Advertisements

Thursday, July 7, 2016

ZADIA YAFANIKISHA SADAKA LICHA YA CHANGAMOTO ZA URASIMU

Licha ya changamoto za urasimu zilizotokana na Serikali ya Zanzibar kupiga marufuku kufutarisha katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani, Jumuiya ya Wazanzibari waishio nchini Marekani (ZADIA) ilifanikisha zoezi la kugawa sadaka kwa aijli ya Ramdahani na Eidul Fitri visiwani Zanzibar.
Katika taarifa yake ya salamu za Siku Kuu ya Eid, Mwenyekiti wa ZADIA Bwana Omar Haji Ali amesema " Serikali ilipiga marufuku kufutarisha wakielezea kwamba wanakhofia kipindupindu. Kwa vile tulikuwa na nia njema, tuliwaomba Maofisa wa Serikali watoe nafasi ya Zanzibar Diaspora Association (ZADIA) ifutarishe. Mlolongo wa Urasimu ukaanza".
Katika taarifa hiyo ambayo Swahilivilla ilipata nakala yake, Bwana Ali alitoa mkono wa Eid kwa Wazanzibari na waislamu wote duniani.
"Kwa niaba ya Zanzibar Diaspora Association, napenda kuchukua nafasi hii kutoa mkono wa Eid kwa Wazanzibari wote popote walipo duniani. Salaam hizo pia ziwaendee Waislam wote wenye furaha na wale ambao nyoyo zao haziko katika hali ya furaha kutokana na sababu moja au nyengine", ilsema taarifa hiyo na kuongeza: "Tunawaombea siku hii ya furaha iwe ni chachu ya kuwaletea furaha nyoyoni mwao na kuwapunguzia au kuwaondolea machungu yaliowakaa"
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hatua ya kufutarisha visiwani Zanzibar ilikuja kama ishara ya Wana ZADIA kuonesha mshikamano wao na ndugu zao waliko nyumbani katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani, ambao baadhi yao hali zao za kiuchumi sio nzuri, ikilinganishwa na Wanadiaspora hao ambao wana uwezo wa kujikimu kimaisha.
"Bahati mbaya hali kwa wengi wa Wazanzibari waishio Zanzibar sio nzuri. Jambo hilo limekuwa likiwagusa wengi wa Wazanzibari na kuona kwamba nchi yao ndogo kama ile, yenye rasilimali kama zile iko katika hali ambayo watu wake sio wote wanatimiza mahitaji yao ya kila siku, ikiwemo ugumu wa kukamilisha futari", ilisema taarifa hiyo, na kusisitiza kuwa kuna haja ya kutafuta suluhisho kwa hali hiyo.
Kutokana na marufuku ya kufutarisha kwa makundi, taarifa hiyo imeeleza kuwa, kwa kushirikiana na shirika la VID Zanzibar, ZADIA ilitoa sadaka za vyakula na fedha taslim kwa familia zenye mayatima katika sehemu mbalimbli za Unguja na Pemba kwa ajili ya futari na Siku Kuu.
Mwenyekiti wa ZADIA, pia ameelezea shukrani zake za dhati kwa wale wote walichangia kwa njia moja au nyingine katika kufaniukisha zoezi hilo.
"Tunapenda kutoa shukrani za dhati kwa wale wote waliochangia pesa, ushauri, ufuatiliaji ugawaji na mpaka sadaka ile ikawafikia mayatima huko waliko, mijini na vijijini, Unguja na Pemba", alifafanua Mwenyekiti huyo, na kuendela: "Msaada wenu wa kufutarisha sio tu umewazesha walengwa kufarijika katika siku za mwisho wa Ramadhani, lakini pia ulizingatia misingi ya Utamaduni wa Kizanzibari ambao mayatima wanalelewa na ndugu na jamaa zao majumbani ili kuimarisha na kujenga ukoo badala ya kuwalea vituoni"
Taarifa hiyo imewasihi wanajuiya ya ZADIA kundelea na moyo huo wa ukarimu, na kujifunza kutokana na changamoto zilizojitokeza mwaka huu ili kuwa ni mwangaza wa kuendeleza shughuli hiyo kwa ufanisi zaidi katika mika inayofuata.
"Tafadhalini endeleeni na msimamo huo huo na kwa vile tumeanzisha utaratibu huu, tuujenge ili tuanze matayarisho ya hatua inayofuata ili tuweze kufanya shughuli hii kwa ufanisi ulio bora zaidi na kujifunza kutokana na changamoto zilizotokea katika harakati hizi kwa ujumla", ilimalizia taarifa hiyo.
Itakumbukwa kuwa Serikali ya Zanzibar ilipiga marufuku harakati za kufutarisha katika mfumo wa makundi kutokana na mripuko wa maradhi ya kipindipindu Visiwani Zanzibar.
Hata hivyo, Swahilivilla ilipata taarifa za baadhi ya mashirika na taasisi mbalimbali kuruhusiwa kuendesha shughuli za kufutarisha visiwani humo.

No comments: