Advertisements

Friday, July 29, 2016

RAIS MAGUFULI ATOA ONYO KWA WATAKAOTHUBUTU KUFANYA VURUGU KATIKA ZIARA YAKE YA SIKU NNE KWENYE MIKOA MINNE



Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew Mtigumwe akimpokea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli mara baada ya kuwasili katika Wilaya ya Manyoni Mkoani Singida.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia mamia ya wakazi wa Manyoni Mkoani Singida mara baada ya kuwasili katika Wilaya hiyo akiwa njiani kuelekea mkoani Singida. 
Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli akiwasalimia wakazi wa Singida mara baada ya kuwasili.



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 29 Julai, 2016 ameanza ziara ya siku nne katika mikoa ya Singida, Tabora, Shinyanga na Geita akitokea mkoani Dodoma, ambapo amezungumza na wananchi kwa lengo la kuwashukuru kwa kumpigia kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na kueleza juhudi zinazofanywa na serikali katika kutatua kero za wananchi na kuwaletea maendeleo.

Akiwa Mkoani Singida, Rais Magufuli aliyeongozana na mkewe Mama Janeth Magufuli amewasihi watanzania kufanya kazi kwa juhudi na kujiepusha na vitendo vya vurugu vinavyohamasishwa na baadhi ya wanasiasa huku akionya kuwa serikali yake haitamvumilia mtu yeyote ambaye atathubutu kuchochea vurugu ikiwemo maandamano kinyume cha sheria.

"Sitaki nchi hii iwe ya vurugu, watakaoleta vurugu mimi nitawashughulikia kikamilifu bila huruma, na wasije wakanijaribu, mimi ni tofauti sana na kama wapo watu wanaowatumia wakawaeleze vizuri, mimi sijaribiwi na wala sitajaribiwa."Wananchi hawa wana shida, na siasa nzuri ni wananchi washibe, siasa nzuri ni wananchi wetu wapate dawa" Amesema Rais Magufuli.

Kuhusu hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali yake ya awamu ya tano tangu aingie madarakani Rais Magufuli ametaja baadhi ya hatua hizo kuwa ni kufuta ada kwa shule za msingi na sekondari, kutoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu zaidi ya laki moja na kuongeza fedha za miradi ya maendeleo katika bajeti ya serikali kutoka asilimia 26 ya mwaka 2015/2016 hadi kufikia asilimia 40 katika bajeti ya mwaka huu 2016/2017.


Hatua nyingine ni kuondoa wafanyakazi hewa 12,500 katika orodha ya waliokuwa wanalipwa mshahara na serikali, kudhibiti upotevu wa mapato serikalini, kutenga shilingi Trilioni moja kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Reli ya kati kwa kiwango cha kisasa yaani Standard gauge na pia akazungumzia hatua zilizochukuliwa dhidi ya wala rushwa na wanaojihusisha na ufisadi kwa kuunda mahakama ya mafisadi huku akiapa kuwa katika kipindi chake hakuna fisadi atakayeendelea kutamba.

Akiwa njiani Rais Magufuli amewasalimu wananchi wa Ikungi na baadaye amefanya mkutano wa hadhara Singida Mjini ambako amesisitiza kuwa serikali yake haiko tayari kumvumilia mtu yeyote atakayekwamisha utekelezaji wa Ahadi na Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Singida

29 Julai, 2016

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwapungia wakazi wa Manyoni mara baada ya kumaliza kuhutubia katika Uwanja wa Shule ya Msingi Tambuka Reli Manyoni Mkoani Singida.
Mbunge wa manyoni Magharibi Yahya Masare akicheza ngoma na kikundi cha Ngoma za asili cha Manyoni kabla ya Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Magufuli kuhutubia mkutano katika Uwanja wa Shule ya Msingi Tambuka Reli Manyoni Mkoani Singida.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwahutubia wakazi wa Ikungi waliomsimamisha wakati akielekea Mkoani Singida. PICHA NA IKULU 

4 comments:

Anonymous said...

Another TRUMP

Anonymous said...

Kuna zaidi ya kushiba na dawa. Watanzania tulipewa dawa bure miaka 24 yote ya Nyerere na chakula kilikuwa rahisi kupatikana lakini watanzania tunahitaji zaidi ya hayo. Tunahitaji demokrasia,uhuru na haki yetu ya kutoa na kupokea mawazo,uhuru wa habari, tunahitaji elimu bora, teknolojia bora,makazi bora,usalama wa watanzania na siasa bora. Tunataka mafisadi wafilisiwe na kufungwa lakini wanafungwa wezi wadogo.Hatutaki kutishwa tishwa. Tanzania imekuwepo kabla ya Magufuli na itakuwa miaka milioni na mamilioni yajayo hivyo Magufuli aache ubabe, amesifiwa amevimba kichwa na wasaidizi wake wanashindwa kumweleza.AIBU AIBU.

Anonymous said...

Hivyo kuelezwa ukweli ndio kutishwa? Tanzania imekuwepo kabla ya Magufuli na wapumbavu pia walikuwepo kabla ya Magufuli na wataendelea kuwepo miaka milioni ijayo,isipokuwa Magufuli anawajibu kutumia madaraka yake kama kiongozi mkuu wa nchi kuhakikisha nidhamu nchini inadumishwa na kuepusha vurugu sizokuwa na ulazima kwa kisingizio cha demokrasia. Maghufuli alipoanzia ni pazuri na anajeuri ya kuwa mbabe, kwa mtu kama Maghufuli alieshuhudia watanzania watumishi wake wa serikali wengi wao wakiwa na elimu ya hali ya juu ya darasani,wengi wakiwa na masters,degree nakadhalika nakadhalika wakipuuza dhamana zao huku wakifanya mambo ya ajabu na ya aibu ya kuiangamiza nchi yao. Maghufuli anawaelewa watanzania naweza kusema kuliko mtu mwengine yeyote ni mtu mwenye kumbu kumbu za ajabu katika kichwa chake. Watanzania wengi wetu ni watu hovyo ni kama bahati kumpata mtu kama Maghufuli kwa Tanzania. Hao wanaodai maandamano, sijui demokrasia aah sijui uhuru wa kujieleza vyote hivyo vilipatikana wakati wa kikwete lakini nini cha maana kilipatikana wakati huo ambacho kilisaidi utendaji wa serikali na kuinua maisha watanzania ambao wengi wao ni wanyonge? Na Kama kuwa kiongozi anaeumwa na hali duni ya maisha ya wananchi wake ni udikteta basi muecheni Magufuli awe dikteta. Na kama kuwa kiongozi ambae anapigana kufa kuhakikisha rasilimali za nchi yake hazitoroshwi na walowezi wa nje bali ziwanufaishe wananchi waliowengi ni udikteta basi muacheni Maghufuli awe dikteta. Na kama kuwa kiongozi aliejitolea muhanga kupambana na ubadhirifu wa aina zote rushwa,mishahara hewa,uzembe kazini,uvuvi kwa raia mmoja mmoja,vyeti feki,ufasadi katika ukusanyaji wa mapato ya serikali ni udikteta? basi muacheni awe dikteta. Na kama kuwa kiongozi anaepambana kufa kuhakikisha amani na usalama Tanzania inadumu ni udikteta basi muacheni Maghufuli awe dikteta. Tunajua mtu kutowa maoni yake ni demokrasia sasa Magufuli ana haki ya kutoa maoni yake na hata kama yakifikia kiwango cha amri ni haki yake pia kwa kuwa yeye ni kiongozi wa nchi aliechaguliwa kidemokrasia kabisa kitendo chochote cha kumfanyia figisu kama kuendesha maandamano haramu na nakadhalika ili ashindwe kuwatumikia wananchi wake huo pia ni uvunjifu mkubwa wa demokrasia. Tangu Obama achuguliwe kuwa raisi katika muhula wake huu wa mwisho dhidi ya Mit Romney wa republican katika uchaguzi ambao Republican walikuwa lazima washinde kwa hivyo ulikuwa uchaguzi wa kufa mtu lakini mwisho ya siku Mit Romney anampigia simu Obama kumpongeza kwa ushindi na kamwe hatujasikia Republican wanataka kufanya maandamano nchi nzima au upumbavu gani? Kama kuna hoja watu wanachuana bungeni hiyo ndio demokrasia sasa hayo mambo ya maandamano na kuwashawishi wananchi wasitishe shughuli zao za maendeleo huo ni uhaini na kama namuona raisi Magufuli anawalealea hao wapuuzi wa aina hiyo badala ya kuwsweka ndani.wakati wa kulea majibi ya kisiasa kwa kisingizio cha demokrasia umekwisha la sivyo Tanzania siku zote tutaitolea mfano Rwanda kwa kupiga hatua za kimaendeleo tukibakia kupiga siasa za hovyo zisizo na tija.

Anonymous said...

Kama Trump anachukua hatua dhidi ya wahujumu uchumi, anasimamia nidhamu,anatambua uwepo wa wasomi,anasimamia ukusanyaji wa kodi then pengine Tanzania ya leo ilipaswa kuwa na akina Trump 10 kwani taifa lilikuwa limejaa wajanjawajanja,political entrepreneurs wasio taka kulipa kodi na wezi.