Advertisements

Friday, August 19, 2016

DAKIKA 90 ZAWAPA MAISHA MAPYA PACHA WA KYELA MUHIMBILI

Daktari bingwa wa upasuaji wa watoto katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili , Dk Victor Ngotta (kushoto) akimfanyia upasuaji Eliudi Joel kwa kushirikiana na Profesa Saber Waheeb (katikati) na Dk Mohamed Malak kutoka Misri (kulia). Madaktari hao wamefanikisha kuwafanyia upasuaji watoto pacha ambao walikuwa wana tatizo katika njia mkojo. Picha na John Stephen
st2

By Herieth Makwetta, Mwananchi hmakweta@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa kushirikiana na jopo la madaktari bingwa kutoka Misri, wakitumia dakika 90, jana walifanikisha upasuaji wa kurekebisha tatizo katika njia ya mkojo kwa watoto pacha waliokuwa wameungana Eliud na Elikana Mwakyusa (3) wakazi wa Kasumulu, Kyela, Mbeya.

Katika upasuaji wa awali wa kuwatenganisha uliofanyika India, watoto hao waliwekewa njia za dharura za mkojo lakini jana wamewekewa za kudumu.

Baada ya upasuaji huo uliofanyika kwa nyakati tofauti kukamilika watoto hao walirejeshwa wodini na hadi jana jioni walikuwa wakiendelea kuimarika kiafya.

Daktari bingwa wa upasuaji wa watoto, Zaituni Bokhary na mwenzake, Yona Ringo ndiyo waliofanya upasuaji wa Elikana, wakati Eliudi alifanyiwa upasuaji na Profesa Saber Waheeb na Dk Mohamed Malak kutoka Misri kwa kushirikiana na Dk Victor Ngotta na Dk Mwajabu Mbaga wa Muhimbili.

Akizungumza mara baada ya upasuaji huo jana jioni, Dk Bokhary alisema kazi hiyo ilichukua saa 1.30 na kwamba hivi sasa wanaendelea vizuri.

“Watoto hawa wataendelea kubaki wodini hadi watakapopona vizuri ndipo tutawaruhusu, upasuaji umekwenda vizuri na watoto wameshawekewa njia za kudumu,” alisema Dk Bokhary.

Alisema mbali ya Elikana na Eliud, watoto wengine wawili waliokuwa na tatizo kama hilo nao walifanyiwa upasuaji jana.

Juzi, madaktari wa hospitali hiyo walianza upasuaji kwa watoto wenye matatizo ya njia ya mkojo na haja kubwa, sambamba na mfumo wa hewa na chakula.

Watoto hao waliozaliwa Februari 20, 2013, wilayani Kyela wakiwa wameungana kiunoni, walitenganishwa kwa upasuaji uliofanyika India kwa gharama za Serikali.

Baada ya kufanikiwa kuwatenganisha, watoto hao walitengenezewa sehemu maalumu ya dharura ya kutolea haja kubwa na ndogo eneo la tumboni na walirejea kijijini kwao Kasumulu Kyela, Februari 27, 2014.

No comments: