Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima
Tanzania, Josephat Gwajima, akitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
jijini Dar es Salaam jana, kusikiliza kesi inayomkabili ya kutoa lugha ya matusi
na kukutwa na silaha. (Na Mpiga Picha Wetu).
Na MwandishiWetu
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es
Salaam, imeahirisha kesi ya kutoa lugha ya matusi na kukutwa na silaha zinazomkabili Askofu Mkuu
wa Kanisa la Ufufuo na Uzima Tanzania, Josephat Gwajima, kutokana na hakimu
anayesikiliza shauri hilo kutokuwapo.
Kesi hiyo iliahirishwa leo na Hakimu Mkazi Magreth Bankika,
ambaye alisema kesi hiyo itaendelea kusikilizwa Septemba 2, mwaka huu.
Askofu Gwjima alikuwapo mahakamani wakati kesi
hiyo ikiahirishwa, ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu iliporipotiwa kuwa ni
mgonjwa.
Askofu Gwajima alifika mahakamani hapo saa 2:00
asubuhi akiongozana na walinzi pamoja na wafuasi wake.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro,
aliieleza mahakama kuwa shauri hilo limetajwa kwa ajili ya kusikilizwa na
shahidi mmoja alikuwapo, lakini wamepata taarifa kuwa hakimu anayesikiliza
shauri hilo hayupo, hivyo kuiomba mahakama kupangiwa tarehe nyingine.
Hakimu Bankika aliahirisha kesi hiyo hadi
Septemba 2, mwaka huu itakapoendelea kusikilizwa.
Katika kesi hiyo ambayo Askofu Gwajima anatetewa
na Wakili Peter Kibatala, anadaiwa kati ya Machi 16 na 25, mwaka huu katika
viwanja vya Tanganyika Packers, vilivyopo Kawe, jijini Dar es Salaam, alitoa
lugha ya matusi dhidi ya Askofu wa Kanisa Katoliki, Mwadhama Policarp Kardinali
Pengo, jambo ambalo lingeweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Hivi karibuni Askofu Gwajima akiwa nje ya nchi, Jeshi
la Polisi lilitangaza kumsaka kwa ajili ya kumhoji kutokana na mahubiri
aliyoyatoa Juni 11, mwaka huu kanisani kwake Ubungo.
Katika mahubiri hayo yaliyosambaa katika mitandao
mbalimbali ya kijamii, askofu huyo alisikikika akiukosoa utendaji kazi wa Rais
mstaafu Jakaya Kikwete na kumtaka Rais John Magufuli kumchukulia hatua kutokana
na mabaya aliyoyafanya katika utawala wake.
Alipojea nchini alikamatwa na polisi katika
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam na kuhojiwa kwa
saa kadhaa na kuachiwa.
No comments:
Post a Comment