Advertisements

Sunday, August 21, 2016

MTU ALIYEFANYA KAZI NGUMU KULIKO ZOTE NCHINI AFUNGUKA

By Florence Majani, Mwananchi

Kifo kinatisha; kifo hakina huruma; kifo hutenganisha wapendanao, lakini kwa bahati mbaya, siku ikifika hakuna anayeweza kukikwepa.

Akionyesha hofu ya kifo alipokuwa na bendi ya Orchestra Makassy, Remmy Ongala aliimba kibao kinachoitwa “Siku ya Kufa”. Maudhui ya kibao hicho yalirejewa na Remmy mwenyewe japo kwa mahadhi tofauti alipojiunga na bendi ya Super Matimila. Huko alitunga kibao kiitwacho “Kifo Hakina Huruma”.

Kana kwamba ana uwezo wa kufanya majadiliano na kifo aliimba: “Kifo, kifo, siku yangu ikifika eeh, kifo niarifu mapema, niage wanangu, niage familia yangu yote, pesa zangu nizigawanye, zimebaki nizile mwenyewe, kifo nakusubiri kwa hamu.”

Mwanamuziki huyo, aliyefahamika zaidi kwa jina la Dk Remmy, alifariki dunia akiacha kifo kikiendelea kuchukua uhai wa mamilioni ya watu duniani katika mazingira tofauti. Baadhi hufa ghafla ajalini, wapo wanaofariki dunia baada ya kuugua, wengine huuawa na wenzao kwa hasira au kisasi au kwa bahati mbaya au bila kujua, lakini kuna wanaouawa kwa hukumu inayotolewa na vyombo vya haki; huhukumiwa kunyongwa hadi kufa.

Wanaopatikana na hatia ya kuua kwa kukusudia huhukumiwa kifo. Japokuwa kila nafsi itaonja mauti, wanaohukumiwa kifo ndio huweza kujua siku na aina ya kifo.

Hivi mtu akihukumiwa kifo na mahakama, je, wanaofanya kazi hiyo ni nani? Kitanzi kikoje? Hali inakuwaje kabla? Je, hupata fursa ya kuaga ndugu na jamaa? Wanaotekeleza hukumu ya kunyonga wenzao hadi kufa pia wanakuwa wametenda kosa la kuua, je, huchukuliwa hatua gani kisheria? Je, wanaoajiriwa kufanya kazi hiyo wanapatikanaje? Wanajisikiaje kukatisha uhai wa wenzao?

Lakini pia katika utumishi wao, ufanisi wao unapimwaje? Je, hupata utulivu wa moyo na amani kiroho?

Kwa kawaida kazi nyingi hutangazwa wazi magazetini na wale wanaojiona wana sifa zinazohitajika, huandika barua za kuomba na kusubiri kuitwa kwa mahojiano. Lakini, ni vigumu kukutana na tangazo la kazi hii ngumu kuliko zote.

Pia, najua kwamba baadhi ya kazi huhitaji wasomi wa kiwango cha juu, nyingine watu wenye ujuzi fulani lakini zipo zinazohitaji wenye nguvu.

Binafsi nadhani kazi hii inahitaji watu wenye moyo wa ujasiri ambao hawawezi kukosa utulivu wa moyo wala amani kiroho wakitekeleza jukumu lao kwa watu waliohukumiwa kifo.

Maswali hayo na mengine mengi nimekuwa nikijiuliza kwa siku nyingi na katika kufuatilia nililazimika kufunga safari hadi mkoani Dodoma ambako nilifanikiwa kumshawishi mtekelezaji wa hukumu hizo afanye mahojiano nami.

Saa 12.00 jioni, nikiwa na mwenyeji wangu wa Dodoma tulifika nyumbani kwa mtu tuliyekuwa tukimtafuta, Anangisye (siyo jina lake halisi).

Huyu ni askari mstaafu aliyefanya kazi Jeshi la Magereza kwa miaka 32 huku akitumia miaka 22 kufanya kazi hiyo maalumu ya kutekeleza hukumu za kifo.

Tulipokewa na mjukuu wake, ambaye alituambia kuwa babu yake aliondoka nyumbani tangu asubuhi. “Shuuuuu,” tulishusha pumzi ikiwa ni ishara ya kukata tamaa, lakini kijana yule alitusihi tuvute subira.

Kijana yule alitukaribisha ndani na wakati tunaingia mama mwenye nyumba, Matilda (pia siyo jina lake halisi) alitupokea na kutukaribisha sebuleni.

Tunaingia katika nyumba hii, ya matofali, ina vyumba vitano na sebule. Vyumba vitatu vimepangishwa na vingine vinatumiwa na Anangisye na familia yake.

Mimi na mwenyeji wangu tukaendelea kukaa sebuleni tukimsubiri Anangisye huku mama mwenye nyumba akituelezea jinsi jino linavyomsumbua.

Baada ya robo saa hivi, sauti ya mwanamume ilisikika nje huku mama mwenye nyumba na yule kijana wakisema, “huyoo”.

Alipokuwa anaingia sebuleni, sote tulisimama na kusalimiana naye huku tukikumbatiana kana kwamba tulifahamiana siku nyingi. Punde alimwita mjukuu wake na kumtuma dukani akatununulie soda.

“Mnasema mnataka kujua kuhusu kazi maalumu?” aliuliza Anangisye nami nikajibu, “ndiyo baba”.

“Mnanitafutia kazi nini maana nimestaafu tangu mwaka 2006,” alisema katika hali ya masihara.

Mara alibadilika na kusema kwa utani. “Lakini endapo itatokea kazi ya kunyonga niko tayari kufanya kwa sababu hakuna mtu yeyote anayeiweza kazi hiyo zaidi yangu,” alisema.

Anangisye ni mcheshi na mkarimu na wajihi wake ni mrefu, mnene, mwenye sauti nzito na anayependa masihara.

Baada ya masihara ya hapa na pale, Anangisye alianza kusimulia historia yake, alivyosoma, alivyopata kazi na jinsi alivyokuwa akitekeleza wajibu wake huo bila hofu.

Huku tukiwa tumetumbua macho na tukirekodi sawia maelezo yake, Anangisye alieleza kwa ufasaha kazi hiyo. Na hii ndiyo simulizi yake:

Mimi bwana ni mzaliwa wa Mbozi, sasa iko mkoani Songwe. Nilisoma hadi darasa la nane katika Shule ya Kati wilayani Mbozi. Mwaka 1974 niliomba kazi ya uaskari magereza. Nilipopata ajira nilipangwa gereza la Sengerema, Mwanza.

Huko nilifanya kazi kwa muda mrefu tu nikiwa askari wa kawaida wa magereza.

Mwaka 1984, yaani baada ya kufanya kazi kwa miaka 10 lilitolewa tangazo na Wizara ya Mambo ya Ndani kwamba anahitajika mtu kwa ajili ya kazi ya maalumu. Niliposikia tangazo lile bila wasiwasi wowote niliomba.

Basi, baada ya muda nikaitwa na Kamishna Mkuu wa makao makuu ya Magereza, Dar es Salaam. Nilipofika Kamishna akaniuliza: “Wewe ndiye Anangisye?”

“Nikamjibu, “ndiyo”.

Akaniuliza tena kama niliomba kazi maalumu na nikamjibu “ndiyo”.

“Basi umekubaliwa,” akasema.

Baada ya kuambiwa hayo nilielezwa zaidi kuwa Jeshi la Magereza limechagua watu wawili, yaani mimi na mwenzangu mmoja ambaye niliambiwa tutakutana Gereza la Isanga, Dodoma ambako kutakuwa kituo kikuu cha kazi yetu.

Niliambiwa kuwa kuanzia siku hiyo nitapelekwa Isanga na nitaripoti kwa RPO. Kwa hiyo nikawa nimeondolewa Sengerema.

Nilipofika Isanga nilitambulishwa kwa mwenzangu na nikaambiwa kuwa tupo wawili tu nchi nzima na tutafanya kazi hii maalumu pale inapotokea na maelekezo mengine tutaendelea kuyapata.

Tuliambiwa kuwa tutakuwa tunafanya hiyo kazi nchi nzima, tutakuwa tunazunguka mikoani pale ambapo kazi zitatokea.

Kozi ya kunyonga

Kitu cha kwanza baada ya kukubaliwa kupata kazi hii mimi na mwenzangu tulipewa mafunzo maalumu kwa muda wa mwezi mmoja palepale Isanga, tukafuzu, sisi wawili tu.

Mafunzo yetu yalihusisha namna ya kufanya kazi hiyo, namna ya kutumia kamba, mikanda ya kumshikilia mtu anayenyongwa pamoja na maandalizi yake.

Kuna namna ya kufunga kile kitanzi, ni lazima kiwe imara na salama ili yasitokee makosa. Lakini pia mikanda na eneo lenyewe na tulielekezwa jinsi ya kumweka mhalifu katika kitanzi chenyewe.

Katika ufanyaji kazi tulikuwa tunalindwa na askari magereza. Kwa mfano, siku ya kufanya kazi, tulikuwa tunasindikizwa na askari wakati wa kwenda na kurudi. Ilikuwa lazima tulindwe na ulinzi mkali wa askari ili isije kutokea tukapata madhara na kushindwa kutimiza wajibu wetu kwa sababu tulikuwa sisi wawili tu.

Kwa mfano, tulipotakiwa kufanya kazi Mbeya tulikuwa tunapewa ulinzi wa askari kutoka Dodoma hadi Mbeya na tulikuwa tunapewa huduma za hali ya juu za malazi na chakula ili tuwe na nguvu.

Kitu kingine ni kwamba ule usiku wa kuamkia siku ya kazi, tulikuwa tunapewa pombe. Mimi nilikuwa nakunywa bia aina ya Safari; basi unawekewa hata kreti zima, tunakunywa, tunakunywa hadi asubuhi.

Hadi ninapoamka asubuhi bado nakuwa na pombe kichwani; kabla ya kazi kuanza bado nakuwa na mning’inio wa pombe kichwani. Jambo hili lilikuwa linatusaidia sana kufanya kazi yetu vizuri na kwa ujasiri.

Mwisho wa mwezi tulikuwa tunalipwa mshahara mzuri tu na pia tulikuwa tunalipwa posho. Kwa wakati ule, kila tukitekeleza kazi tulikuwa tunapewa Sh700 kwa kichwa, baadaye katika miaka ya 1990 posho hii iliongezeka hadi Sh5,000 na baadaye miaka ya mwanzoni mwa 2000 tulipewa Sh50,000. Halafu nilikuwa na ofa ya kutofanya kazi nyingine yoyote.

Matanga kabla ya kifo

Unajua vifo vingine vyote hutokea ghafla, lakini kifo cha kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa kinajulikana. Mhalifu anajua kifo chake tangu siku anaposomewa hukumu yake ila anachosubiri ni kutekelezwa kwa hukumu hiyo basi.

Kwa utaratibu wa magereza, mhalifu aliyehukumiwa kifo, hutayarishiwa matanga siku moja kabla ya kunyongwa. Wanamweka katika chumba maalumu; kila mmoja kwenye chumba chake. Wanamfungia humo na wanampa chakula na huduma yoyote anayoitaka, hayo ndiyo matanga yake.

Wakati waliohukumiwa kifo wakiwa kwenye matanga, wafungwa wengine huimba nyimbo za maombolezo kama sehemu ya kuwaombea wenzao kabla kifo hakijawameza. Matanga hayo ni ya siku moja tu.

Atekeleza hukumu kadhaa

Nimesema nilianza kazi hii mwaka 1974 na nilistaafu mwaka 2006. Nimefanya kazi ya askari magereza kwa miaka 32 lakini pia nimefanya kazi hii maalumu kwa miaka 22. Nakumbuka kwamba katika kipindi changu cha kazi nimewahi kunyonga watu zaidi ya.. (kwa sasa hatutataja idadi).

Kabla ya kumweka kitanzini, mfungwa yeyote huwa na maandalizi yake. Viongozi wa dini zote mbili za Kiislamu na Kikristo huitwa, wanafika magereza na kuwaongoza wahalifu sala ya toba.

Huo ndio utaratibu. Wakishafanyiwa sala ya toba au kuongozwa sala yoyote ile inayofaa kabla ya kifo, huwekwa tayari kwa ajili ya kunyongwa.

Anakuwepo pia mwanasheria wa magereza au korona. Haiwezekani wakanyongwa bila ya kuwepo viongozi wa dini.

Hanyongwi mtu mmoja, inawezekana kwa siku moja wakawa watu wanane au kumi, inategemea na waliohukumiwa mwezi huo. Baada ya kutekeleza hukumu hiyo kwa mtu mmoja, nilikuwa naenda kupumzika kwa dakika 45 kabla ya kuendelea na kazi hiyo kwa mtu mwingine.

Kwa kawaida kazi huanza saa 2.00 asubuhi, baada ya kumaliza kazi tunakwenda kupumzika ofisini, tunakunywa kinywaji pale, baada ya dakika 45 tunarudi tena kuendelea na kazi.

Baada ya mapumziko ya dakika 45, tunakwenda kuangalia kama ameshafariki dunia, tukimaliza kuhakiki tunaendelea na wengine hadi waliopangwa siku hiyo wameisha. Kwa siku walikuwa watu wanane kutegemeana na idadi ya waliohukumiwa na kitanzi kinaweza kutumiwa na watu watatu kwa mpigo. Kwa hiyo, tukimaliza watatu, tunasubiri na kuendelea na kazi.

Kitanzi kilivyo

Kitanzi kilivyo ni kamba iliyoning’inizwa juu kwenye mbao katika eneo mfano wa chumba ambalo pia ni kama shimo. Anayenyongwa husimama juu ya mbao akiwa ameshikiliwa na kufungwa kitambaa cheusi usoni.

Sisi tunaingiza kitanzi kwenye shingo. Ubao huwa umeegeshwa na kazi yetu ni kufyatua kitufe mfano wa gia ya gari, na kikifyatuliwa humfanya huyo mtu kuning’inia na hapo kitanzi humkaba.

Sisi kazi yetu ni kufyatua tu kitanzi, baada ya mtu kuning’inia na kuhakikisha kuwa amekufa, tunaondoka. Askari wengine wana kazi ya kuitoa miili na kuipanga kwenye vitanda vilivyojengwa kwa sementi ambavyo vipo katika chumba cha kitanzi.

Baada ya kumaliza kazi yetu, kuna askari ambao wana kazi ya kuwatoa nje na kuanza shughuli za kuwazika, kazi ambayo hufanywa ikihusisha wafungwa wachache na askari tu.

Hii kazi haiwezi kuhusisha ndugu wa wafungwa, bali kundi dogo la wafungwa linatengwa kwa ajili ya kuhudhuria mazishi hayo.

Mashtaka kortini

Ingawa kazi hii maalumu hufanywa kwa mujibu wa sheria, baada ya kumaliza walikuwa wananipeleka mahakamani na kunisomea mashtaka kama muuaji mwingine yeyote. Lakini nilikuwa najibu kuwa mimi nimeua kwa mujibu wa sheria.

Baadaye utaratibu huo ulibadilishwa baada ya Serikali kuona kuwa kusomewa mashtaka mbele ya mahakama huku kukiwa na raia kunaweza kuhatarisha maisha yetu. Baadaye wakabadilisha nikawa nasomewa mashtaka mbele ya mkuu wa magereza tu.

Nikimaliza kusomewa mashtaka na mimi nilikuwa najitetea kwa kutumia vifungu vya sheria, basi naachiwa huru na kuendelea na kazi zangu.

Hapo nikaingilia na kumuuliza: “Ulikuwa huwaonei huruma?”

Huruma itoke wapi wakati tayari nimeapa na ninatelekeza kazi yangu kwa mujibu wa sheria? Wale watu mara nyingi walikuwa wanalalamika na kutoa maneno makali pale panapoanza kuwekewa kitanzi. Wanalalamika na kusema ‘sisi tunatangulia lakini hata ninyi mtatufuata tu’ ila sisi hatuzungumzi chochote tunatekeleza.

Nataka kazi tena

Sasa hivi nimestaafu tangu mwaka 2006, lakini endapo itatokea kazi hiyo niko tayari kufanya kwa sababu hakuna mtu yeyote anayeiweza kazi hiyo zaidi yangu. Hapa Tanzania nipo peke yangu mwenye ujuzi huu, kwa hiyo ikitokea kazi wakiniita mimi nafanya tu kwa sababu ni kazi kama nyingine.

Mwenzangu tuliyeanza kazi pamoja alifariki mwaka 2002. Huyu alikuwa na roho ngumu ikilinganishwa na mimi.

Kwa kweli inasikitisha, wafungwa wengine walikuwa wanawalilia wenzao siku moja kabla ya kifo chao. Lakini wafungwa pia hasa wale waliohukumiwa kifo, walikuwa katika hali mbaya zaidi kwa sababu walikuwa wanasikia jinsi miili inavyodondoka kwenye kitanzi na wakati mwingine sauti za maombolezo ya wenzao wakiwa kitanzini. Yule bwana (aliyekuwa anafanya naye kazi) alifariki dunia nikatafutiwa mtu mwingine, lakini hakuweza kuifanya kazi hiyo.

Ilitangazwa tena nafasi hiyo, akapatikana mtu mwingine akapewa mafunzo, lakini aliifanya ile kazi kwa siku moja tu, alikimbia na hakurudia tena kutokana na hofu ya ile kazi, akapangiwa kazi nyingine.

Hofu aliyokuwa nayo mwenzangu ni sawa na niliyokuwa nayo nilipoanza kazi hiyo mwaka 1984. Hakika siku ya kwanza kufanya kazi hii nilipata shida. Nilikuwa naweweseka. Wale watu niliowanyonga nilikuwa naona kama wananikimbiza kwa mashoka, wanasema ‘wewe umetuua wewe’ nawaona kabisa na sura zao.

Usiku wa siku ile ya kwanza sikulala nilikuwa napiga kelele hadi mke wangu akaamka. Hali hii ilinisumbua kwa kipindi kirefu. Wakati huo baba yangu alikuwa hai, nikamsimulia jinsi nilivyokuwa naweweseka usiku, baba alinisaidia kuzunguka na kuhangaika, hali ikatulia mpaka sasa nipo sawa.

Baba alinitia moyo akisema: “Mwanangu kazi ni kazi, bora mkono uende kinywani.”

Hata mke wangu hakupenda niifanye kazi hii, lakini baadaye nilipiga moyo konde na kuendelea.

Mwisho ni kilio changu serikalini. Jamani mafao ya kustaafu ni kidogo. Naiomba Serikali ituongezee kidogo na kutukumbuka.

Ilikuwa simulizi iliyojaa hisia tofauti kwetu na ilitufikirisha sana.

Waliohukumiwa kifo

Ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora iliyotolewa Mei 2015 ilionyesha kuwa kuna Watanzania 465 wanaosubiri kunyongwa magerezani.

Ripoti ya Mpango wa Kujitathmini Kuhusu Hali ya Utekelezaji wa Haki za Binadamu (UPR) unaotekelezwa kwa mara ya pili nchini, inaonyesha kuwa kuna mafungwa 465 wanaosubiri adhabu ya kifo, kati yao wanaume ni 445 na wanawake ni 20.

Historia ya hukumu ya kifo

Mwanasheria wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Harold Sungusia anasema hukumu ya kifo ilianzishwa wakati wa utawala wa Wajerumani.

Sungusia anasema hukumu hiyo iliendelezwa na Waingereza ambao waliitungia sheria mwaka 1932.

“Waliiboresha sheria hiyo mwaka 1945, na maboresho zaidi yalifanyika 1954. Lengo lilikuwa ni kuwanyamazisha wanaoingilia serikali,” anasema.

Sungusia anasema hata baada ya Tanganyika kupata uhuru, sheria hiyo iliendelea kutumika.

Anayataja makosa manne ambayo yanaweza kusababisha hukumu ya kifo kuwa ni kuua kwa kukusudia, uhaini, kuasi jeshini na makosa mengine ya jeshini.

Sungusia anasema wanaharakati wa haki za binadamu wanaipinga adhabu ya kifo kwa sababu mifumo ya kisheria ina udhaifu.

“Kutokana na mifumo yetu, hatuna uhakika kama anayehukumiwa ni kweli ametenda kosa. Wapo wengi waliohukumiwa kunyongwa, lakini wakashinda rufaa na sasa wapo huru,” anasema.

Sungusia anaeleza zaidi kuwa adhabu ya kifo imepitwa na wakati kwa sababu imejikita katika msingi wa ‘jino kwa jino’.

Hoja ya Sungusia inapata uzito kwa kuangalia hukumu kadhaa. Desemba 18, mwaka 2007, Jaji Frederick Werema aliidhinisha adhabu ya kunyongwa hadi kufa kwa Evelina Ngatala, mkazi wa Makambako, Njombe baada ya mahakama kumtia hatiani kwa kosa la kumuua bila kukusudia mtoto mchanga wa siku tisa.

Ngatala alidaiwa kumuua mtoto huyo kwa kumpa sumu ya kuulia wadudu wa kwenye nafaka.

Baadaye, mwaka 2011 Mahakama ya Rufani ilitengua adhabu ya kifo dhidi ya Ngatala. Wakili aliyekuwa akimtetea mshitakiwa huyo, Onesmo Francis aliiomba mahakama hiyo kumwondolea mteja wake huyo adhabu aliyopewa kutokana na ushahidi wa kimazingira uliokuwepo kutokidhi mahitaji.

Tofauti na Sungusia, mwenyekiti wa Chama cha Walemavu Tanzania, John Mlama anaunga mkono adhabu ya kifo kwamba inasaidia kupunguza mauaji ya kikatili hasa kwa walemavu wa ngozi.

“Watu wanadhamiria kabisa kuwaua watu wenye ulemavu, ninapata shaka kwa nini adhabu hii haitekelezwi,” anasema.

Mlama anasema adhabu ya kifo itawalinda wenye ulemavu na itapunguza mauaji, hivyo ni vizuri watawala wakaendelea kutekeleza adhabu hiyo kwa sababu hata mtuhumiwa anapofungwa kifungo cha maisha, bado Serikali inatumia gharama kubwa.

“Kwa nini hawanyongwi? Tatizo ni kamba, kalamu? Kama tatizo ni hivyo tuwakabidhi Serikali ili wawaadhibu wauaji wa albino,” anasema.

No comments: