Advertisements

Tuesday, August 23, 2016

MBUNGE WA JIMBO LA TANGA KWA TIKETI YA CUF AKAMATWA TENA NA POLISI KWA KUTOA MANENO YA UCHOCHEZI

Mbunge wa jimbo la Tanga kwa tiketi ya chama cha wananchi CUF chini ya umoja wa katiba ya wananchi (UKAWA) Mheshimiwa Mussa Mbaruk amekamatwa na jeshi la polisi kisha kufikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Tanga kwa kosa la kutoa maneno ya uchochezi na chuki kwa jamii.

Akisoma shtaka linalomkabili Mheshimiwa Mbaruk mwanasheria wa serikali Saraji Iboru amedai mahakamani hapo mbele ya kaimu hakimu mfawidhi wa mahakama ya hakimu mkazi Hilda Lyatuu kuwa Agosti 13 mwaka huu katika eneo la madina lililopo kata ya Msambweni jijini Tanga Mussa Mbaruk alitamka maneno ya uchochezi na chuki kwa jamii hatua ambayo ingeweza kuhamasisha vitendo vya uvunjifu wa amani.


Akinukuu vipengele vya sheria kuhusu shtaka hilo mwanasheria wa mtuhumiwa Warehema Kibaha aliiomba mahakama hiyo impe dhamana mteja wake huku shauri hilo likiendelea kusikilizwa.

Kwa kuzingatia ombi hilo kaimu hakimu mfawidhi wa mahakama ya hakimu mkazi Hilda Lyatuu amemtaka mtuhumiwa kuwa na wadhamini wawili na kila mmoja awe na shilingi milioni 3 na mmoja wapo kati ya hao awe ni mtumishi wa umma masharti ambayo yalitekelezwa na kuachiwa huru hadi shtaka lake litakapo tajwa tena kesho Agosti 23 mwaka huu.

Chanzo: ITV

No comments: