ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 6, 2016

Kuna tofauti ya utawala wa sheria na sheria ya utawala

Viongozi wa Chadema wakiwa wameshikana mikono kuonyesha mshikamano. Picha ya Maktaba

By Idd Hamis, MWANANCHI

Inaelekea kuna ‘bundi’ anainyemelea nchi yetu taratibu na huenda watu wamechoka amani iliyopo.

Kutunishiana misuli kunakoendelea kati ya Chadema na Serikali hakuashirii heri hata kidogo.

Chadema kimetangaza uamuzi wa mkutano wa Kamati Kuu ya chama hicho kwamba Septemba mosi itakuwa siku ya kufanya mikutano na maandamano ya amani kupinga walichokiita “utawala wa kidikteta”.

Kwa sisi tuliosoma shule enzi za chama kimoja cha siasa na kuijua vyema historia ya nchi yetu, siku hiyo ilikuwa siku ya mashujaa kuwaenzi wale wote waliokufa wakipigania uhuru na heshima ya nchi yetu.

Nimetafakari mantiki ya Chadema kuichagua siku hii na kauli zinazotolewa na Rais John Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), naona nchi inaelekea kwenye mgongano ambao kama busara hazitotumika damu janga kubwa linaweza kutokea.

Kauli hizo ni kama ile aliyoitoa Rais akiwa mkoani Singida aliposema: “Wasije wakanijaribu, mimi ni tofauti sana na kama wapo watu wanawatumia wakawaeleze vizuri”.

Maana yake ni kwamba Chadema wanapoazimia kufanya mikutano ya hadhara nchi nzima wanamjaribu Rais kama atavitumia vyombo vya dola kuwadhibiti na yeye hayuko tayari kujaribiwa. Msimamo huu unapingwa kwa nguvu zote na Chadema kupitia Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salim Mwalimu, siku aliyozungumza na waandishi wa habari na kusema:

“Hatutorudi nyuma, mkakati wetu wa Septemba Mosi uko palepale”. Kwa kweli kwa kauli hizi naona giza kubwa linalinyemelea Taifa letu.

Kwa kuichagua Septemba Mosi, nadhani Chadema wanataka kutuma ujumbe kwamba wao wako tayari kuingia katika orodha ya mashujaa wa nchi hii, kwa maana kuwa wamejiandaa kutekeleza maamuzi yao hata ikibidi kujitoa mhanga.

Marufuku ya shughuli za kisiasa

Rais amepiga marufuku shughuli zozote zile za vyama vya siasa kufanyika nje ya maeneo ya wanasiasa husika. Akisisitiza hili , rais alisema: “siyo mtu unatoka Hai kwenda Kahama kushawishi watu wafanye fujo”.

Yako masuala kadhaa ya kujadili hapa. Kwanza, je katiba ya nchi au niseme sheria inasemaje kuhusu Mtanzania kutoka shemu moja kwenda sehemu nyingine kufanya siasa? Je, mikutano ya hadhara na maandamano ni fujo?

Jibu la swali la kwanza, Katiba ya nchi yetu inamruhusu Mtanzania kufanya shughuli za kisiasa mahali popote ndani ya nchi alimradi havunji sheria.

Ndiyo maana moja ya masharti ya kusajiliwa chama chochote kile cha siasa nchini ni lile la kuwa na wanachama kutoka pande zote mbili za Muungano na chama kisichokidhi matakwa haya ya kisheria kinaweza kufutiwa usajili.

Kwa hiyo kumzuia Mtanzania wa chama chochote kile kufanya shughuli za kisiasa ikiwa ni pamoja na mikutano ya hadhara na hata maandamano ambayo yanatambulika kisheria ni kumnyima haki yake ya kikatiba na ni kuvunja sheria.

Utawala wa sheria dhidi ya sheria za utawala

Sakata linaloendelea kati ya Serikali na Chadema ni kilelezo cha wazi cha kutamalaki kwa sheria za utawala, badala ya utawala wa sheria nchini Tanzania.

Katika nchi ya kidemokrasia, ainisho la utawala wa sheria linasema utawala wa sheria ni hali ya kuweko vizuizi vya kisheria kuzuia maamuzi ya kiimla na udhibiti wa kisheria kwa ajili ya kumlinda mwananchi na kuwepo utaratibu na uwazi wa kisheria.

Katika nchi yenye utawala wa sheria huwezi kukuta mgongano kati ya sheria na maamuzi au matamko ya viongozi.

Kwa mfano, huwezi kukuta sheria inaruhusu vyama vya siasa kufanya mikutano ya kisiasa, huku viongozi wanaweka mpaka wa mikutano hiyo kwamba ifanyike katika maeneo ya viongozi husika tu au nyakati za uchaguzi pekee.

Viongozi wa vyama vyote vya siasa wako huru kwenda mahali popote pale katika nchi kufanya shughuli za kisiasa iwe ni kukutana na wanachama wao katika mikutano ya ndani au kukutana na wananchi katika mikutano ya hadhara.

Si busara hata kidogo kuwazuia viongozi wa vyama vya siasa wa kitaifa au hata kama si wa kitaifa kwenda sehemu yoyote ya nchi kufanya siasa, kwa sababu hiyo ndiyo kazi ya viongozi na chama cha siasa.

Utawala wa sheria maana yake ni kuhakikisha kutumika kwa sheria kama zilivyokusudiwa na siyo kuzipa tafsiri waitakayo watawala. Kufanya hivyo ndiko kunakohakikisha kwamba haki za wananchi zinalindwa na haki za watawala pia zinalindwa.

Kinyume cha utawala wa sheria ni kile kiitwacho ‘sheria za utawala’au kwa Kiingereza; ‘Law of rule’. Hali hii hutokea pale ambapo utawala unatoa amri zake kinyume cha sheria hali ambayo hukaribisha upinzani kutoka kwa wananchi.

Tangu Rais Magufuli aingie madarakani, kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi wa kada mbalimbali kwamba nchi yetu imeanza kubobea kidogo kidogo kwenye sheria za utawala.

Wataalamu wa mambo ya sheria na katiba wanasema kukosekana kwa utawala wa sheria na kutamalaki sheria za utawala, ni hali inayoweza kujitokeza katika nchi zote, zile za kidemokrasia na hata zile za kidikteta.

Ndiyo maana wakaja na msamiati “dictatorial democracy” yaani demokrasia ya kidikteta au ya kiimla kwa lugha nyepesi. Kinachoendelea katika nchi yetu hii ya kidemokrasia ni sheria ya utawala badala ya utawala wa sheria.

Tunaweza kuepuka shari hii?

Kanuni ya kwanza ya mwendo ya Newton inasema: “kitu huendelea kuwa katika hali ya kupumzika au mwenendo endelevu isipokuwa kikilazimishwa kufanya vinginevyo na nguvu kutoka nje”.

Tulikuwa na hali ya utulivu kisiasa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2015, vyama vya siasa vikipigana vikumbo kufanya kazi ya siasa nchi nzima.

Hali hii sasa inaelekea kuingia dosari na kulitumbukiza Taifa katika machafuko yanayoepukika. Kwangu lawama zinastahiki kwa pande zote mbili, upande w Serikali na ule wa vyama vya upinzani.

Hali hii inayojitokeza ilijitokeza mara baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2010 pale Chadema ilipoitisha maandamano na migomo nchi nzima katika kile walichokiita ‘kuifanya nchi isitawalike’.

Kwa kiongozi wa Serikali yoyote ile hata kama wangekuwa wao Chadema, hakuna atakayenyamaza akisikia kuna watu wanataka kuifanya nchi isitawalike. Hapo nchi inaweza hata kuingia katika sheria ya utawala badala ya utawala wa sheria.

Tunapomsikia Rais Magufuli akisema “wasije wakanijaribu, mimi ni tofauti sana”, ningependa niwaase Chadema kwamba kweli Magufuli ni tofauti a na mtangulizi wake.

Hili ameshalieleza waziwazi hata kule Dodoma mara baada ya kukabidhiwa uenyekiti wa CCM. Kwa hiyo nasema si busara Chadema kuamua kumpima maana madhara yake yatakuwa makubwa.

Tofauti kati ya hali ile ya maandamano na migomo iliyojiri mara baada ya uchaguzi mkuu 2010, ni kwamba safari ile chokochoko zilitokana na wapinzani wenyewe lakini safari hii naona ni Serikali ndiyo inayowachokoza wapinzani.

Yaliyojiri bungeni kati ya Naibu Spika, Dk Tulia Ackson na wabunge wa upinzani, sakata la kufutwa matangazo mubashara ya Bunge na sasa kuifinya mipaka ya wigo wa mwanasiasa kufanya siasa zao ni uchokozi tosha wa Serikali kuwachokoza wapinzani.

Lakini hebu turejee kwa Chadema na vyama vingine vya upinzani. Hivi sheria zinapovunjwa na Serikali kwa kubinya haki za wananchi kama hii ya kufanya mikutano ya hadhara ya kisiasa na maandamano, wananchi wanatakiwa kufanya nini?

Nadhani sheria imetoa fursa ya kutafuta tafsiri mahakamani. Nimeshuhudia mahakama ikifutilia mbali kesi zilizofunguliwa na wagombea wa CCM dhidi ya wabunge na madiwani wa upinzani.

Ushauri wangu kwa Chadema ni kwamba nendeni mahakamani kwanza kudai haki yenu ya kufanya mikutano na maandamano. Kama ngazi zote za mahakama mtanyimwa haki yenu, hapo wafikirie mengine.

Hata mkifikia kuamua kuandamana na kufanya mikutano kwa nguvu na yakawakuta ya kuwakuta na mjue kweli yatawakuta, hapo mtaingia katika orodha ya mashujaa, vinginevyo mtakuwa mnaitumia siku ya mashujaa vibaya.

10 comments:

Anonymous said...

Umeandika mengi lakini lazima utambue kuwa kwa katiba tuliyonayo nguvu ya Raisi ni kubwa na Magufuli anatoa matamko hayo ndani ya mamlaka yake.
Pili, pengine hutambui ni kwa kiasi gani viongozi wa vyama vya siasa hutumika na powerful elites kuinfluence misimamo ya serikali especially serikali za kiaafrika.Raisi yuko well informed na kinachoendelea na ndio maana akasema "nendeni mkawaambie walio watuma kuwa mimi sijaribiwi".watakao athirika ni wananchi wanaochezeshwa ngoma wasiyoijua.TAFAKARI..

Anonymous said...

Chadema na waandishi wao na vyombo vya habari vinavyo wapigia debe wanajizonga kwani mpaka leo wameshindwa kutamka wazi au kutoa tangazo rasmi yakuwa wanamtambua John Maghufuli kuwa raisi halali wa watanzania sasa wewe mwenye akili yako timamu pima yupi hapa mwenye matatizo kati ya serikali na upizani?

Anonymous said...

Akili timamu ni kuwa wewe hapo juu una hitaji msaada wa kufukishwa milembe.. Sheria za Nchi ziko wazi zikimpa MTanzania uhuru wa kufanya mikutano ya kisiasa nchi nzima sasa Magufuli anatumia kifungu kipi cha sheria kama siyo ubabe wa kimamlaka?..Huyu Jamaa anaviashiria vya udikteta ..kwa hiyo unataka kutudanganya kuwa tatizo ni Ukawa kutomkubali kama Rais?..wewe unahitaji msaada wa kifikra..nchi yetu inatumbukia kusipojulikana sababu ya ulevi wa madaraka..iweje haki ya mikutano kwa nchi nzima iwe ya Rais pekee?..ebo!! Hivyo vyama vitajijenga lini?..kwa nini ni dhambi kumkosoa?..kwa nini bunge amelitia mfukoni?..fikiri kabla ya kuanika utumbo wako hapa ..kila mwenye akili timamu hawezi kuunga mkono upuuzi huu..tushindane kwa hoja siyo nguvu za kimamlaka!!

Anonymous said...

Chonde chonde Maguful. Nchi umeikuta salama na ikiwa na amani tele. Usituharibie nchi yetu tukawa na wakimbizi kama Somalia au Rwanda!!. Kama siasa hauziwezi kwanini usiendelee na chemistry yako???. Kwenye siasa kuna ushindani na pia kuna kukosolewa na kama hauyawezi hayo ACHANA NA SIASA KAFANYE CHEMISTRY.
Amani ya nchi si kitu cha kuchezeachezea namna hiyo na kutoa matamko ya jabza na mihemko bila kufuata katiba na sheria za nchi.Likisanuka hapo hata huo URAISI UTAKUSHINDA NA UTAKUWA KAMA MUGABE.
USHAURI WANGU,FUATA KATIBA NA SHERIA ZA NCHI NA HAKUNA MTU ATAYEKULAUMU.

Anonymous said...

Jamani tusidanganywe na hawa viongozi wa upinzani ambao sasa hawana ajenda. Naapa vikitokea vifo vyovyote vile hatokuwepo yeyote miongoni mwao. Uchaguzi umeisha. Wamwache Magufuli afanye kazi. Katika awamu hii ya maendeleo yetu tukitanguliza siasa hatuendi kokote. Hata nchi za Ulaya hazikuendelea kwa utawala bora. Watu wanahitaji kusukumwa ili kupigana na rushwa katika kutoa na kuboresha huduma. Haya ndio anayoyafanya Magufuli. Upinzani wanatafuta watakao toa damu ili wadai tulisema. Wasituharibie nchi. Wasubiri 2020. Sasa ni Kazi Tu.

Anonymous said...

Magufuli wape kichapo cha uhakika. Hiyo ndiyo lugha ya wapinzani Afrika wanayoielewa. Muda wa kampeni umekwisha. Anayedai Mirembe ataishia huko yeye mwenyewe.

Anonymous said...

Vilevile Sheria inasema wazi kuwa mikutano au mikusanyiko yote ni lazima ipate kibali cha polisi. Kwahiyo kwa sheria zilizopo hazimpi mtanzania uo uhuru wa kufanya mikusanyiko sio tu ya kisiasa hata ya kijamii,dini.

Anonymous said...

Kwa sheria tulizonazo,iwapo tarehe 1/9 yatafanyika maandamano na kwa namna yoyote raia wakapoteza maisha.basi ndio utakuwa mwisho wa kitu kinachoitwa Chadema na viongozi walio instigate maandamano hayo unaweza usiwaone uraiani kwa kipindi kirefu.- mark my word !

Anonymous said...

Mlizoea kupinduax2 JK.ambae nae alikubali kuchezewa sharubu kwakua nae alikuwa na mengi ya pembeni hakutaka yawe gumzo.This time mtanyooka tu.Watanzania tunataka siasa za maendeleo sio sarakasi zisizo na tija.

Anonymous said...

AT LEAST MAGUFULI ANAJITAHIDI KUTULETEA MAENDELEO, NYIE WAPINZANI MNAYO NJAA YA UTAWALA I.E "POWER HUNGRY". WANANCHI TUNAYO NJAA YA MAENDELEO. OKAY, KAMA CHADEMA NI WASOMI SANA NA MNAIJUA SANA SIASA, TUNAWAPA POLE SANA MAANA YAELEKEA MMESOMA LAKINI HAMJAELIMIKA, KWA SABABU SISI WAYONGE TUNACHOTAKA NI MAENDELEO (ECONOMIC DEVELOPMENT) NA SIYO MASS DEMOSTRATION NA MIKUTANO INAYOTUPOTEZEA MUDA WA KUFANYA KAZI ZETU. HATUNA MUDA WA KUPOTEZA KIJINGAJIMGA. THERE IS A DISCONNECT BETWEEN YOU FOLKS WASOMI WA CHADEMA NA SISI "COMMON PEOPLE" VIJIJINI, SISI TUNATUMIA MUDA WETU KULIMA, KUVUA SAMAKI, NA KUCHUNGA MIFUGO YETU, NYIE NA HIZO KAUNDA SUITS NA VIJITAI VYENU KAZI YENU KUBWA NI KUPIGA KELELE NA KUJIPENDEKEZA KWA WAZUNGU ULAYA NA MAREKANI. SAWA, MKAZANE KUZIPOKEA HIZO HANDOUTS TOKA NCHI ZA NJE, WANANCHI HATUTAKUBALI KUVURUGWA NA WACHACHE WENYE TAMAA YA VYEO. SISI VIJINI TUKO TAYARI KUWACHAPA VIBOKO KAMA MTALETA VURUGU ZA KUKWAMISHA MAENDELEO YETU. VIJINI SISI TUNAMMUUNGA MKONO JPM, MWENYEZI MUNGU AENDELEE KUMLINDA ILI NCHI YETU IENDELEE KIUCHUMI NA AMANI. WENYE NIA YAKUITAKIA NCHI YETU MAOVU, WATAKIONA CHA MTEMAKUNI.