Advertisements

Thursday, July 14, 2016

ZITTO AKOSOA MBUNGE WAKE KUTEMWA NA JPM



Kiongozi wa ACT, Zitto Kabwe
By Waandishi Wetu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Rais John Magufuli juzi alitumia muda mwingi kueleza jinsi mchakato wa kuteua wakurugenzi wa wilaya ulivyotawaliwa na umakini, akisema kuwa amepitia jina la kila mteule, lakini jina la Hidaya Usanga limetia doa.

Rais alikuwa akizungumza hayo muda mfupi baada ya jina la kada huyo wa zamani wa CCM aliyehamia ACT Wazalendo, kuondolewa kwenye orodha ya wakurugenzi walioteuliwa kuongoza moja ya wilaya za Mkoa wa Mara wakati wakisubiri kula kiapo.

Usanga, aliyegombea ubunge wa Jimbo la Malinyi mkoani Morogoro kwa tiketi ya ACT-Wazalendo baada ya kuanguka katika kura za maoni ndani ya CCM, aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Mji wa Tarime.

Lakini, tofauti na ilivyokuwa kwa Emile Yotham Ntakamulenga, aliyeteuliwa kuwa mkuu wa Wilaya ya Serengeti, uteuzi wa Usanga haukutenguliwa kwa kutangazwa kwa kutumia kipaza sauti, bali ulifanywa kimyakimya.

Baada ya kukamilisha taratibu zote za usaili, Usanga aliitwa na wateule wenzake wa wilaya za Mara na kuambiwa kuwa asingehusika kwenye kiapo, lakini hakuna taarifa rasmi iliyotolewa na Ikulu hadi sasa kuhusu kutenguliwa kwa uteuzi wa Usanga, ambaye amedai alirejea CCM tangu Januari 18.

Zitto apinga

Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe aliiambia Mwananchi jana kuwa ameshangazwa na kitendo cha Rais kutengua uteuzi wa Usanga, akisema amefanywa hivyo kwa sababu ya itikadi za kisiasa.

Zitto alisema Rais Magufuli amekuwa akisisitiza kuwa anafanya uteuzi wa nafasi za utumishi wa umma kwa kuangalia sifa na uwezo wa mtu na si chama anachotoka, lakini hilo limeonekana si kweli.

“Inakuwaje anamuengua mtu kwa sababu ya chama chake? Hizi ni nafasi za utumishi wa umma, ambazo hazina chama. Mtu yeyote anaweza kuteuliwa bila kujali chama chake,” alisema mbunge huyo wa Kigoma Mjini.

“Rais amekuwa akisema vitu ambavyo haviamini na ndiyo maana amemnyima Hidaya nafasi ya ukurugenzi kwa sababu anatoka chama cha upinzani.”

Zitto, ambaye bado anamtambua Usanga kama mwanachama wa ACT, alisema amegundua mambo matatu ndani ya utawala wa sasa wa awamu ya tano.

“Kwanza Ikulu hawako makini katika uteuzi, kwa sababu huyu (Usanga) alikuwa mgombea wa ubunge na ipo katika rekodi, sasa kwa nini hawakulijua hilo mapema, mpaka wanakwenda kushtuka dakika za mwisho,” alisema Zitto.

“Jambo jingine ambalo nimeligundua ni kuwa Rais ana ubaguzi wa vyama, lakini pia hana ubinadamu kwa sababu huwezi kuwa unafukuza watu Ikulu, hii ni kuharibu sifa ya Ikulu.”

Akizungumza kwenye hafla ya kuapisha wakurugenzi hao juzi, Rais alisema mchakato huo ulikuwa makini na ulichukua zaidi ya miezi minne.

“Kwa hiyo tulianza uchambuzi wa kina kwelikweli. Mmepitia kwenye milolongo mingi kwelikweli. Vyombo mbalimbali vimehusika,” alisema Rais.

“Lengo lilikuwa moja tu; ninataka kujenga Tanzania ya aina gani? Na je, nichague watu wa aina gani watakaoifikisha hiyo Tanzania ninayoitaka na ndiyo maana process (mchakato) ilikuwa ndefu.

Alisema anamjua kila mtu aliyeteuliwa na amepitia kila jina na kwamba alikuwa analazimika kulala usiku wa manane kupitia majina hayo.

Lakini kutoapishwa kwa Usanga kunatia doa jingine kwenye umakini wa vyombo vinavyomsaidia Rais kufanya uteuzi.

Katika uteuzi wa viongozi wa Serikali za wilaya uliofanywa katika siku za karibuni na Ikulu, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) na Tamisemi, ambayo zamani ilikuwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, imelazimika kufanya marekebisho muda mfupi baada ya majina kutangazwa.

Awali, Utumishi ilitangaza majina ya watu 134 walioteuliwa kuwa makatibu tawala wa wilaya, lakini Rais Magufuli akatengua uteuzi wa baadhi yao na kuwaweka kwenye timu yake ya wakurugenzi wa wilaya iliyotangazwa baadaye.

Taarifa iliyotumwa na Ikulu ilisema kuwa “Rais Magufuli ameamua kuwabadilishia majukumu na sasa watatumikia vyeo vyao vya ukurugenzi badala ya ukatibu tawala wa wilaya”.

Taarifa hiyo haikubainisha majina yaliyojitokeza kwenye nafasi mbili tofauti ambayo wahusika walikula kiapo juzi tayari kuanza majukumu hayo ya kiserikali.

Muda mfupi baada ya kutangazwa kwa wakurugenzi hao, Zitto alionyesha makosa yaliyofanywa na Ikulu alipoandika kwenye ukurasa wake wa Facebook.“Naamini bado wengine watapata uteuzi humu ndani maana kuna makosa ambayo yatafanya nafasi ziwe wazi.”

Zitto aliwataja walioandikwa mara mbili kuwa ni Dk Leonard Massale, ambaye aliteuliwa kuwa DC wa Ilemela lakini amepangiwa kuwa DED wa Wilaya ya Dodoma. Taarifa ya Ikulu ilirekebisha kasoro hiyo kwa kusema: “Jina hilo limeingizwa katika orodha ya wakurugenzi kwa makosa. Dk Leonard Moses Massale ataendelea kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.”

Kutokana na marekebisho hayo, Ikulu ilisema uteuzi wa mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma utatangazwa baadaye. Ma - DAS ambao Zitto aliwataja kuteuliwa tena ni Justin Joseph Monko aliyepangwa wilayani Musoma na akuteuliwa kuwa mkurugenzi wa Wilaya ya Liwale na Hanji Yusuph Godigodi, aliyeteuliwa kuwa DAS wa Kyerwa, lakini kwenye uteuzi huo amepangiwa Wilaya ya Kigoma.

Pia yumo Joel Mwakibibi aliyepelekwa Biharamulo kuwa DAS, lakini akateuliwa kuwa DED wa Kakonko, Kigoma.

Kasoro nyingine zilizojitokeza na kulazimisha Ikulu kusahihishwa ni za nafasi mbili za wakuu wa wilaya ambazo zilirekebishwa kabla ya kiapo. Lakini ikasahau na ikamualika Ntakamulenga, aliyetangazwa kuwa mkuu wa Wilaya ya Serengeti lakini aliondolewa katika viwanja vya Ikulu muda mfupi kabla ya kula kiapo cha maadili na nafasi yake akapewa Nurdin Babu, ambaye pia alikuwapo eneo hilo.

Mtazamo wa wadau

Wadau waliozungumza na Mwananchi jana walikosoa kitendo cha Ikulu kuondoa jina la Ulanga kwenye uteuzi wa wakurugenzi wa wilaya, wakituhumu kuwa kilitokana na itikadi za kisiasa.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda alisema Rais Mafuguli aliweka wazi tangu awali kwamba maendeleo yataletwa na watu wote bila kuangalia chama.

“Lakini tunachoona sasa ni tofauti na kauli zake za mwanzo,” alisema Mbunda.

Mhadhiri huyo alitoa mfano wa kauli aliyotoa Rais juzi Ikulu kuwa hawezi kumchagua mtu ambaye si mwanachama wa CCM kwa sababu haamini sera za chama hicho.

“Tungetaka kuona kauli zake za awali zinafanya kazi. Tunashuhudia sasa ni mkanganyiko wa kauli na uteuzi wake,” alisema Mbunda.

Alisema wengi wanaopewa nafasi hizo ni makada wa chama hicho ambao walikosa nafasi mbalimbali kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita.

Maoni hayo yalikinzana na yale ya Dk Benson Bana wa chuo hicho ambaye alisema ni jambo la busara kwa mkurugenzi huyo mteule kuondolewa mapema. Ameondolewa kistaarabu. Asingeondolewa ingeleta shida baadaye,” alisema.

Dk Bana alibainisha kuwa kanuni na taratibu za uteuzi wa wakurugenzi haziruhusu mtu ambaye aligombania nafasi ya uongozi kwenye uchaguzi na kukosa, kupewa nafasi kama ilivyo kwenye nafasi za ukuu wa wilaya.“Ukurugenzi wa halmashauri ni utumishi wa umma, haupaswi kufungamana na upande wa chama chochote.” alisema.

“Anatakiwa kuwa mwanachama mwenye kadi yake mfukoni, lakini si aliyewahi kusimama jukwaani. Ule si ubaguzi, ni utaratibu, alisema Bana.”

Alipotafutwa na gazeti hili kutoa ufafanuzi kuhusu suala hilo, msemaji wa Ikulu, Geryson Msigwa alisema hana taarifa za tukio hilo.“Cheki na Tamisemi,” alisema.

Hata hivyo, Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene hakupatikana jana kuzungumzia suala hilo.

Nyongeza na Suzan Mwilo

4 comments:

Anonymous said...

Who listens to this guy Zitto? Increasingly he is becoming petty and irrelevant. Magufuli has pulled the rug under their agenda sasa hawana muelekeo!!

Anonymous said...

Zito mbunge wako sio mtu makini huwezi kukihama chama kwa sababu umeshindwa katika kura za maoni na pengine wananchi ndio waliopendekeza kuwa hafai hii inaonesha yakwamba alikuwa msaliti ndani ya CCM pengine akiendeleza hujuma kwa manufaa ya ACT wazalendo halafu utarajie CCM kumpongeza? Nnaimani hata angepewa huo ukurugenzi basi angeendeleza hujuma zake kwa nafasi alionayo ili serikali ya Magufuli ionekane haifai. Sawa sawa tu kwa Magufuli kutomchagua kwani jamaa anaonekana sio mtu mwenye dhamana.

Anonymous said...

Maskini Zitto. Mtapatapaji tu.

Anonymous said...

asipotapatapa atapata wapi kula? ujanja mjini sharti upige kelele usikike ili upate umaarufu hata kama ujinga mtupu