Advertisements

Friday, August 12, 2016

KICHANGA CHAIBIWA MOROGORO 2013 CHAPATIKANA DAR

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Leonce Rwegasira
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Leonce Rwegasira

POLISI mkoani Morogoro inawashikilia wanawake wawili, wakazi wa Mbezi jijini Dar es Salaam, Sarafina Henry (28) na Johari Hussein (22) kwa tuhuma za wizi wa mtoto wa kike ( jina lake limehifadhiwa) na kuishi naye tangu mwaka 2013 hadi Agosti 7, mwaka huu.

Mtoto huyo alipoibwa, alikuwa na umri wa mwaka mmoja na nusu na amepatikana akiwa ametimiza umri wa miaka minne na nusu, huku watuhumiwa hao wakimwandaa kumwanzisha kusoma elimu ya awali (chekechea).

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Leonce Rwegasira alisema jana kuwa watuhumiwa hao walikamatwa Agosti 7, mwaka huu Kawe jijini Dar es Salaam.

Rwegasira alisema wanawake hao walimwiba mtoto huyo Julai 4, 2013 saa 11 jioni maeneo ya Karume Manispaa ya Morogoro akiwa na umri wa mwaka mmoja na nusu.

Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi, mama mzazi wa mtoto huyo aitwaye Ashura Shabani (33) mkazi wa Karume katika Manispaa ya Morogoro aliripoti Kituo Kikuu cha Polisi mjini hapa kuwa mtoto wake huyo ameibwa katika mazingira ya kutatanisha.

Akielezea tukio hilo kulingana na maelezo ya mama mzazi wa mtoto huyo, mtoto wake aliibwa baada ya wanawake wawili waliofika nyumbani kwake kwa ajili ya kutaka huduma za kusuka nywele.

Alisema wanawake hao walifanikisha uhalifu huo baada ya ndugu wa mama wa mtoto huyo kwenda dukani kufuata rasta na ndipo walipomrubuni awape mtoto wambebe na mmoja wao kumbeba na kisha kutokomea kusikojulikana kwa kipindi chote tangu 2013 hadi Agosti 7, mwaka huu.

Akizungumzia mazingira ya kukamatwa kwa watuhumiwa hao, alisema mdogo wa mama mwenye mtoto aliyeibwa akiwa anaishi eneo la Kawe jijini Dar es Salaam, alimwona mwanamke mmoja akiwa amembeba mtoto anayefanana na wa dada yake, ambaye aliibwa kipindi kirefu siku siku za nyuma.

Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi, mdogo huyo baada ya kumwona mwanamke huyo akiwa na mtoto huyo, alikwenda kutoa ripoti Kituo cha Polisi Kawe, ambako Askari Polisi walifanya uchunguzi na kufanikiwa kumkamata Johari Hussein ambaye alikutwa na mtoto huyo.

Baada ya kuhojiwa kama mtoto huyo ni wake, Johari alikataa na kusema kuwa hajawahi kuwa na mtoto isipokuwa mtoto aliyekuwa naye ni wa dada yake, ambaye ni Sarafina na alimpeleka ili amwezesha kwenda kuandikishwa shule ya watoto iliyopo eneo la Kawe.

Kaimu Kamanda alisema baada ya kufika nyumbani kwa dada yake huyo, aliyekuwa amemwachia mtoto na alipohojiwa, alidai mtoto huyo alimzaa akiwa Mwanza alipokuwa akiishi kabla ya kuhamia Dar es Salaam.

Aliongeza kuwa baada ya kuhojiwa kwa kina, mwanamke huyo alidai hakuwa na mtoto isipokuwa mtoto huyo alitelekezwa na mama yake na yeye aliamua kumchukua na kukaa naye kipindi chote hicho. Alisema uchunguzi unaendelea kufanyika na kwamba watuhumiwa hao watafikishwa kwenye vyombo vya sheria kujibu tuhuma za makosa yao.

Kwa upande wao, watuhumiwa hao walijitetea kwa nyakati tofauti, mmoja akisema mtoto huyo aliletewa na dada yake ili amsaidie kumwandikisha shule, wakati mtuhumiwa wa wizi wa mtoto huyo akidai alimchukua mtoto huyo akiwa mdogo baada ya kutelekezwa na mama yake huyo na kuamua kuishi naye kama mwanawe wa kumzaa.

Mama mzazi wa mtoto huyo, Ashura alilaani vitendo vinavyofanywa na baadhi ya wanawake wenzao kuiba watoto, kwa kuwa ni dhambi kubwa na matukio hayo yanawaletea majonzi na uchungu zaidi wanawake wanaotendewa matukio hayo.

HABARI LEO

No comments: