Advertisements

Monday, August 8, 2016

Olof Palme: Waziri Mkuu aliyeuawa mitaani akitoka sinema kwa miguu

UNAWEZA usiamini; waziri mkuu wa nchi anauawa mitaani akiwa anatembea kwa miguu kutoka ukumbi wa sinema na mkewe! Hilo lilitokea miaka 30 iliyopita wakati wasomaji wengi wa safu hii walikuwa hawajazaliwa ama walikuwa watoto wadogo.
Aliyeuawa alikuwa ni Olof Palme (majina yake kamili yakiwa ni Sven Olof Joachim Palme aliyekuwa Waziri Mkuu wa Sweden.

Palme alikuwa ni mmoja wa marafiki wakubwa wa aliyekuwa kiongozi wa nchi hii, Julius Nyerere na rafiki mkubwa wa mamilioni ya walimwengu waliokuwa wanapiga vita ukoloni, umaskini na kutetea amani kwa watu wote wenye fedha na wasiokuwa na fedha. Aliamini binadamu wote walistahili kufurahia kila alichokiweka Mungu duniani.

Alishutumu waziwazi uonevu wa mataifa makubwa dhidi ya mataifa madogo uliokuwa ukiongozwa na Marekani na Urusi ya Kikomunist. Aliyalaani kwa majina mataifa makubwa yaliyokuwa yanaanzisha vita kwa ajili ya kujinufaisha.

Kwa kifupi, alikuwa ni rafiki mkubwa wa Waafrika na maskini wengine waliojaa katika kona mbalimbali za dunia. Pendo la walimwengu kwake linaweza likalinganishwa tu na lile alilokuwa anapewa aliyekuwa kiongozi wa Afrika Kusini, marehemu Nelson Mandela.

Palme aliyezaliwa Januari 30, 1927, aliuawa kwa kupigwa risasi na mtu ambaye hajajulikana mpaka leo na lengo lake likiwa halijajulikana pia. Mpaka leo walimwengu wanajiuliza Palme alikuwa amekosa nini hadi kuadhibiwa kwa ‘mtindo’ huo. Ni kitendawili kinachoendelea mpaka leo.

Pamoja na wema wake wote huo, Palme, mume wa Lisbet Palme na aliyekuwa kiongozi wa Democratic Party, aliuawa usiku wa Februari 28, 1986 kwa kupigwa risasi kutoka nyuma na mtu aliyekuwa karibu nao, yeye na mkewe. Risasi ya pili ililengwa kwa mkewe, Lisbet, lakini bahati ilimkwangua mgogoni, akanusurika japokuwa ilimuumiza vibaya.

Ifahamike kwamba viongozi wa nchi za Nordic yaani Sweden, Norway na Finland huwa hawatii maanani sana kuwa na walinzi wakiamini nchi zao ni za wastaarabu na zenye amani.

Ndivyo alivyotoweka Olof Palme, kiongozi aliyekuwa na taswira ya kuvutia na kipenzi cha ‘malofa’ duniani, ambapo hadi leo hakuna aliyekamatwa kwa kumuua na kwa sababu ipi!

GPL

1 comment:

Anonymous said...

Kifo chake hakina tofauti na akina Patrice Lumumba, kwame, Sankara, Shavez wa venezuela, Arafat,hata nyerere pengine angetibiwa China angevuta umri kidogo. Sasa nadhani tukapata mwanga hapa nani alimua huyo mswidish?