Advertisements

Thursday, August 4, 2016

MKURUGENZI WA MASHITAKA (DPP) AWAFUTIA KESI YA RUSHWA KANGI LUGOLA NA WENZAKE

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam imewaachia huru wabunge watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliokuwa wanakabiliwa na mashitaka ya kuomba rushwa ya Sh milioni 30. 

Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage aliwaachia huru washitakiwa hao baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), kuwasilisha hati ya kuwafutia mashitaka.

Wabunge hao na majimbo yao katika mabano ni Kangi Lugola wa Mwibara mkoani Mara maarufu kama ‘Nyoka wa Shaba,’ Suleiman Saddiq ‘Murad’ (Mvomero – Morogoro) na Victor Mwambalaswa (Lupa – Songwe). 

Awali Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi akisaidiwa na Wakili Emmanuel Jacob kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), waliieleza mahakama kuwa kesi hiyo imetajwa kwa ajili ya washitakiwa kusomewa maelezo ya awali.

Kishenyi alidai mbali na kutaka kuwasomea maelezo ya awali washitakiwa hao, DPP anaomba kuwafutia mashitaka yao kwa kuwa hana nia ya kuendelea na mashitaka dhidi yao.


Baada ya maelezo hayo, Wakili wa Utetezi, Mpale Mpoki aliiomba mahakama itoe agizo ili apewe maelezo ya mlalamikaji. Hakimu Mwijage alisema, mahakama imekubali ombi la DPP hivyo kuanzia sasa wabunge hao wapo huru.

Aidha, alisema wakili Mpoki anatakiwa afanye juhudi kwenda katika ofisi za DPP ili kupata taarifa hizo, kinyume cha hapo mahakama haiwezi kutoa amri kwamba apatiwe maelezo hayo.

Baada ya washitakiwa hao kuachiwa huru, ndugu na marafiki wa wabunge hao waliokuwa wamefika mahakamani, walianza kuangua kilio cha furaha. 

Akizungumza kwa niaba ya wabunge wenzake, Lugola alisema watakaa na wanasheria hao ili wajue nini cha kufanya kutokana na udhalilishaji waliofanyiwa na Takukuru.

"Tumesikitishwa sana na kitendo cha Takukuru walivyotufikisha mahakamani na kutushitaki kwa kashfa ya rushwa na dunia nzima imetambua, lakini tangu tufike mahakamani mioyo yetu ilimtanguliza Mungu na leo (jana) Mungu ametoa majibu,” alisema Lugola.

Alisema walikuwa wanajua kuwa kesi hiyo ni ya kutunga na ilijaa siasa kwa kuwa awali Takukuru ilisema upelelezi umekamilika, lakini hawakuwa na ushahidi na ndio maana wameamua kuifuta.

Kwa mara ya kwanza wabunge hao walipandishwa kizimbani, Aprili mosi mwaka huu wakidaiwa kuwa Machi 15 mwaka huu, kati ya saa mbili na saa nne usiku, katika Hoteli ya Golden Tulip, Kinondoni jijini Dar es Salaam, kwa pamoja wakiwa kama wabunge na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), waliomba na kushawishi kupewa rushwa ya Sh milioni 30.

Inadaiwa waliomba fedha hizo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Gairo, Mbwana Magotta, kama kishawishi cha kutoa mapendekezo ya hati safi kwa halmashauri hiyo, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Kupandishwa kizimbani kwa wabunge hao kulitokana na kashfa ya rushwa iliyomsababisha Spika wa Bunge, Job Ndugai kupangua wenyeviti na makamu wenyeviti kwa kuwaondoa kwenye kamati walizokuwa wanaziongoza. Mabadiliko hayo yaliwagusa pia wabunge 27, ambao baadhi yao wanadaiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa.

No comments: