MBUNGE wa zamani wa Jimbo la Kahama, James Lembeli, ameibukia katika mkutano wa Rais, Dk. John Magufuli, huku akimwomba kiongozi huyo kuhakikisha anakisafisha Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Lembeli ambaye mwaka jana alijiengua ndani ya CCM na kujiunga na Chadema, alisema ikiwa Rais Magufuli atafanya hivyo, yuko tayari kurejea CCM.
Mwanasiasa huyo aliondoka CCM kwa kile alichodai kuwa chama hicho kimekithiri vitendo vya rushwa pamoja na unafiki miongoni mwa wanachama na viongozi wake.
Lembeli alizungumza jana mjini Kahama baada ya kuitwa kuwasalimia wananchi katika mkutano wa Rais Magufuli, ambaye anaendelea na ziara yake ya kuwashukuru Watanzania kwa kumchagua.
“Iwapo mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli atakisafisha chama hicho basi na mimi ninaweza kurudi katika chama hicho kwa lengo la kuwahudumia wananchi,” alisema Lembeli.
Alimshukuru Rais Magufuli kufika wilayani Kahama, ambapo alisema hana kinyongo na kwamba ataendelea kusalimiana na watu mbalimbali, kwani kubadili msikiti si mwisho wa uislamu.
“Kama Rais Magufuli, atakisafisha chama hicho sina budi kurudi kundini kwani kwa sasa bado nasubiri kiongozi huyo aisafishe CCM,” alisema
Akizungumza na wananchi wa Mji wa Kahama, Rais Dk. Mgufuli, alisema yote aliyoyaahidi atayafanyia kazi na kuongeza kuwa hatalewa madaraka ya urais na kuwataka Watanzania kumtanguliza Mungu katika kazi wanazozifanya za kila siku.
“Wana Kahama tambueni kuwa Lembeli ni rafiki yangu wa siku nyingi na kuwepo kwake hapa ninategemea mabadiliko makubwa kutoka kwake na ninakushauri urudi Tanzania kwani ulikokwenda ulikuwa umepotea njia,” alisema Rais Mgufuli.
Pamoja na hali hiyo Rais Magufuli, alimtaka Lembeli, kurejea ndani ya CCM kwani chama alichokuwa nacho kwa sasa ndipo walipo mafisadi aliokuwa akiwazungumzia kila siku.
Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM taifa, alisema katika kuonesha dhamira ya kupambana na ufisadi, tayari Serikali yake imetenga Sh bilioni 2.5 kwa ajili ya kuwashughulikia mafisadi.
“Ninakuomba Lembeli urudi kundini mimi ninakujua unavyowapenda wananchi wako wa Kahama na ukirudi sita kukata mkia kwani huko ulikokwenda umepotea njia na mimi ndiyo mwenyekiti ninayewapinga wasaliti ambao asubuhi wapo CCM jioni wapo upinzani,” alisema Magufuli.
Awali akizungumza katika mkutano huo kwa niaba ya vyama vya upinzani, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Wilaya ya Kahama, Rajabu Yahaya, alimpongeza Rais Magufuli na kusema kuwa kazi inayofanywa kwa sasa na kiongozi huyo ndiyo ilikuwa ikipiganiwa na wapinzani kwa miaka yote.
CHANZO: MTANZANIA
No comments:
Post a Comment