ANGALIA LIVE NEWS

Monday, August 1, 2016

Pacha walitenganishwa kwa upasuaji wapata tatizo

Watoto pacha waliotenganishwa, Eliud na Elikana Mwakyusa (3) wakiwa nyumbani kwao.

By Godfrey Kahango, Mwananchi gkahango@mwananchi.co.tz

Watoto pacha waliotenganishwa, Eliud na Elikana Mwakyusa (3) ambao wazazi wao ni wakazi wa Kasumulu- Kyela, Mkoa wa Mbeya, licha ya afya zao kuimarika kwa kuweza kuzungumza, kula na kutembea vizuri, sasa wanasumbuliwa na tatizo la kutokwa na haja kubwa na ndogo bila ya wao kujitambua.

Watoto hao walizaliwa Februari 20, 2013 wilayani Kyela wakiwa wameungana kiunoni kabla ya kutenganishwa nchini India na madaktari bingwa kwa njia ya upasuaji. Serikali ilichukua jukumu la kuwasafirisha ili kupatiwa matibabu.

Baada ya kufanikiwa zoezi la kuwatengenanisha kwa njia ya upasuaji madaktari waliwatengenezea sehemu maalumu ya kutolea haja kubwa na ndogo eneo la tumboni na walirejea kijijini kwao Kasumulu Kyela, Februari 27, 2014.

Agosti 2014 watoto hao walipelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na walifanyiwa upasuaji mdogo wa kuziba haja kubwa na kuimarisha sehemu ya haja chini ya Daktari Bingwa wa Upasuaji Kitengo cha Watoto, Dk Zaituni Bokhary.

Dk Bokhary alifanikiwa kumrekebisha Eliud, lakini hakumfanyia upasuaji Elikana kutokana na afya yake ya wakati huo kutokuwa nzuri.

Hata hivyo, baada ya mwezi mmoja kupitia Elikana naye alifanyiwa upasuaji huo na jopo la madaktari wa Hospitali Rufaa ya Mbeya, wakiongozwa na Dk Bokhary na hatimaye kurejea kijijini kwao.

Akizungumza na gazeti hili jana, baba mzazi wa watoto hao, Erick Mwakyusa alisema watoto wake kwa sasa wanaendelea vizuri wakiwa na afya njema, lakini tatizo linalowasumbua ni kutokwa kwa haj azote mbili bila ya wao kujua.

Mwakyusa alisema aliwasiliana na daktari wao, (Dk Bokhary) kumweleza tatizo hilo alijibiwa kwamba huenda hali hiyo inatokana na matatizo yao, baada ya muda fulani itaacha lakini akawaahidi kwamba muda wowote atakapopata nafasi ya kuja Mbeya, basi atawafanyiauchunguzi ikiwa ni pamoja na kuziba sehemu ya haja ndogo na kuwatengenezea ya kudumu.

Mama wa watoto hao, Grace Mwakyusa alisema anamshukuru Mungu kwa kuona watoto wake wanakuwa na maendeleo mazuri ya kiafya, lakini tatizo hilo linamnyima usingizi kwani anashindwa kufanya shughuli nyingine mbali na nyumbani kwa sababu ya watoto wake hawezi kumuachia mtu yoyote.

“Kwa sasa nashindwa hata kufanya biashara. Hii hali ya wanangu kujisaidia bila ya kujitambua siwezi kuwaacha hata kwa jirani, inanibidi niwe nao karibu muda wote. Hivyo, tunamsubiri daktari aje kuwafanyia uchunguzi wa tatizo hili,” alisema Grace.

Alisema mbali na tatizo hilo, watoto wake wana afya nzuri na kwa kiasi kikubwa imeimarika na hawajawahi sumbuliwa kwa ugonjwa wowote unaoweza kuwafanya walazwe hospitalini.

“Pia, kama ni homa, basi ni za kawaida kwa watoto na wanapelekwa kituo cha afya ama zahanati wanatibiwa na kurudi nyumbani, japo hawaugui mara kwa mara,’’ alisema.

Maelezo ya Dk Bokhary

Akizungumza kwa njia ya simu na gazeti hili, daktari wa watoto hao, Dk Bokhary alisema upasuaji wa maeneo kama hayo mara nyingi yana changamoto. Hivyo hakushanga kusikia watoto hao wamepatw na tatizo hilo, lakini kinachohitaji ni wazazi wake kuwafanyisha mazoezi ya chooni ya muda mrefu.

”Watoto hao wanahitaji mazoezi ya kuwapeleka chooni. Wazazi ndiyo wenye wajibu wa kuwafanyia mazoezi mara kwa mara, hakuna njia nyingine. Walizaliwa wakiwa hawana sehemu ya haja kubwa wala ndogo hivyo kilichofanyika ni utaalamu wa kuwatafutia njia ya kudumu ya kutolea haja. Pia, upasuaji wa maeneo hayo una changamoto.

Dk Bokhary alisema anatambua watoto hao wamebakiwa na upasuaji wa haja ndogo na wanahitaji kufika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaamu ili awafanyie upasuaji huo, lakini kinachowakwamisha wazazi wa watoto hao ni gharama ya kuwasafirisha, matibabu na malazi wakiwa hospitalini hapo.

Alisema kutokana na hali duni ya kiuchumi ya wazazi wa watoto hao, anafikiria kuja Mbeya ili awafanyie katika Hospitali ya Rufaa Mbeya, lakini anashindwa kupata nafasi kutokana na shughuli zinazomwandama katika Hospitali ya Muhimbili.

Alisema, “Niliwaambia waje Muhimbili ili wafanyiwe upasuaji mdogo wa kuwawekea njia ya kudumu ya haja ndogo… lakini tatizo ni kwamba hawamudu gharama za usafiri, huku ni lazima kutakuwa na kuwatunza watoto hadi watakaporuhusiwa.”

“Ndiyo maana niliwaambia nitakuja Hospitali ya Rufaa Mbeya, ila sasa huku nimebanwa. Lakini ninafikiria kutafuta nafasi ile nije niwafanyie upasuaji huo,” alisema Dk Bokhary.

Dk, Bokhari alisema endapo wadau watajitokeza kuwasaidia watoto hao kufika Dar es Salaam, itakuwa jambo jema badala ya kumsubiria aje Mbeya siku ambayo hajui lini atapata nafasi.

Wazazi walonga kuwapeleka Muhimbili

Baba mzazi wa watoto hao, Mwakyusa alisema suala la kuwapeleka watoto wake Muhimbili anakwamishwa na kipato kidogo alichonacho kwani anaweza kufika Dar es Salaam, lakini hana sehemu ya kuishi. Pia, gharama za matibabu ni jambo ambalo limechelewesha kuwapatia matibabu watoto hao kwa wakati.

“Ninaweza kujikusanya kwa hiki kidogo ninachopata kwa kubeba abiria na pikipiki yangu, nikapata nauli ya kwenda Dar es Salaam, lakini shida ni kwamba tukiwa hospitalini hatutaweza kumudu gharama za pale. Sina ndugu yoyote kwamba nitafikia kwake, hatujui hospitalini tutakaa siku ngapi na gharama sitazimudu,” alisema Mwakyusa.

Alisema pikipiki ambayo alipewa msaada na Balozi wa Kenya nchini Tanzania ndiyo anaitegemea kumuingizia kipato. Usafiri huo aliupata baada ya balozi huyo kuguswa na taarifa ya watoto hao na maisha ya wazazi wao.

Anasema huwabeba watu muda wote na kujipatia fedha za kujikimu na familia, hivyo iwapo wataondoka kwenda Dar es Salaam, atalazimika kusimama biashara jambo litaongeza ugumu wa maisha.

1 comment:

Unknown said...

Mungu azidi kuwapa afya hao viumbe wa wake,