Advertisements

Wednesday, August 3, 2016

MADIWANI WA UKAWA WASUSIA KIKAO CHA PAUL MAKONDA KWA MADAI KWAMBA ANAWADHARAU

Madiwani wa Ukawa wa Manispaa ya Kinondoni wamesusa kikao kilichoitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa madai kiongozi huyo hana uhusiano mzuri na viongozi wa upinzani. 

Jana, Makonda aliitisha kikao cha wakuu wa wilaya, wakurugenzi, wakuu wa idara za manispaa za Temeke, Ilala na Kinondoni na madiwani wote, wakiwamo wabunge wanaounda halmashauri hizo.

Kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Arnaoutoglou kililenga kuzungumzia masuala mbalimbali, kama maeneo yaliyovamiwa na uboreshaji wa elimu mkoani Dar es Salaam. 

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, meya wa Kinondoni, Boniface Jacob alisema Makonda amekuwa na tabia ya kudharau na kutoheshimu viongozi wenzake, hasa wa upinzani akiwaona hawatendi kazi vizuri. 

Pia, Jacob alidai kuwa Makonda amekuwa na tabia ya kuingilia kazi zinazofanywa na viongozi wengine kwa kutumia cheo cha ukuu wa mkoa, jambo ambalo meya huyo alisema ni kinyume cha sheria. 

“Akitaka tumpe ushirikiano, Makonda abadilike la sivyo mtindo utakuwa huuhuu, mambo yatakuwa hivi. Huu ni mwanzo na ndiyo maana leo (jana) Ukawa Kinondoni tumekuwa na msimamo mmoja,” alisema Jacob. 

Jacob, ambaye pia ni diwani wa Ubungo (Chadema), alisema hawakuona umuhimu wa kwenda katika kikao hicho kwa sababu kiongozi wa mkutano huo anawadharau. 

Akijibu tuhuma hizo, Makonda alisema madiwani waliohudhuria kikao hicho maeneo yao yalikuwa na shida na yanahitaji kushughulikiwa, hivyo si kazi yake kuhesabu watu na kubaini nani hakufika mkutanoni. 

Alisema ajenda kuu ya kikao hicho ilikuwa ni kujadiliana namna bora ya kuvirudisha viwanja vilivyochukuliwa na kuvirejesha kwa matumizi yaliyokusudiwa. 

“Huyo anayelalamika mwambie huo anaoufanya ni utoto akikua ataacha. Narudia tena siyo kazi yangu kuangalia nani hajaja kwenye kikao,” alisema.

Kwenye kikao hicho, meya wa Ilala (Chadema), Charles Kuyeko alikuwapo kwenye mkutano huo pamoja na madiwani wenzake, sambamba na wale wa Temeke. 

Makonda si mgeni wa tuhuma .Aliteuliwa kuwa mkuu wa wilaya ya Kionondoni katika kipindi ambacho alikuwa akituhumiwa kuhusika kwenye sakata la kupigwa kwa Waziri Mkuu wa zamani, Jaji Joseph Warioba kwenye mdahalo wa Katiba uliofanyika Hoteli ya Blue Pearl. 

Katika kipindi hicho, Makonda pia alikuwa akituhumiwa kumrushia tuhuma za ufisadi Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa akiahidi kuwa CCM isingempitisha kugombea urais. 

Akitoa majumuhisho ya kikao cha jana kilichoanza saa 2:00 asubuhi hadi saa 5:00 asubuhi, Makonda aliwataka watu waliovamiwa na kujenga kwenye maeneo yasiyoruhusiwa, kuanza kubomoa majengo yao kabla ya Serikali kuwafikia. 

Kabla ya kutoa majumuisho hayo, Makonda alitoa nafasi kwa madiwani wa manispaa hizo kueleza kero zinazowakabili, hususan zinazohusu ardhi. 

“Najua mchakato huu utawagusa hadi vigogo, lakini mimi siogopi vita kwa sababu ndani yangu ninaongozwa na Mungu pekee,” alisema Makonda. 

Mbali na hilo, Makonda alisema endapo mtendaji wa ardhi atayebainika kuhusika katika kuchezea michoro na ramani ili aachie ardhi na kujipatia fedha, atashughulikiwa kwa mujibu sheria. 

Katika hatua nyingine, Makonda amemwagiza kamishna msaidizi wa ardhi wa Kanda ya Dar es Salaam, Mathew Nhange kumwambia Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi awaondoe maofisa ardhi na mipango miji wa Kinondoni na Ilala baada ya kushindwa kutoa taarifa za kuridhisha katika mkutano huo. 

Huku akiwataja maofisa hao wanaotoka Kinondoni na Ilala, Makonda alisema alishakutana na wakuu wa idara kwenye vikao vilivyopita, hivyo alitegemea kuwa watumishi hao wangetoa taarifa zilizokamilika. 

Kamishna naomba umwambie katibu mkuu mimi siwataki watumishi hawa katika manispaa hizi. Mwambie awatoe na kuwapangia kazi nyingine,” alisema Makonda. 

Kamishna Nhange alisema agizo hilo analifanyia kazi na kwamba atampa katibu mkuu taarifa za watumishi hao jana.

1 comment:

Anonymous said...

Sio kudharauliwa kususa ni moja ya sera yao ya maendeleo.