Advertisements

Sunday, August 14, 2016

NDEGE MBILI ATCL KULETA MAPINDUZI

Bombardier Q400
By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Dar es Salaam. Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) limesema ujio wa ndege zake mpya mbili aina ya Bombardier Q400 utaleta mapinduzi makubwa kihuduma na kiutendaji kwa shirika hilo.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Patrick Itule amesema ujio wa ndege hizo utalirejesha shirika hilo kwenye biashara ya ushindani dhidi ya kampuni nyingine za ndege nchini.Ndege hizo zinazotengenezwa na Kampuni ya Bombardier ya nchini Canada, zinatarajiwa kuwasili nchini wiki ya tatu na ya nne ya Septemba, mwaka huu, zikipishana kwa wiki moja.

“Baada ya ujio wa ndege hizi hatuoni tena sababu ya sisi kukwama, tutakuwa tumeingia rasmi kwenye biashara ya ushindani kwa kuwa changamoto kubwa ya uhaba wa ndege ambao umekuwapo kwa miaka kadhaa, sasa itakuwa imeanza kutatuliwa,” alisema Itule huku akisisitiza kuwa shirika hilo halitakuwa tayari kuwavumilia wafanyakazi watakaoshindwa kuendana na kasi ya mabadiliko ya sasa.

Amesema shirika hilo limeunda kikosi kazi kinachosimamia mbalimbali, likiwamo la mafunzo ya watendaji wake ili waendane na matakwa ya biashara hiyo. Alisema uvutiaji huo utaambatana na utoaji huduma kwa gharama nafuu na alimshukuru Rais John Magufuli kwa jitihada zake za kulifufua shirika hilo.

Ofisa Biashara wa shirika hilo, Josephat Kagirwa alisema ndege hizo zina uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja na ujio wake utaongeza njia za kusafiri kutoka mbili za sasa na kufikia njia zaidi ya 10. Alitaja baadhi ya mikoa ambayo shirika hilo litaboresha safari zake kuwa ni Dodoma, Mwanza, Arusha, Mbeya, Kigoma, Tabora, Mpanda, Kilimanjaro, Mtwara, Zanzibar, Pemba, Bukoba na Visiwa vya Comoro. Hata hivyo, alisisitiza kwamba safari hizo katika maeneo yaliyotajwa na kwingineko zitaanzishwa baada ya kufanyika upembuzi yakinifu.

No comments: