Advertisements

Saturday, August 20, 2016

MALAIKA MIHAMBO, MSUKUMA ANAYEFANYA KWELI OLYMPIC

RIO DE JANEIRO, Brazil

KILA wakati michezo ya Olimpiki inapofanyika, Tanzania tumekuwa na kawaida ya kutoka mikono mitupu, sababu nyingi zimekuwa zikitajwa huku kubwa ikiwa ni kukosa maandalizi ya kutosha.

Lakini kwenye michezo ya Olimpiki ya mwaka huu inayoendelea jijini Rio De Janeiro, Brazil, ghafla Wabongo walishtuka kuliona jina la Mihambo likigonga vichwa vya habari katika mchezo wa kuruka umbali mrefu.

Jina Mihambo ni la asili ya Kisukuma, lakini linatamba likiwakilisha Bendera ya Taifa la Ujerumani. Mwanadada Malaika Mihambo, aliyezaliwa Februari 3, 1994, amekonga nyoyo za wapenzi wengi wa mchezo wa kuruka kutokana na kufanya makubwa kwenye michezo ya Olimpiki ya mwaka huu.

Katika fainali ya kuruka umbali mrefu iliyofanyika juzi Jumatano, mrembo huyo mwenye umri wa miaka 22 tu, aliweka rekodi ya kuruka umbali wa mita 6.95 na kushika nafasi ya nne, nyuma ya Tianna Bartoletta wa Marekani aliyepata medali ya dhahabu (aliruka umbali wa mita 7.17), Brittney Reese wa Marekani pia (umbali wa mita 7.15) na Mserbia Ivana Španović (umbali wa mita 7.08).
MALAIKA MIHAMBO NI NANI?
Mrembo huyu ambaye ana rekodi kibao za kuruka na ambaye ni bingwa katika michuano kadhaa aliyoshiriki, ni Mjerumani mwenye asili ya Tanzania.

Baba wa mrembo huyu ni Msukuma wa Mwanza au Shinyanga lakini alihamia Zanzibar kwa shughuli mbalimbali za kimaisha, huko alikutana na mpenzi wa Kijerumani wakaanzisha uhusiano baadaye wakaenda kuishi nchini humo ambako Malaika alizaliwa.

Kutokana na kuzaliwa na baba Mtanzania, Malaika angeweza kuwa Mtanzania na kututoa kimasomaso (ingawa kwenye ardhi ya Bongo sidhani kama angeweza kwa kuwa Wabongo hatuna kawaida ya kujiandaa) lakini alichagua kuwa Mjerumani.
ALIVYOANZA FANI
Malaika alianzia mbali. Awali, alikuwa na fani nyingi; mfano alikuwa akicheza dansi, judo na michezo mingine kibao ya majukwaani, wakati huo alikuwa na umri wa miaka nane. Alipofikisha umri wa miaka 11 ndiyo akajikita rasmi kwenye mchezo wa kuruka.
REKODI ZAKE
Julai 2013 alifanikiwa kushinda Kombe la Michuano ya Vijana wa Ujerumani akiwa ameruka umbali wa mita 6.60, Juni 2015 akashinda Kombe la Vijana Wenye Umri wa Chini ya Miaka 23 Ujerumani, alimaliza nafasi ya tisa katika michuano ya Kombe la Dunia la Vijana 2011. Mwaka 2013 alitwaa medali ya dhahabu katika Michuano ya Vijana Ulaya na alimaliza nafasi ya nne mwaka uliofuata katika michuano hiyo.

Lakini hakuwahi kuruka umbali wa mita 6.95 kama alivyofanya juzi jijini Rio. Hivyo hiyo ndiyo rekodi yake kubwa kabisa.
Kwa ujumla, mara moja amewahi kutwaa medali ya shaba katika michuano ya Ulaya, mara moja amefika fainali ya michezo ya Olimpiki, mara moja amefika fainali ya Michuano ya Dunia, bingwa wa U23 Ulaya mara moja, bingwa wa vijana Ulaya mara moja, Bingwa wa Taifa mara moja na mara moja ameingia fainali ya michuano ya Ulaya.

NA KITABU AMEPIGA

Mrembo huyu amekuwa akifanya michezo pamoja na masomo kwa wakati mmoja. Ana digree ya Sayansi ya Siasa na Uchumi aliyopata katika Chuo Kikuu cha Mannheim, Ujerumani.

Habari kwa hisani ya GPL

No comments: