Advertisements

Sunday, August 14, 2016

SERIKALI MKOANI SIMIYU YAAZIMIA KUWACHUKULIA HATUA WATENDAJI WANAOTOA TAKWIMU ZA UONGO

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka akizungumza na Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri za  Mkoa huo (hawapo pichani), katika Mafunzo elekezi yaliyotolewa kwa viongozi hao Mjini Bariadi kwa lengo la kuwajengea uwezo wa Kiutendaji
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini(kushoto) akitoa maelezo ya utangulizi kwa Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri za  Mkoa huo (hawapo pichani) kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa huo Anthony Mtaka (kulia) kufungua Mafunzo elekezi kwa viongozi hao
Baadhi ya Wajumbe wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka (hayupo pichani) wakati akifungua mafunzo elekezi kwa Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri za  Mkoa huo, yaliyotolewa kwa lengo la kuwajengea uwezo wa Kiutendaji.Mstari wa Kwanza kutoka kushoto Wakuu wa Wilaya,Tano Mwera (Busega), Seif Shekalaghe (Maswa), Joseph Chilongani (Meatu), Benson Kilangi (Itilima) na Festo Kiswaga (Bariadi).

Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Simiyu wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka (hayupo pichani) wakati akifungua mafunzo elekezi kwa Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri za  Mkoa huo, yaliyotolewa kwa lengo la kuwajengea uwezo wa Kiutendaji. Kutoka (kushoto) Kamanda wa Polisi Mkoa, Mkuu wa Usalama wa Taifa, Afisa Uhamiaji, Kamanda wa Zimamoto na Mkuu wa TAKUKURU
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka (wa pili kulia kwa waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na  Wakuu wa Vyombo Vya Ulinzi na Usalama Mkoa, Makatibu Tawala Wasaidizi, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri za  Mkoa huo, baada ya kufungua Mafunzo elekezi yaliyotolewa kwa viongozi hao wa Wilaya Mjini Bariadi, kwa lengo la kuwajengea uwezo wa Kiutendaji. (wa pili kushoto)Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini (kushoto)Mkuu wa Wilaya Busega, Tano Mwera na( kulia) Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga.


Na Stella Kalinga, SIMIYU
Serikali Mkoani Simiyu imesema haiko tayari kuwavumilia na kuwaacha katika vyeo na majukumu waliyonayo watendaji wanaotoa takwimu zisizo za kweli.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa mkoa huo, Mhe. Anthony Mtaka wakati wa ufunguzi wa mafunzo elekezi yaliyotolewa kwa Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa huo, yaliyofanyika jana Mjini Bariadi, kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kiutendaji, kwa kuwa baadhi ya viongozi hao wametoka katika sekta binafsi ambazo zina mifumo tofauti ya kitendaji na mfumo wa Serikali.

“Tunawezaje kukaa na Mtendaji ambaye ukimwomba taarifa za upungufu wa madawati anadanganya, idadi ya wanafunzi anadanganya, walimu anadaganya tutamchukulia hatua tu. Lazima tupeleke ujumbe kwamba taarifa za uongo hazina nafasi tena katika Mkoa wa Simiyu. Namwagiza Katibu Tawala Mkoa, aanze kuchukua hatua stahiki dhidi ya watendaji wote waliotoa taarifa zisizo za kweli  hususani katika takwimu za wanafunzi, walimu, madawati na vyumba vya madarasa”, alisema Mtaka.

Mtaka amesema azma ya Serikali Mkoani humo ni kuhakikisha Nafasi za watendaji wasio waadlifu zinajazwa na watumishi waadilifu, wenye sifa na elimu ya kutosha waliopo katika Halmashauri za Mkoa huo.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka viongozi hao wa Wilaya kubaini watumishi wenye sifa na uwezo wa kutekeleza majukumu ya Serikali katika maeneo yao na wawape fursa watumie talanta zao kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Pamoja na kubaini watumishi wenye sifa, viongozi hao wameelekezwa kuwachukulia hatua watumishi wanaopenda kufanya kazi kwa mazoea, ikiwa ni pamoja na kuwapangia majukumu yanayoendana na uwezo wao wa kufanya kazi.

Katika kuboresha ukusanyaji wa mapato, Mtaka ametoa wito kwa viongozi hao kuibua vyanzo vipya vya mapato na kusimamia ukusanyaji wa Mapato hayo kwa kuzingatia maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ya kutowabugudhi wananchi wanyonge na akawataka Wakurugenzi wa Halmashauri  kuhakikisha wanatenga asilimia 10 ya mapato yao ya ndani kwa ajili ya kuimarisha vikundi vya uzalishaji vya vijana na wanawake 
Sanjari na hilo Mtaka amewataka Viongozi hao wa Wilaya kutambua fursa za maendeleo katika maeneo yao na kuzitekelezafursa hizo kwa manufaa ya Wananchi walio katika maeneo yao.

Akizungumza baada ya mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe, Tano Mwera alisema mafunzo hayo yamemsaidia  kumpa mwanga na dira ya utendaji katika nafasi yake hasa katika utaratibu wa mawasiliano na mahusiano kati ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kwa Mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu za Nchi, Nafasi yake kama Kiongozi wa Serikali Wilayani pamoja na Sheria na Miongozo ya Vyombo vya Ulinzi na Usalama.

Mafunzo hayo ya siku moja kwa Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri ambayo yaliongozwa na Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini. yaliendeshwa na Makatibu Tawala Wasaidizi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama wa Mkoa huo.

No comments: