Advertisements

Wednesday, August 10, 2016

GAZETI LA MSETO LATAKIWA KUOMBA RADHI NA KUMLIPA FIDIA YA BILIONI MOJA WAZIRI WA UJENZI MHE. NGONYANI

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi. Edwin A. Ngonyani

Na: Abushehe Nondo, MAELEZO 
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi. Edwin A. Ngonyani amelitaka gazeti la Mseto kumuomba radhi na kumlipa fidia ya shilingi bilioni moja kutokana na kuandika habari ya kumchafua.

Akizungumza na waandishi wa habari Ofisi kwake Waziri Ngonyani amesema kuwa Gazeti hilo la tarehe 4 Agosti 2016 liliandika habari yenye kichwa cha Habari, Waziri amchafua JPM ikimuhusisha na upokeaji wa fedha kutoka moja ya Kampuni ya Madini wakati akiwa Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa (Stamico).

Nimewaandikia notisi ya siku saba ikiwataka waombe radhi na kunilipa fidia, na wasipofanya hivyo hatua stahiki kuwapeleka mahakamani akiwemo Mwandishi Josephat Isango, Mwanahalishi Publisher na Mchapaji wa gazeti hilo. Alisema Mhandisi Ngonyani.

Mhandisi Ngonyani amesema kuwa habari hiyo siyo ya kweli na mwandishi ametumia nyaraka za kughushi ikiwemo barua iliyoandikwa tarehe 24 Julai na kutiwa saini yake akiwa Kaimu Mkurugenzi wa STAMICO wakati ukweli ni kwamba tarehe hiyo yeye alikuwa ni Mkurugenzi kamili na siyo Kaimu kama barua hiyo inavyosomeka.

Ameongeza kuwa habari hiyo imewachafua watu wengi ikiwemo familia yake, wapiga kura wake wa jimbo la Namtumbo ambao walijitoa katika kumsaidia wakati wa kampeni na hali kadhalika zimemchafua Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kumhusisha na fedha kutoka kwa wawekezaji wa nje kwa kuwaahidi kuwa mitaji yao nchini itakuwa salama. Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli alishasema kama kuna mfanyabiashara yeyote aliyechangia kuingia kwake ikulu ajitokeze na hakuna aliyefanya hivyo, Iweje leo mtu tu anaibuka na kuandika habari za kugushi. Aliongeza.

Aidha Naibu Waziri huyo ametumia fursa hiyo kuwataka waandishi wa habari nchini kuwa waangalifu pindi wanapoandika habari za kutunga kwa kutotumia majina halisi kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na kanuni za uandishi wa hadithi (Habari za kutunga).

Waandishi wa habari mnatakiwa kufuata maadili ya kazi yenu kwa kuandika habari zenye ukweli ili kuliepusha taifa kuingia katika machafuko na migogoro isiyo ya lazima .Alisema Naibu waziri huyo.

No comments: