Advertisements

Thursday, September 1, 2016

JELA MIAKA 30 KWA KUMBAKA BIBI KIZEE

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kigoma, imemhukumu Omari Mzuzu (25), mkazi wa Kijiji cha Ilagala, wilayani Uvinza kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la ubakaji.
Mzuzu ametiwa hatiani baada ya kumbaka bibi mwenye umri wa miaka 70 na kumsababishia maumivu makali sehemu zake za siri.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Sylvester Kainda, alisema mahakama inatoa adhabu hiyo baada ya upande wa mashtaka kuthibitisha kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo.
Hakimu Kainda alisema mahakama hiyo inatoa adhabu kali dhidi ya mshtakiwa ili iwe fundisho kwake na vijana wengine wenye tabia ya kikatili kama yake.
Alisema upande wa mashtaka ulipeleka mahakamani mashahidi wane, ambao walithibitisha pasina kuacha chembe yoyote ya shaka kuwa mshtakiwa alimbaka bibi huyo, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Hakimu Kainda alisema bibi huyo alikuwa amelala na mjukuu wake usiku, mjukuu wake alitoka nje kwenda chooni na aliporudi alimkuta mshtakiwa huyo akimbaka bibi yake.
Alisema baada ya kuona bibi yake anabakwa, mjukuu huyo alipiga kelele na wasamaria wema walifika na kumkamata mshtakiwa kisha kumpeleka kwa mwenyekiti wa Kitongoji cha Ruguda.
Baada ya kumfikisha kwa mwenyekiti wa Kitongoji, walimpeleka kituo cha polisi Ilagala na kumhoji hatimaye walimfikisha mahakani ili sheria ichukue mkondo wake.
Kabla ya hukumu kutolewam mahakama ilimpa nafasi mshtakiwa kujitetea na ndipo alipodai kuwa alifanya tendo hilo si kwa utashi wake bali shetani alimdanganya na ni kosa lake la kwanza, hivyo kuomba apunguziwe adhabu.
Hakimu Kainda alitupilia mbali utetezi huo na kusema kitendo ulichokifanya mshtakiwa ni kikatili, kwa kuingia ndani ya nyumba usiku na kumbaka bibi huyo na kwamba huo ni unyama, kwa hiyo atakwenda jela miaka 30 ili akajifunze namna ya kuishi na jamii.
Awali, akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali Shaaban Masanja, alidai kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Febuari 28, mwaka huu, majira ya usiku.

CHANZO: NIPASHE

    No comments: