Advertisements

Thursday, July 7, 2016

SHEHE ATAKA ADHABU KALI WA MADEREVA WAZEMBE

Kaimu Shehe wa Mkoa wa Dodoma, Ahmed Saidi
Kaimu Shehe wa Mkoa wa Dodoma, Ahmed Saidi

KAIMU Shehe wa Mkoa wa Dodoma, Ahmed Saidi ameiomba serikali kuwachukulia hatua kali madereva wazembe wanaosababisha ajali zinazopoteza maisha ya nguvu kazi ya taifa.

Alitoa kauli hiyo jana, ikiwa ni siku mbili baada ya ajali ya mabasi mawili ya Kampuni ya City Boy yaliyogongana eneo la Maweni, Manyoni mkoani Singida na kusababisha vifo vya watu 31 mpaka jana na wengine 48 kujeruhiwa.

Wakati kiongozi huyo wa kiimani akieleza hayo katika mawaidha ya Sikukuu ya Idd el Fitr kwenye Msikiti wa Gadaffi mkoani Dodoma, miili ya watu waliokufa kwenye ajali hiyo imetambuliwa na kuchukuliwa na ndugu zao isipokuwa ya watu watatu.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Thobias Sedoyeka alisema jana kwa njia ya simu kuwa, miili hiyo iko katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma ikisubiri kutambuliwa na ndugu.

Shehe Saidi alisema ipo dhana kuwa ajali hizo zote ni kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu, lakini si kweli na kwamba zinasababishwa na uzembe wa binadamu wenyewe, wakiwemo madereva wazembe wanaostahili adhabu kali ya serikali.

“Angalieni kama ile ajali iliyotokea kijiji cha Maweni pale Manyoni ikihusisha mabasi mawili, tena ya kampuni moja jinsi madereva wake walivyokuwa wazembe na kusababisha vifo vingi vya watu wasiokuwa na hatia. Hapa hakuna haki ya kumlaumu Mungu, hawa washughulikiwe tu,” alisema.

Pia amewataka Waislamu kuhakikisha wanadumisha amani na upendo kama walivyofanya katika kipindi chote cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambacho wengi walikuwa watiifu mbele za Mwenyezi Mungu.

Amewataka baada ya kumalizika kwa mfungo wasigeuke na kukumbuka mambo ya anasa hususani ulevi, usherati, uzinzi ugomvi, ushirikina na zinaa. Kuhusu ajali ya mabasi ya City Boy, Kamanda Sedoyeka alisema madereva waliosababisha ajali watafunguliwa mashitaka ya kuua bila ya kukusudia na si makosa ya usalama barabarani kama ilivyozoeleka.

Alimtaja Jeremiah Martin (34) aliyekuwa akiendesha basi aina ya Scania lenye namba za usajili T 531 BCE kutoka Dar es Salaam kwenda Kahama, kuwa anashikiliwa na polisi na atafikishwa mahakamani kesho huku dereva mwingine, Martin Mwakalukwa akiendelea kutafutwa kutokana na kusababisha ajali.

Kutokana na ajali hizo, tayari Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) imetangaza kuyafungia mabasi 12 ya Kampuni ya City Boy ili kupisha uchunguzi. Makampuni mengine yaliyofungiwa na Sumatra ni kampuni za Mohammed Trans, Otta High Class na Super Sami. Imeandikwa na Regina Kumba, Dar es Salaam na Sifa Lubasi, Dodoma.

HABARI LEO


1 comment:

Anonymous said...

I agree