Advertisements

Tuesday, August 9, 2016

SAMIA AWAIBUA MAWAZIRI KUJIBU KERO


Makamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia kwenye kilele cha maadhimisho 23 ya Sikukuu ya Wakulima Nane Nane kwenye viwanja vya Ngongo mkoani Lindi Kilele cha maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima, Nanenane, kimehitimishwa kwa mawaziri wawili kusimamishwa jukwaani kutoa ufafanuzi kuhusu kero za wakulima nchini.


Maadhimisho hayo yaliyofanyika kitaifa mkoani Lindi, yalihitimishwa jana kwa hotuba ya mgeni rasmi Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, kuelezea kero alizokumbana nazo kwenye mabanda ya maonyesho ya wakulima aliyoyatembelea.
Samia alizitaja kero alizokutana nazo kwenye mabanda ya wakulima ni ukosefu wa soko, bei duni ya bidhaa, upungufu wa maghala ya kuhifadhi mazao, migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji na kodi ya chakula cha mifugo.
Kuhusu kodi ya chakula cha mifugo, Samia aliahidi kuwa Serikali itaangalia kwa undani suala hilo na namna ya kuiondoa, lakini alikatisha hotuba na kumwita Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kutoa maelezo.
Dk Mpango alipokwenda jukwaani alisisitiza aliyosema Makamu wa Rais Samia kwamba; “Naahidi maagizo yako kuhusu kodi ya chakula cha mifugo mtaona matunda yake muda si mrefu,”alisema Dk Mpango.
Hata hivyo, baada ya Dk Mpango kutoa maelezo yake, Makamu wa Rais Samia alimwita Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage kueleza mipango ya wizara yake na ambavyo wananchi watanufaika na fursa za uwekezaji.
Mwijage alisema tayari Serikali iko kwenye mchakato wa kujenga kiwanda kikubwa cha mbolea wilayani Kilwa mkoani Lindi. Alisema mradi huo wa mbolea unalenga kuzalisha tani 3,850 za mbolea kwa siku na unatarajiwa kutoa ajira takriban 5,000.
Awali, Samia aliziagia mamlaka husika kuhakikisha zinatenga maeneo kwa ajili ya wakulima na wafugaji ili kuondoa migogoro kati ya makundi hayo. Pia, alisema Serikali itashughulikia changamoto ya upatikanani wa soko lenye bei nzuri za mazao ya wakulima na upatikanaji wa maghala ya kuhifadhi mazao.

No comments: