma za
By Rehema Matowo, Mwananchi rmatowo@mwananchi.co.tz

Geita. Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba ‘amelisaidia’ jeshi lake la polisi alipoongoza operesheni ya kumkata raia wa China anayedaiwa kumpiga mchimbaji mdogo na kumjeruhi katika mgodi wa dhahabu wa Nyamahuna uliopo wilayani Geita.

Tukio la kijana huyo kupigwa, lilisambaa kwenye mitandao ya kijamii mwishoni mwa wiki iliyopita ikidaiwa kuwa kijana huyo amepigwa hadi kuuawa baada ya kudai kuongezewa mshahara.

Taarifa hizo zilimlazimu Nchemba kufunga safari hadi katika Gereza la Geita na kukutana na kijana huyo, Masanja Shokala na kisha kuondoka naye akiwa amefungwa pingu hadi kwenye mgodi huo ili kuwatambua waliomtesa na kumpiga.

Akiwa ameambatana na kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Geita, ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Ezekiel Kyunga, Nchemba alisema kitendo cha walinzi wa watano wa mgodi huo ambao ni Watanzania kushirikiana na Mchina hiyo kumfunga kijana huyo mikono na miguu kisha kuanza kumpiga si cha kiungwana na kutaka sheria ichukue mkondo wake.

“Niliona hizi taarifa nikasema ni vizuri nifike kujua ukweli nimejionea mwenyewe. Hata waliompiga hawana maelezo zaidi ya kukanyagana, mara alikua mlevi mara mwizi mara mkorofi, hakuna ukweli juu ya hili lakini walimpiga na hadi sasa ana alama na kibaya zaidi aliyepigwa yupo mahabusu lakini waliompiga hawajakamatwa,” alisema Mwigulu.

Alieleza kukerwa na utendaji wa baadhi ya polisi kukubali kumkamata mtu aliyepigwa na kumuweka ndani huku waliompiga wakiwa huru na kuahidi kutoa maelekezo ya kiofisi ili kukomesha vitendo hivyo.

Mmoja wa walinzi wa mgodi huo, Peter Kassim alidai kijana huyo aliiba mawe mgodini na alipokamatwa alitaka kukimbia ndipo walipomfunga kisha kumfikisha mikononi mwa polisi.

Hata hivyo, Shokala alisema siku ya tukio aliitwa na walinzi na kuambiwa anahitajika ofisini na baada ya kufika alianza kupigwa na kutakiwa kueleza alikoficha mawe.

“Sikupigana kama wanavyosema... nilipofika nilianza kupigwa nikiambiwa niseme nilikoficha mawe walinipiga sana hadi nikazimia niliposhtuka nilijikuta mahabusu,” alisema Shokala.

Baada ya maelezo hayo, Nchemba alihoji: “Mkuu wa Mkoa tusaidie, wanasema eti kijana alikuwa mlevi na alikuwa anawapiga, mlevi ana nguvu za kupigana?” Mkuu wa Mkoa akajibu: “Hapana mlevi hana nguvu za kupigana.”

No comments: