Advertisements

Tuesday, September 6, 2016

GHARAMA ZA USAFIRI KUTOKA MBEZI LOUIS MPAKA UBUNGO ZAWA MWIBA KWA WANANCHI

Uamuzi wa Serikali wa kuzuia daladala zinazofanya safari kati ya Mbezi Louis na Mkoa wa Pwani kutofika Kituo cha Simu 2000 kilichopo Ubungo jijini Dar es Saalam umekuwa mwiba kwa wananchi wa maeneo hayo kutokana na kupaa kwa gharama za usafiri.
Baadhi ya wananchi waliohojiwa na gazeti hili wamesema tangu Serikali ilipozuia magari kufika katika kituo hicho wanalazimika kuongeza bajeti ya nauli kwa siku kwa wastani wa Sh500 tofauti na ilivyokuwa awali.
Awali, baadhi ya wananchi hao walikuwa wanatumia magari mawili kutoka Chalinze, Mlandizi, Ruvu na Kibaha kuingia jijini hapa, lakini sasa wanalazimika kutumia magari matatu mpaka manne kufanikisha safari zao.
Mkazi wa Kibamba, Erick Adolph amesema kwa sasa anapata shida ya kupata huduma muhimu kutokana na wingi wa abiria anaowakuta Kituo cha Mbezi, huku daladala zikiwa chache. “Ukitokea Kibamba, ukashuka Mbezi unatakiwa kupanda magari ya mwendokasi hadi Kimara, ukifika upande jingine mpaka Posta hapo unajikuta unatumia gharama kubwa inayokaribia Sh2,000 kwa hali ya kawaida watu wa kipato cha chini tunaumia,” alieleza Adolph.
Mkazi wa Kibaha mkoani Pwani, Amenye Andrew amesema licha ya mpango wa Serikali kuzuia magari hayo ili kupunguza foleni, ungewekwa utaratibu wa kuongeza mengine yatakayohudumia abiria wengi.
“Kutotumika kwa utaratibu wa mwanzo kunamaanisha abiria wengi watakosa magari ya kufika mjini, hivyo ni wakati mwafaka wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), kuweka utaratibu wa kulipia Sh800 kwa mabasi ya mwendokasi kutoka Mbezi hadi mjini,” amesema.
Amesema utaratibu wa sasa wa kulipia Sh400 kutoka Mbezi hadi Kimara na kisha kutoa Sh650 kwenda katikati ya jiji unawaumiza.
Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri wa Barabara wa Sumatra, Johansen Kahatano alisema inabidi wananchi wawe wavumilivu kwa kuwa mfumo ndiyo umeanza.
Ameongeza kuwa watazitatua ufumbuzi kero hizo ili abiria waweze wafurahie usafiri.
Kahatano ameongeza kuwa kero ya upandaji wa gharama za usafiri itashughulikiwa baada ya Sumatra kuanzisha safari mpya kutokea Kibamba mpaka Buguruni na Makumbusho.
“Kwa sasa kuna daladala zinazokwenda Makumbusho na zinakwenda Buguruni na baadhi Kariakoo na Muhimbili. Pia yapo mabasi ya mwendokasi, wananchi wawe na subira tu mambo yatakuwa mazuri,” amefafanua.
Mkurugenzi huyo alitoa rai kwa wananchi kutumia kadi za mabasi ya mwendokasi ili kupunguza gharama kwa kutozwa Sh800 kutoka Mbezi mpaka mjini, badala ya tiketi za karatasi.

No comments: