Advertisements

Thursday, July 7, 2016

SHEIN AKEMEA CHOKOCHOKO ZANZIBAR

Waumini wa dini ya Kiislamu wakiwa katika swala ya Sunna ya Idd el Fitr, iliyoswaliwa katika viwanja vya Maisara Suleiman mjini Unguja jana, baada ya kumalizika kwa mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani. (Na Mpigapicha Wetu).
RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema uchaguzi mkuu visiwani humo ulishamalizika na hakuna mpango wa kuwepo kwa serikali ya mpito.

Amesema uchaguzi umekwisha kabla ya mwingine utakaofanyika mwaka 2020; hivyo kazi kubwa inayofanywa sasa ni kusimamia na kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015-2020 kwa ajili ya kuwaletea wananchi maendeleo.

Alisema hayo jana wakati akihutubia Baraza la Iddi na kusisitiza kuwa atapambana na watu ambao wamekuwa wakifanya mbinu serikali ishindwe kutekeleza mipango yake.

Alisema wapo watu wamekuwa wakijaribu kufanya mbinu na vituko serikali ishindwe kutekeleza mipango yake, ikiwemo kusimamia ilani ya chama na bajeti ya serikali kwa mwaka 2016/2017.

Dk Shein aliwapongeza wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa kupitisha bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2016/2017, ambayo kazi kubwa itakayofanywa ni kusimamia mapato na kupata fedha za kutekeleza mipango hiyo.

“Wananchi napenda kusema tena kwamba uchaguzi umekwisha na utafanyika mwingine ifikapo mwaka 2020...wanaotaka kuwepo kwa serikali ya mpito wasahau,” alisema.

Alisema hakuna sababu ya kuwepo kwa serikali ya mpito kwa sababu CCM ilishiriki katika uchaguzi wa marudio na kushinda kwa kishindo. Aliwataka wananchi kupuuza propaganda zinazotolewa na wapinzani kwa ajili ya kile alichosema ni kuwazubaisha wananchi washindwe kufanya kazi zao vizuri.

Alikemea matukio yanayojitokeza zaidi katika kisiwa cha Pemba, yakiashiria uvunjifu wa amani na utulivu.

Alivitaka vyama vya siasa kufanya kazi zao bila ya kukiuka sheria zilizopo. Alisema vitendo vya chuki na ufisadi ni kinyume na maagizo ya Mungu.

“Nimesikitishwa sana na matukio yote ambayo yamelitia aibu kubwa taifa letu kwani hayaendani na mafunzo tuliyoyapata katika kipindi cha swaumu...tunatakiwa kuacha kujenga kiburi na ufisadi,” alisema.

Wakati huo huo, alikemea matukio ya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia ikiwemo vya kuwadhuru watoto, ikiwemo baadhi vilivyofanyika katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.Alisema serikali imejizatiti kupambana na matukio hayo, ikiwemo kuanzishwa kwa mahakama ya watoto, itakayosikiliza kwa haraka kesi zinazohusu kundi hilo.

Alitaka jamii kuwa tayari kutoa ushahidi mbali ya vyombo vya sheria ikiwa ndiyo njia muafaka ya kukomesha matukio hayo.

“Serikali tumejipanga kupambana na matukio ya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia lakini jamii nayo iwe tayari kutoa ushahidi mbele ya vyombo vya sheria,” alisema.

Kwa upande wake, Mufti wa Zanzibar, Shehe Mkuu Saleh Kabi alimpongeza rais kwa ustahimilivu katika kuongoza visiwa vya Unguja na Pemba kwa utulivu mkubwa na hekima.

“Huo ndiyo uongozi bora uliotukuka wa kuongoza nchi kwa kutumia busara na hekima japo unajua wapo watu wanaofanya vitimbi,” alisema.

Sherehe za baraza la Iddi zilihudhuriwa na viongozi mbali mbali, akiwemo Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Makamu wa Rais mstaafu, Dk Mohamed Gharib Bilal.

HABARI LEO

No comments: