Advertisements

Wednesday, August 10, 2016

DC KALIUA AAHIDI KUWATUMBUA WATENDAJI WAZEMBE

Na Musa mbeho, Kaliua

MKUU wa wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora Abel Yeji ameapa kuwatumbua Wenyeviti na Watendaji wa Vijiji na Kata wanaoshindwa kutekeleza wajibu wao kwa wananchi ikiwemo kusoma taarifa za mapato na matumizi katika maeneo yao.

Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana mjini Kaliua Yeji alisema watendaji wa vijiji na kata wanapaswa kuwa karibu zaidi na wananchi wao na kuelewa kero zote zinazowakabili ikiwemo kuzitafutia ufumbuzi.

Alisema kitendo cha watendaji hao kujifanya miungu watu wakati hawawatumikii wananchi ipasavyo ikiwemo kutoitisha mikutano ya hadhara ya kutoa taarifa za maendeleo na kusoma taarifa za mapato na matumizi hakiwezi kufumbiwa macho, ni uzembe wa hali ya juu.

‘Hawa watendaji wanajifanya miungu watu katika vijiji na kata zao, hata ushirikiano na wananchi hawana, ndio maana hawaitishi mikutano wala kusoma taarifa za mapato na matumizi, na Wenyeviti wamekaa tu’,alihoji zaidi.

Ili kukomesha hali hiyo alimwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo John Marko Pima kuwachukulia hatua watendaji wote wa vijiji na kata wenye tabia za namna hiyo.

Aidha aliwaomba madiwani kuhakikisha kila Mtendaji anawajibika ipasavyo kwa wananchi wake ikiwemo kutoa taarifa za miradi ya maendeleo katika kijiji na kata husika na kusoma ripoti ya mapato na matumizi.

‘Ndugu zangu Madiwani naomba sana mnisaidie katika hili, nataka kuona ufanisi wa hawa watendaji vinginevyo nitawatumbua ’, aliongeza.

Katika Mkutano huo DC Yeji alitoa tamko la serikali la kuruhusu mikutano ya hadhara kwa wanasiasa yenye lengo la kuhamasisha maendeleo katika vijiji, kata na majimbo na sio maandamano kwa kuwa hayana tija ya kimaendeleo.

Alisisitiza kuwa viongozi wote waliochaguliwa na wananchi katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwaka jana wanaruhusiwa kufanya mikutano ya kisiasa katika maeneo yao lengo
likiwa kuhamasisha amani, utulivu na maendeleo ya wananchi.

‘Ndugu zangu wanasiasa mikutano inayotakiwa kwa kipindi hiki ni ya kuhamasisha maendeleo ya wananchi na sio maandamano, kwa kuwa hayana tija kwa maendeleo ya wananchi’, alibainisha.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo Haruna Kasele alibainisha wazi kuwa baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu sasa kilichobaki ni kazi tu na kila kiongozi awe wa kitongoji, kijiji, kata au jimbo
anapaswa kutekeleza wajibu wake wa kuwaletea maendeleo wananchi na sio vinginevyo.

‘Naomba hili lieleweke, DC wetu yuko wazi, kampeni zilishaisha kilichobaki ni utekelezaji wa ahadi za maendeleo kwa kila kiongozi aliyepewa ridhaa na wananchi, na sio kuzunguka nchi nzima kwa
maandamano yasiyo na tija’, aliongeza Kasele.

No comments: