Advertisements

Wednesday, July 13, 2016

WAZIRI AMTAKA MKANDARASI KUMALIZA UJENZI KWA WAKATI, AKAGUA MAENDELEO YA UJENZI WA DARAJA LA RUVU CHINI UNAOENDELEA.

 Mkandarasi wa Kampuni ya Estim Construction anayejenga Daraja la Ruvu Chini na Kariakoo (Wa pili kushoto) akitoa maelezo ya ujenzi huo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (Kulia kwake) wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi huo Wilaya Bagamoyo, Mkoani Pwani.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa mbele) akipita kwenye daraja la muda lililopo pembezoni mwa  Daraja la Mto Ruvu wakati alipokagua ujenzi wa daraja hilo lenye urefu wa Mita 140 katika barabara ya Msata-Bagamoyo, Mkoani Pwani.
Muonekano wa Sehemu ya juu ya Daraja la Ruvu Chini ambapo Ujenzi wake unaendelea na kutarajiwa kukamilika mwezi Novemba mwaka huu.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amemtaka mkandarasi wa Kampuni ya Estim Construction anayejenga Daraja la Ruvu Chini linalounganisha barabara ya Bagamoyo-Msata yenye urefu wa Km 64 mkoani Pwani kukamilisha ujenzi wa daraja hilo ifikapo mwezi Novemba mwaka huu.

Prof. Mbarawa amesema hayo wakati alipokagua ujenzi wa Daraja hilo na kuhimiza kukamilika kwa wakati uliopangwa ili  kuhakikisha barabara hiyo inapitika majira yote ya mwaka na kurahisisha huduma ya usafiri kwa wakazi wa mkoa wa Pwani na mikoa jirani.

“Hakikisheni ujenzi wa Daraja hili unakamilika kwa wakati ili lianze kutumiwa na wananchi kwa wakati wote kwa ajili ya  kujiletea maendeleo yao binafsi.” Amesema Prof.Mbarawa.
Vile vile Profesa Mbarawa amemhimiza Mkandarasi huyo kuzingatia viwango vya ubora kulingana na thamani ya fedha ili Daraja hilo liweze kudumu kwa muda mrefu.

“Ni vema daraja hili lijengwe  kwa ubora unaotakiwa kulingana na thamani ya fedha ili liweze kuhimili athari za Mvua zinajitokeza eneo hili”. amesisitiza Waziri Mbarawa.

 Aidha Waziri Mbarawa ameongeza kuwa Serikali inaendelea kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika miradi inayotarajiwa kuanza kutekelezwa maeneo mbalimbali nchini.

Zaidi ya Shilingi Bilioni 129zitatumika katika ujenzi wa Barabara ya Msata-Bagamoyo Km 64, Daraja la Ruvu chini yenye urefu wa Mita 140 pamoja na Barabara ya Maingiliano ya Daraja hilo yenye urefu KM 4.2.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

No comments: