ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, September 29, 2016

Mapokezi ya viongozi CUF yaota mbawa



Katibu Mkuu wa Cuf, Maalim Seif Sharif Hamad
By Elias Msuya, Mwananchi

Dar es Salaam. Hofu ya kutokuwapo usalama ndani ya ofisi kuu za CUF Buguruni, imesababisha kuahirishwa mapokezi ya viongozi wakuu wa chama hicho.

Mapema jana, ilitangazwa kwamba Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, wajumbe wa baraza kuu la CUF na kamati ya uongozi ya chama wangefanyiwa mapokezi makubwa katika ofisi hizo lakini yaliahirishwa ghafla baadaye usiku kwa kuhofia kuwapo vurugu.

Kiongozi wa wabunge wa CUF waliokuwa wameandaa mapokezi hayo, Riziki Shahari alisema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kuwa wameahirisha mapokezi hayo baada ya kujiridhisha kuwa hali ya usalama siyo nzuri.

“Tunazo taarifa kuwa yapo makundi hatari ya watu yanayoishi ndani ya ofisi huku yakilindwa na vyombo vya dola tangu ofisi hiyo iporwe na aliyewahi kuwa mwanachama na kiongozi wa juu wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akishirikiana na watu wanaomuunga mkono.

“Tunajipa muda wa kushauriana na viongozi wa juu wa chama chetu huku tukiwaomba wanachama wote walioko Dar, mikoani na Zanzibar wawe watulivu kwani chama kina viongozi makini na hawawezi kuwa tayari kuona maisha ya wanachana na viongozi yanahatarishwa kwa kuigeuza ofisi kuu kuwa uwanja wa mapambano,” alisema Shahari.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro alisema wabunge 41 kati ya 43 wa CUF walioandaa mapokezi hayo walikuwa wamekwishafika Dar es Salaam, lakini wamechunguza na kubaini kuwa yangeleta maafa.


Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa CUF – Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alisema pamoja na hayo, chama hicho kimeshamalizana na Profesa Lipumba na kusisitiza kuwa si mwanachama tena.

No comments: