Advertisements

Sunday, August 7, 2016

Kwaheri Yanga ya wanachama

Mwenyekiti wa klabu ya Yanga Yusuf Manji
By Oliver Albert, Mwananchi oalbert@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ni dhahiri wimbi la mabadiliko ndani ya klabu kongwe za soka, Simba na Yanga limeshika kasi baada ya jana wanachama wa Yanga kuridhia kwa kauli moja kuikabidhi timu yao kwa mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuf Manji ili aisimamie.

Uamuzi huo ulifikiwa ikiwa ni wiki moja tangu watani zao, Simba kupitia mkutano mkuu kukubali hoja ya kuuza asilimia 51 ya hisa za klabu hiyo kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘MO’ kwa Sh21 bilioni. Wakati hayo yakifanyika Yanga, wajumbe watatu wa kamati ya utendaji walifutiwa uanachama kwenye klabu hiyo.

Mageuzi mapya Yanga yalifikiwa kwenye mkutano mkuu wa dharura wa klabu hiyo, ambao Manji anayemiliki Kampuni ya Quality Group aliomba kukodishiwa klabu hiyo kwa miaka 10.

Alieleza kuwa asilimia 75 ya mapato itakwenda kwake na asilimia 25 ndiyo itabaki kwa klabu na baraza la wadhamini.

Katika mkutano uliofanyika kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam jana, Manji alisema anataka aisimamie Yanga kwa miaka 10 na kisha atairudisha kwa wanachama, huku akiahidi kuipa maendeleo, ikiwamo kuijengea uwanja. “Yanga hainunuliwi, lakini nipeni timu na nembo kwa miaka 10 na baada ya muda huo timu itarudi kwenu na jambo hilo litakuwa na faida kwani Yanga itakuwa na maendeleo makubwa.

“Katika miaka 10, asilimia 75 itakuwa yangu na asilimia 25 itakwenda kwa klabu chini ya wadhamini na hasara zote zitakuwa juu yangu,” alisema Manji.

Baada ya kusema hayo, wanachama walipiga makofi na kuridhia Manji apewe timu aiendeshe kwani ameifanyia mengi na ndiyo maana sasa hivi inawapa furaha kwa kutandaza soka safi.

Hata hivyo, baada ya wanachama kuridhia, ilikubaliwa suala hilo lipelekwe kwenye bodi ya wadhamini ili nalo litoe baraka.

Baraza la wadhamini la klabu hiyo linaundwa na Francis Kifukwe, Mama Fatma Karume, Jabir Katundu na Kapteni George Mkuchika.

Baraza kujadili

Kifukwe aliliambia gazeti hili jana kuwa, wanalichukua suala hilo na watakutana na wataalamu watakaowashauri kwa kuzingatia sheria za nchi.

“Hatuwezi kuzungumzia gharama kwa sasa, lazima tukutane na wataalamu watakaotushauri kitaalamu na kisheria ndipo tutajua tufanyaje,” alisema Kifukwe.

Mapato ya Yanga

Akifungua mkutano huo, Manji alisema kipato cha Yanga kwa mwaka hutokana na wadhamini, viingilio ingawa mara nyingi klabu imekuwa ikijiendesha kwa hasara.

Mwenyekiti huyo alisema udhamini wa Azam TV hauwanufaishi, huku Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likionyesha wazi kuikandamiza timu hiyo.

Manji alisema kwa mwaka wamekuwa na upungufu wa Sh1.5 bilioni kutokana na mahitaji ya klabu na hivyo kulazimika kukopa.

“Kipato kwa mwaka kutoka TBL (Kampuni ya Bia Tanzania) ni Sh500 milioni, mdhamini wa ligi, Vodacom Sh73 milioni, kipato kutokana na kuuza wachezaji Sh74 milioni, kipato kutokana viingilio kwa mwaka ni Sh678 milioni na hivyo jumla ni Sh1.3 bilioni.

“Jumla ya matumizi kwa mwaka kwa mishahara, usajili wa wachezaji, posho, gharama za usafiri na mengineyo ni Sh2.88 bilioni, hivyo tunakuwa na upungufu wa Sh1.5 bilioni, ambazo klabu inakopa kwa riba na imekuwa ikikopa kwa miaka 10 iliyopita na imeshindwa kulipa kiasi cha Sh11 bilioni,” alieleza Manji. Alisema mwezi huu, klabu inahitaji Sh500 milioni za kuendesha shughuli zake mbalimbali, ikiwamo mishahara za wachezaji, gharama za usajili na Sh88 milioni za udhamini mpya kutoka Quality Group.

Watatu wafutiwa uanachama

Katika mkutano huo, wajumbe watatu wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Hashim Abdallah, Ayoub Nyenzi na Salum Mkemi waliondolewa katika nyadhifa zao na kufutiwa uanachama kwa makosa mbalimbali. Manji alisema hayuko tayari kufanya kazi na wajumbe hao kwani ni kama mzigo kwake na kutaka wanachama wanaowataka wajumbe hao waendelee kubaki, wawapigie kura.

Hata hivyo, hakuna mwanachama aliyeinuka na kuonyesha kuwa wamebariki uamuzi wa kuwatimua. Mkemi alifutwa uanachama kwa kosa la kuzungumza na vyombo vya habari akidai mwenyikiti anawanyanyasa wanachama na kujiamulia mambo, wakati Hashim na Nyenzi, ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF walihusishwa na sakata la mapato katika mechi ya Yanga na Medeama.

Hashim ndiye pekee alihudhuria mkutano huo kati ya wajumbe hao watatu waliofutiwa uanachama na baada ya Manji kutamka kuwa amemfuta uanachama, aliinuka kwenye kiti na kuondoka ukumbini.

Yapata sare na Mtibwa

Wakati hayo yakiendelea, kikosi cha Yanga kililazimishwa suluhu na Mtibwa Sugar, katika mchezo wa jana wa kirafiki uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

No comments: