Advertisements

Monday, August 8, 2016

MUHIMBILI KUANZA KUPANDIKIZA FIGO JANUARI


Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Profesa Lawrence Mseru

By Herieth Makwetta na Raymond Kaminyonge, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mzigo wa gharama ya Sh900,000 mara tatu kwa wiki kwa ajili ya kusafisha figo kwa wenye matatizo hayo, ‘dialysis’ utamalizika Januari wakati Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) itakapoanza kutoa huduma ya upandikizaji wa figo.

Kwa sasa wagonjwa wa figo wanategemea tiba hiyo kutoka kitengo cha usafishaji wa figo na damu (Renal Dialysis Unity) cha MNH, unaohusisha utoaji wa maji yaliyojaa mwilini, uchafu, pia sumu zitokanazo na vyakula au dawa.


Tiba hiyo ya dialysis ni ghali kwani mgonjwa hutakiwa kutoa Sh300,000 kwa mara moja, huku akitakiwa kuipata angalau mara tatu kwa wiki hivyo kumgharimu Sh900,000.

Akizungumza katika kipindi cha Funguka kinachorushwa na Azam TV, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Lawrence Museru alisema kwa kipindi chote wagonjwa waliokuwa wakihitaji tiba isiyopatikana nchini walikuwa wakipelekwa India kutokana na unafuu wa gharama.

Alisema huduma ya upandikizaji figo ni mwendelezo wa jitihada za hospitali hiyo kuhakikisha huduma hizo zinapatikana nchini baada ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na Kitengo cha Upasuaji wa Mifupa (MOI) kufanikiwa kwa asilimia 100.

“Wagonjwa wanaohitaji kupandikizwa figo wapo wengi Muhimbili, kwa sasa waliopo ni 100 kati yao wanahitaji kusafishwa na wengine asilimia 80 wanahitaji kupandikizwa, huduma hii imekuwa ikifanyika nje kwa miaka mingi,” alisema Profesa Museru.

Alisema tayari maandalizi yameanza kufanyika kwa utafiti, kinachosubiriwa kwa sasa ni timu ya wataalamu kwenda kwa mafunzo ya miezi miwili nchini India.

“Tumeamua kwamba ifikapo Januari mwakani tutaanza kutoa huduma hiyo, matarajio yetu Septemba mwaka huu timu ya madaktari bingwa watakwenda India kusoma na watakaporudi tutakuwa tayari tumeshafanya mabadiliko katika vyumba vya upasuaji na ICU, hivyo Januari huduma itakuwa tayari imeshaanza,” alisema.

Huduma kwa viziwi

Alisema huduma mojawapo wanayotarajia kuianzisha ni kupandikiza vifaa vya kusaidia kusikia inayotarajiwa kuanza Novemba.

Alisema mtoto anapozaliwa kiziwi anakuwa hawezi kuongea wala kusikia, lakini akiwekewa kifaa hicho ambacho kimeboreshwa hivi karibuni ataishi maisha ya kawaida kama wengine.

Profesa Museru alisema kifaa kitamsaidia mtoto kusikia na kujifunza kusema, hivyo ataweza kwenda shule ya kawaida kufanya kazi yoyote baadaye.

Alisema huduma hiyo imekuwa ikitolewa kwa watoto wengi kupelekwa nje, ambapo Sh100 milioni zimekuwa zikitumika kutibu mtoto mmoja.

Upatikanaji wa dawa

Profesa Museru alisema upatikanaji wa dawa katika hospitali hiyo ni wa asilimia 95.

“Tunahakikisha dawa zote zipo na zinapatikana na malalamiko ya wagonjwa yamepungua kwa kiasi kikubwa,” alisema.

Alisema ikitokea dawa anayehitaji mgonjwa imekosekana katika hospitali hiyo, idara ya famasia inachukua jukumu la kutafuta dawa na kumpatia mgonjwa.

Alisema kama Rais John Magufuli alivyoagiza watu wapate dawa kwa bei nafuu hivi sasa dawa zinapatikana.

Madaktari na hospitali binafsi

Kuhusu madaktari wa hospitali hiyo kutibu wagonjwa katika hospitali binafsi, Profesa Museru alisema ilitokana na madaktari kutolipwa masilahi yao kwa wakati.

Alisema kwa muda mrefu madaktari wa hospitali hiyo walikuwa na malimbikizo ya madai yao kwa sababu hawakuwa wakilipwa kwa wakati.

Alisema wengi walihamisha wagonjwa kutoka Muhimbili kwenda kwenye hospitali binafsi kwa sababu waliamini huko wangepata masilahi bora.

Profesa Museru alisema kati ya Machi na Aprili, hospitali hiyo ililipa malimbikizo yote ya madaktari na sasa wanalipwa kwa wakati.

Alisema waliona kutibu wagonjwa katika hospitali ya Muhimbili, wasingekuwa na uhakika wa lini watalipwa masilahi yao.

Maiti kuchanganywa

Profesa Museru aliwaomba radhi Watanzania kwa matatizo yaliyojitokeza hivi karibuni kwa kushindwa kukisimamia kitengo cha maiti na maiti mbili zikachanganywa.

Alisema katika matukio mawili tofauti, ndugu walipewa maiti ambazo si zenyewe na kusababisha usumbufu.

Alisema sasa kitengo hicho kitaimarishwa kwa kuweka wasimamizi watakaoshirikiana na ndugu kutambua maiti ili tatizo hilo lisitokee tena.

Hata hivyo, Profesa Museru aliwataka ndugu kuwa makini katika kutambua maiti za wapendwa wao ili kuepusha usumbufu unaoweza kujitokeza.

Wagonjwa wa rufaa

Alisema wagonjwa wanaotakiwa kufikishwa Muhimbili ni wale waliopitia utaratibu wa rufaa za hospitali za mikoa na kanda.

Alisema wagonjwa wanaotakiwa kufika katika hospitali hiyo ni wenye matatizo ambayo hayawezi kutibiwa katika hospitali nyingine.

Hata hivyo, alisema nusu ya wagonjwa wanaotibiwa katika Hospitali ya Muhimbili wanaweza kutibiwa kwenye hospitali nyingine.

Alisema hali hiyo husababisha msongamano usiokuwa wa lazima katika hospitali hiyo.

Alisema kuwa wanawake wasio na matatizo yoyote ya kujifungua hawatakiwa kufikishwa Muhimbili bali wanatakiwa kutibiwa katika hospitali nyingine.

“Labda hata huko kwenye hospitali za mikoa na kanda inawezekana zimezidiwa na wagonjwa ndiyo maana wanakuja Muhimbili,” alisema.

Ufisadi na rushwa

Alipoulizwa kuhusu ufisadi na rushwa, Profesa Maseru alikiri kuwa kumekuwa na malalamiko hayo, na kwamba kunapokuwa na idadi kubwa ya wagonjwa baadhi huamini ili kupata huduma ni lazima kutoa rushwa.

“Madaktari wetu na wagonjwa wanaelezwa kwamba rushwa hairuhusiwi katika hospitali hiyo na wanapothibitika kufanya makosa hayo wanachukuliwa hatua,” alisema.

Uhaba wa madaktari

Alipoulizwa kuhusu uhaba wa madaktari, Profesa Museru alisema kwa Tanzania daktari mmoja anatibu wagonjwa 18,000 wakati kwa viwango vya Shirika la Afya Duniani (WHO) daktari mmoja anatakiwa kutibu wagonjwa 10,000.

Alisema tatizo hilo litapungua kwa sababu sasa kuna vyuo vingi vinavyofundisha madaktari.

Migomo ya madaktari

Profesa Museru alisema hatarajii hospitali hiyo kuwa na mgomo wa madaktari, kwa sababu sasa kuna utaratibu wa kukaa na kuzungumza nao kuhusu uendeshaji wa hospitali hiyo na maslahi yao kwa ujumla.

“Kila mara tunazungumza ili kutatua matatizo yetu yanayotukabili na kufikia makubaliano, sitarajii migomo katika hospitali hii,” alisema.

No comments: