Advertisements

Sunday, September 18, 2016

ALIYEKUWA MKURUGENZI MKUU (NIDA) AKOSA DHAMANA ARUDISHWA RUMANDE

MAHAKAMA Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, imetoa masharti ya dhamana kwa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Dickson Maimu na wenzake watano, wanaokabiliwa na mashitaka ya kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 1.2.
Jaji Eliezer Feleshi, alitoa masharti hayo juzi baada ya kukubali hoja za maombi yaliyowasilishwa na washtakiwa hao. Hata hivyo baada ya kutolewa kwa masharti hayo, washtakiwa walirudishwa rumande baada ya kushindwa kuyatimiza.
Mbali na Maimu, washtakiwa wengine waliopewa masharti ya dhamana ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Joseph Makani, aliyekuwa Ofisa Usafirishaji, George Ntalima, na aliyekuwa Mkurugenzi wa Sheria, Sabina Raymond.
Wengine ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Bima ya Aste Insurance Brokers Company, Astery Mwita Ndege, aliyeingia mkataba na Nida wa kutoa huduma za bima na Xavery Silverius Kayombo, ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Gotham Internatianal Limited.
Akitoa masharti hayo, Jaji Feleshi alisema, Maimu alitakiwa kutoa dhamana ya Sh milioni 315.9, mshtakiwa wa pili Sh milioni 105.8, wa tatu Sh milioni 6.9, wa nne na watano kila mmoja Sh milioni 22.05.
Aidha, kila mshtakiwa anatakiwa kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika, wanaotakiwa kusaini hati ya dhamana ya nusu ya fedha zilizotajwa na Mahakama.
Aliongeza kuwa, washtakiwa hawaruhusiwi kusafiri nje ya Dar es Salaam bila kibali cha Mahakama pia wawasilishe hati za kusafiria kwenye ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na kila mmoja anatakiwa kufika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa muda na tarehe kesi itakapopangwa.
Awali washtakiwa hao, waliwasilisha maombi hayo na Mahakama iliyatupilia mbali, hata hivyo waliwasilisha tena maombi hayo. Washtakiwa hao wanadaiwa kutumia vibaya madaraka yao wakati wakitekeleza majukumu yao, kutumia nyaraka za uongo na kuisababishia mamlaka hiyo hasara ya Sh bilioni 1.2.

No comments: