Advertisements

Friday, July 22, 2016

SUA YAGUNDUA UGONJWA MPYA WENYE DALILI ZA MALARIA

Sehemu ya Chuo Kikuu cha Kilimo Cha Sokoine
CHUO Kikuu cha Sokoine (SUA), kimegundua ugonjwa mpya unaosambazwa na panya ujulikanao kama homa ya ‘Leptospirosis’ ambao dalili zake zinafanana na malaria, homa ya matumbo na dalili nyingine 40 kwa binadamu.

Mtafiti kutoka chuoni hapo, Dk Georgies Mgode alisema hayo alipokuwa akizungumza na wanahabari kuhusu ugonjwa huo.

Alisema asilimia 20 ya watu wenye homa ambao hawana malaria hapa nchini wana ugonjwa huo. Dk Mgode alisema, hadi sasa ugonjwa huo haupimiki katika hospitali yoyote hapa nchini na barani Afrika.

“Kwa bahati mbaya haupimiki katika hospitali yoyote hapa nchini na barani Afrika. Na Afrika ndiko kumeathirika zaidi kuliko sehemu nyingine duniani ambapo watu 95 hadi 100 kati ya 100,000 wana ugonjwa huu,” alisema mtafiti huyo.

Alisema kitengo cha utafiti na udhibiti wa viumbe hai waharibifu katika chuo hicho, kimefanya utafiti wa ugonjwa huo kwa miaka 23 na kugundua kuwa upo kwa wanyama wafugwao kama ng’ombe, mbuzi, kondoo, nguruwe, mbwa na paka.

Vile vile, alisema popo na samaki wa maji baridi wanabeba vimelea wa ugonjwa huo. Alisema utafiti huo umefanyika Morogoro mjini, Kilosa, Kilombero, Katavi na Kilimanjaro.

Alisema mkoani Morogoro ugonjwa huo kwa binadamu ni kati ya asilimia 10 hadi 15, Moshi ni asilimia tisa na Katavi asilimia 30. Kwa wafugaji wa mbwa Dar es Salaam ni asilimia 39.

Alisema, mkoani Morogoro nguruwe wenye vimelea ni asilimia 41, paka asilimia 14, panya asilimia 17, kiruka njia asilimia 25, Morogoro mjini popo walioweka makazi kwenye miti ambapo kuna makazi ya watu asilimia 19 na samaki wa maji baridi ni asilimia 54.

HABARI LEO

No comments: