Advertisements

Friday, August 12, 2016

CHADEMA INAVYOPANGUA KETE YA CCM



Mwenyekiti wa Chadema Taifa,Freeman Mbowe.
By Suzan Mwillo, Mwananchi

Dar es Salaam. Wakati Serikali ya CCM imekuwa ikijenga mazingira ya kuzuia uwezekano wa vyama vya upinzani kufurukuta, Chadema imekuwa ikichanga karata zake na kuendelea kujiimarisha na kushindana kisiasa na chama tawala.

Kwa mujibu wa baadhi ya wasomi na wanasiasa nchini, matukio makubwa ya kisiasa yanayoandaliwa na Chadema na kuibua mijadala imekuwa ikifanywa kimkakati sambamba na ya chama tawala, CCM.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda aliliambia Mwananchi kwamba aonavyo yeye matukio mbalimbali ya Chadema ni mikakati ya kisiasa. “Inabidi wafanye matukio ili chama kiendelee kubaki katika ramani ya siasa,”alisema Mbunda.

Mwenyeki wa Chadema, Freeman Mbowe amesema tofauti na mawazo ya baadhi ya watu, matukio hayo zikiwamo operesheni mbalimbali za chama si mikakati ya kudumu bali ni za muda maalumu kwa malengo maalumu ambayo ikikamilika wanabuni mbinu nyingine.

Chadema wamekuwa wakibuni mikakati mbalimbali ya kuwafikia wananchi tangu mikutano na maandamano ya vyama vya siasa ilipopigwa marufuku na Rais John Magufuli hadi mwaka 2020. Mikutano iliyoruhusiwa ni ya wabunge tu tena katika majimbo yao, lakini si ya wanasiasa.

Katika Bunge la Bajeti, wabunge wa Chadema wakishirikiana na wenzao kutoka vyama vya siasa vinavyounda Ukawa walikuwa wakisusa vikao kwa staili tofauti. Kuna siku walitoka nje wakiwa wamevaa mavazi meusi, siku nyingine walibandika vitambaa mdomoni na kuna siku walibeba mabango yenye ujumbe mbalimbali.

Julai mwaka huu, CCM ilipoandaa mkutano maalumu uliopangwa kwa ajili ya kumkabidhi Rais Magufuli kijiti cha uenyekiti wa chama hicho, Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) lilizua hofu lilipotangaza kwamba litakwenda pia Dodoma kulisaidia Jeshi la Polisi kuzuia mkutano huo kwa kuwa Serikali ilipiga marufuku mikutano ya ndani na nje.

Hatua hiyo ya Bavicha ilisababisha Jeshi la Polisi kuweka ulinzi mkali kila kona mjini Dodoma kuzuia uwezekano wa Bavicha kuvuruga mkutano huo wa CCM. Hata hivyo, Bavicha walipiga chenga, walikutana Dar es Salaam ambako walifanya mkutano wao.

Wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM walipokuwa katika shangwe na nderemo baada ya kukamilisha ajenda yao ya kumchagua kwa asilimia 100 Rais Magufuli, Kamati Kuu ya Chadema iliketi Dar es Salaam na kutoka na mkakati wa kupinga uvunjaji wa Katiba na sheria waliouita operesheni Ukuta ambao unasumbua vyombo vya usalama hadi sasa.

Matukio hayo ambayo yametokea kwa kufuatana yamekuwa yakigonga vichwa vya habari huku baadhi wakidai ni dalili za vurugu na uchochezi, lakini pia yanakiweka chama hicho kwenye mjadala kuliko vingine.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa waliotafutwa na gazeti hili jana kuzungumzia namna Chadema inavyocheza karata zake kuhakikisha inasikika sawa au hata kuifunika CCM, wamesema huo ni mkakati wa upinzani kuendelea kutamba kwenye ‘ulingo wa siasa.’ Baadhi ya operesheni zilizoijengea umaarufu ni kama Sangara na Movement For Change (M4C).

Akizungumzia mfuatano wa matukio hayo, Mbunda amesema aonavyo yeye matukio hayo ni mikakati ya kisiasa akibainisha kuwa kila chama kina wapangaji mikakati ambao hupanga na kutathmini mikakati hiyo. “…Siyo mikakati yote inayofaulu. Wakiona huu haufai wanaweza kubadili.”

Mhadhiri huyo alitoa mfano wa Operesheni Ukuta ya Chadema iliyopangwa kufanyika Septemba Mosi mwaka huu kwamba huenda wakati ukifika chama hicho kikabadili uamuzi wake baada ya kufanya tathmini ya operesheni hiyo.

Mbunda amesema kwamba hizo ni amsha amsha ambazo husaidia vyama hasa vya upinzani kuendelea kuonekana katika uso wa siasa na kwamba vyama mbalimbali duniani hutumia mbinu hizo hivyo siyo jambo la kushangaza. “Wasipofanya hivyo hata watu watahoji kwa sababu hayo ndiyo maisha ya siasa,”alisema Mbunda.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Dk Benson Bana ambaye alisema kinachofanywa sasa na Chadema ni mkakati wa kuendelea kubaki na kusikika kwenye uwanja wa siasa.

Dk Bana, ambaye ni mhadhiri wa UDSM amesema chama hicho kinafanya hivyo ili kisipotee kwenye ramani ya siasa hadi Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Mchambuzi huyo wa masuala ya siasa alibainisha kuwa chama hicho kikuu cha upinzani kinafanya hivyo kwa sababu kilikuwa hakijajipanga kuona Serikali ya awamu ya tano inatekeleza baadhi ya ajenda zao.

“Hawajajipanga kuwa na mikakati endelevu…wanaona wamenyang’anywa tonge mdomoni. Mikakati yao ni ya kuziba ombwe hilo,” alisema.

Pia, Dk Bana amesema jambo hilo siyo baya kwenye ulimwengu wa siasa tatizo ni aina ya mikakati kwamba Chadema inapaswa kuja na mikakati ambayo inakidhi haja ya Watanzania siyo mikakati ya kumwita Rais John Magufuli dikteta. “Watathmini mikakati yao. Waje na mikakati yenye mashiko,”amesema Dk Bana.

3 comments:

Anonymous said...

Kufanya vituko ili kuendelea kufahamika kama mkakati wa kiasiasa haiwezi kuwa sababu ya kuharibu amani na utulivu wa nchi yeyote ile. Sijui kwanini hata Polisi hawafanyi kama wenzao wa Marekani wanavyofanya. Kwa mfano, maandamano pale Umoja wa Mataifa, unapewa saa wakati mwingine hata dakika za protest yenu. Mnaambiwa kutaneni kwa kuanzia mtaa kadhaa piga kona kwenda mtaa kadhaa kutaneni hapo kwa saa moja Kisha funga duka. Ukikaidi kipigo kama kazi. Nasi ni vyema tuwape fursa kwa masharti ili kulinda amani na utulivu. Wakikaidi mbaroni tu. Wako watu wengi hawana kazi wako tayari kudanganywa na wanasiasa. Lakini wakati tunawapa fursa ya kudanganywa hatuna budi kulinda kwanza amani na utulivu wetu. Tumuache Magufuli afanye kazi yake ambayo Watanzania wengi walimpigia kura na kumkabidhi. Mengine tungojane 2020. Hiyo ndiyo siasa. Itakuwaje wengine wahalioni hilo. Hakuna nchi iliyoendelea kwa kupiga siasa tu. Sasa Kazi tu siasa baadae.

Anonymous said...

Uchambuzi pumba kabisa. Yaani kama alivyosema Maghufuli upizani ikiwemo chadema sawa na nyoka aliekatwa kichwa kamwe mkia wake hautoacha kutikisika lakini ameshakufa zamani. Kiuhalisia hii makala imeandaliwa na watu wa chadema na hao wanaojiita wasomi watafiti ni watu wa Chadema sasa hapo huoni yakuwa ni huo mkia unaotikisika wa nyoka aliekwisha kufa. Hao Chadema washindwa na CCM goi goi ya kikwete,CCM iliokuwa na kila aina ya udhaifu,CCM iliojaa kila aina ya majipu mwili mzima yaani tunaweza kusema CCM ya wakati ule was a dead man walking in the street na Chadema wakati ule ipo katika ubora wake hasa Zito,Dk Slaa na maamluki Lowasa na ufisadi wake akitafuna CCM chini kwa chini na walishindwa kuiangusha CCM. Sasa hii CCM ya Mzee wa hapa kazi,mzee wa serikali ya uwazi zikipatikana shillingi kumi Magufuli anawaambia watanzania tumepata kiasi kadhaa na tumetumia kiasi kadhaa na kwa kitu fulani. Yaani watanzania wamekatwa kiu yao ya kupata kiongozi waliokuwa wakimtafuta kwa miaka mingi sana. Yaani wazungu wanasema Magufuli is hitting the spot katika nyoyo za watanzania kwa mambo anayoyafanya. Ni ajabu kusoma yakwamba haya makala hapo juu yamefanyiwa upembuzi yakinifu na wasomi na kama kweli hawa ni wasomi wetu wanaosomesha vio vyetu vikuu basi haishangazi hata kidogo kuona Tanzania tupo nyuma katika nyanja mbali mbali.mimi sikusoma lakini nikiiangalia hali ya siasa nchini Tanzania najuwa yakwamba wapinzani wapo katika changamoto nzito sana ya kuipiku CCM ya Magufuli.Wana kazi nzito ya kuizidi kete CCM ya Magufuli. Huo ndio ukweli halisi na hizo blah blah nyengine ni furahisha baraza. Na hakuna jambo baya zaidi litakalo waharimu upizani hasa chadema kama kujifananisha kinguvu na CCM lol, ni makosa makubwa. Ushauri wa bure kama mimi ningelikuwa miongini mwa viongozi wa upizani hasa chadema basi kuachana na siasa za vitisho na mapambano na serikali kwani huko ni kuwajengea mtaji CCM. Kete ya kuvurugwa kwa amani ni mtaji nambari moja wa CCM kujijenga kwa wananchi na badala yake chadema wanatakiwa kujikita zaidi vijijini yaani kurudi vijijini na kujijenga zaidi kwa kuhubiri amani na maendeleo badala ya vitisho na maandamano.Watanzania ni watu wanaoiabudu amani sasa kumsikia mtu anasherekea maandamano japo ni halali kwa mtanazamo wa watanzania wengi mtu kama huyo huwa kapotoka . Kwa vijana wa mjini sawa lakini huwezi kuipiga CCM kwa kura za mjini peke yake.

Anonymous said...

Upinzani huu ni bankrupt. They are grappling for relevance and appeal. They have found none. They have no agenda but their leaders self interests. The state of our opposition leaders is pathetic and a tragedy for our country. We deserve a better opposition better.